Habari za Punde

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein. Amesema Zanzibar Bila ya Vitendo Vya Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto Inawezekana Iwapo Iwapo Kutakuwa na Ushirikiano Kupiga Vita Vitendo Hivyo.


Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, akiwahutubiwa Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Kitaifa imeadhimishwa katika Mkoa huo katika viwanja vya Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.
---
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amesema kuwa Zanzibar bila ya vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto inawezekana iwapo kutakuwa na ushirikiano katika kuvipiga vita vitendo hivyo.

Mama Shein aliyasema hayo leo katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Koba huko Makunduchi Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika maelezo yake Mama Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kupambana na vitendo vya udhalilishjaji wa wanawake na watoto hapa nchini.

Alisema kuwa vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watotyo vinaendelea akusikika katika jamii, hivyo jamii ni lazima ishirikiane na Serikali katika kupiga vita vitendo hivyo.

Aliwataka wananchi kutowaonea aibu wala muhali wahusika kwa kutoa taarifa katika vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua.

Aidha, aalisisitiza jambo la kuzingatia ni kuiwa mabadiliko yanayosisitizwa katika ujumbe wa mwaka huu yaende sambamba na mikakati ya Serikali ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto kama ilivyoainishwa katika Mpango Kazi wa mwaka 2017 hadi 2022 dhidi ya vitendo hivyo.

Mama Shein alieleza kuvutiwa sana na ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu usemao “Wakati umefika: Tushirikiane kuleta mabadiliko ya wanawake vijijini”.

Alieleza kuwa ni dhahiri kuwa ujumbe huo umezingatia uhalisia uliopo katika jamii kwamba wanawake wanaoishi vijijini ndio wanaokabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleo kuliko wale wanaoishi mjini.

Mama Shein alitoa pongezi maalum kwa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba chini ya uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuchukua jitihada mbali mbali za kuleta maendeleo ya Wanawake.

Alieleza kuwa jitihada hizo ni pamoja na kurekebisha Sera na Sheria ili kuwawezesha wanawake kukabiliana vyema na changamoto mbali mbali ambazo zilikuwa zikipunguza kasi ya maendeleo ya wanawake katika masuala mbali mbali katika jamii.

Katika hotuba yake hiyo, Mama Shein aliwataka wanawake kutumia nafasi zao kuendelea kuhimiza amani na mshikamano kwani mambo hayo yakitoweka waathirika wakubwa huwa ni wanawake na watoto.

Vile vile aliwataka wanawake kushirikiana katika malezi bora ya watoto kulingana na maadili, silka na utamaduni wa Kizanzibari ili watoto wawe raia wema, wazalendo na wenye maadili na hofu ya MwenyeziMungu. 

Sambamba na hayo, Mama Shein aliwataka wanawake kutafakari maendeleo, changamoto na fursa za wanawake katika jamii na kuwakumbusha wanawake na jamii kwa jumla kuwa wanawake ndio nguzo ya familia.

Hivyo, ni vyema wakatambua kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika kuyatekeleza vyema majukumu yao na kusisitiza kuwa familia ikiimarika na kupata ustawi ndipo jamii nzima nayo hustawi na kupiga hatua za maendeleo.

Pia, Mama Shein alieleza kuwa ni vyema wakatambua kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika kuyatekeleza vyema majukumu yao na kusisitiza kuwa familia ikiimarika na kupata ustawi ndipo jamii nzima nayo hustawi na kupiga hatua za maendeleo.

Pia, Mama Shein alieleza kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kudhibiti maambukizo ya Virusi vyake kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huku akisisitiza kuwa Zanzibar inaungana na nchi nyengine duniani katika kumaliza maradhi hayo ifikapo mwaka 2030.

Pamoja na hayo, Mama Shein aliwataka wanawake kupeana moyo na kuzitumia fursa mbali mbali za kujiimarisha kiuchumi, ili kujiongezea kipato na kupambana na umasikini ikiwa ni pamoja na kujiunga katika vikundi vya ushirika wa aina mbali mbali ili iwe rahisi kwa Serikali na washirika wengine wa maendeleo kuwaunga mkono. Mapema Mama Shein alipata fursa ya kutembelea maonyesho ya vitu mbali mbali yaliyoandaliwa katika maadhimisho hayo.

Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Maudline Castiko alieleza juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wanawake wa Zanzibar wanapata haki zao za msingi huku akisisitiza azma ya Serikali ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatuma Kharib Bilal alisema kuwa ujumbe wa siku ya wanawake duniani umekuja wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Taasisi husika ikiwemo Wizara hiyo imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuleta mabadiliko kwa wanawake vijijini pamoja na kuondoa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Nao “UN Woman” ulipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwapa kipaumbele wanawake sambamba na kuwapa haki zao za msingi huku ukiahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Mapema akisoma risala ya Wanawake wa Zanzibar, Zawaadi Akida alieleza kuwa wanawake wa Zanzibar wamefurahishwa sana na mchakato unaoendelea wa kuhakikisha watendaji wa vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto hawana dhamana na kuzitaka vyombo husika kusimamia kwa makini ili kuinusuru jamii ya Kizanzibari na matukio hayo.

Alieleza kuwa wanawake wa Zanzibar wanajivunia mafanikio yaliyopatikana hapa Zanzibar hivi sasa ikiwa ni pamoja na kuwainua wanawake vijijini kwa kuwapatia na kuwaunganisha na fursa mbali mbali za maendeleo.

Wanawake hao walieleza kuwa vijiji vingi vya Zanzibar hivi sasa vimekuwa vikipata huduma mbali mbali muhimu zikiwemo afya, elimu, maji safi na salama pamoja na fursa za mikopo na taaluma za ujasiriamali kwa ajili ya kuinua hali za kiuchumi.

Zawadi alieleza kuwa pamoja na maendeleo yaliopatikana wanawake wa vijijini bado wanakabiliwa na changamoto ambazo zinarejesha nyuma maendeleo yao miongoni mwake ni ukosefu wa soko la uhakika kwa bidhaa wanazozizalisha, kukosa fursa za kumiliki rasilimali hususan ardhi pamoja na udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Hafla hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan, Makamo Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwaiba Kisasi na viongozi wengine wa Serikali na Mkoa huo ambapo Vikundi mbali mbali vya sanaa vilitumbuiza.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.