Habari za Punde

Maofisa utumishi watakiwa kuwa waangalifu na watendaji wanaohitimu masomo kuthibitisha vyeti vya

Na Salmin Juma, Pemba

Maofisa Utumishi wa Wizara na taasisi mbali mbali za Serikali Kisiwani Pemba, wametakiwa kutofumbia macho watendaji wao  wanaorudi masomoni na kuleta vyeti visivyo sahihi kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ya mishahara ili kuondosha kuitia hasara Serikali.

Hayo yalielezwa na Ofisa Mdhamini, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Pemba, Masoud Ali Mohammed, alipokuwa akibadilishana mawazo na Maofisa Utumishi hao  katika ukumbi wa Katiba na Sheria Pemba.

Massoud, aliwaeleza  Maofisa Utumishi hao kuondokana na muhali na kujiridhisha na vyeti vinavyoletwa na watumishi wanaotoka masomoni katika kuwapatia stahiki zao ili kuepusha msongamano wa kuangamizana na kutiana katika matatizo yasiokuwa ya lazima.

“Ndugu zangu maofisa utumishi nawaambieni ni wakati sasa wa kujitathmini tulikotoka na tonakokwenda tuangalieni wenzetu waliopita yaliowakuta tusifikire kwamba sisi tumefika hakuna atakaefumbia macho uovu tujihadhari na mapema yasijeyakatukuta na sisi matatizo”alisema Mdhamini.

Aliwaomba maofisa Utumishi hao waendelee  kutoa stahiki zinazopaswa kutolewa kwa watumishi wao tena kwa kuwa waangalifu sana na pia kuwaita watumishi katika kila Wizara na kuwapatia mafunzo elekezi ya kuwafumbua macho kwa yale yanayohusu masomo.

Kwa upande wake ,Ofisa Utumishi kutoka Tawala za Mikoa, Khadija Haroun, akichangia  mada alisema wameyapokea maelekezo hayo na watayafanyia kazi ipasavyo  kikubwa ni ushirikianao wa pamoja katika utekelezaji wa majukumu hayo .

Khadija, aliiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma na wao maofisa utumishi katika kuwapandisha kimaslahi  ili kuwakuza kiutendaji zaidi kwani nao wana mzigo mkubwa wa kusimamia wafanyakazi waliomo  katika taasisis zao.

Hata hivyo ,  Mohamed Juma Rashid ,Ofisa Utumishi  kutoka Wizara ya Habari , Utalii , Utamaduni na Michezo  Pemba, aliwaomba wakuu wa taasisi kuwa karibu nao wao maofisa Utumishi zaidi  na kusikiliza michango yao ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.