Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk. Shein Aipongeza Kampuni ya ZTE Kuunga Mkono Azma ya SMZ.


RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Kampuni ya Kimataifa ya Mitandao ya Kisasa ya Mawasiliano ya ZTE ya China  kwa kuunga mkono azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza Mradi wa Serikali Mtandao (e-Government) ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia na kuimarisha ufanisi wa utendaji Serikalini.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni ya Kimataifa ya Mitandao ya Kisasa ya Mawasiliano ya ZTE kutoka nchini China ukiongozwa na Makamo Mkuu wa Rais wa Kampuni hiyo Zhao Peng.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo na ujumbe wake kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhishwa na hatua za utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mradi huo wa Serikali  Mtandao (e-Goverment) na kueleza mipango inayoendelea katika kuanza awamu ya pili ya Mradi huo.

Alieleza kuwa tayari mchakato wa kuanza kwa awamu ya pili ya Mradi huo unaendelea kukamilishwa  ambapo utahusisha uanzishwaji wa Mfumo wa Huduma za Afya kwa njia ya Kielektroniki (e-Health)  pamoja na Uanzishwaji wa Mfumo wa Kodi (e-Tax).

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha ufanisi wa utendaji Serikali, utoaji wa huduma na upatikanaji wa taarifa za umma na kuimarisha matumizi ya (TEHAMA) kwa ujumla hali ambayo itaifanya Zanzibar nayo kuingia katika mabadiliko ya kiteknolojia kwa mafanikio makubwa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo haja ya kuwepo utaratimu na mfumo maalum wa kupata mafunzo kwa watendaji kutoka katika sekta hizo husika ili irahisishe utendaji wa shughuli hizo zitakapoanza.

Alieleza kuwa kwa vile teknolojia hiyo ni mpya na muhimu hapa nchini, hivyo suala la kupatiwa mafunzo kwa watendaji husika linapaswa kupewa kipaumbele huku akiipongeza Kampuni hiyo kwa mafanikio iliyoyapata na kuzivutia nchi nyingi duniani.

Nae Makamo Mkuu wa  Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Mitandao ya Kisasa ya Mawasiliano ya ZTE kutoka nchini China  Zhao Peng alimpongeza Rais Dk. Shein kwa ushirikiano mzuri uliopata kampuni hiyo katika kutekeleza majukumu yake kwenye awamu ya kwanza ya Mradi huo.

Alieleza kuwa makubaliano ya utekelezaji wa Mradi huo kwa awamu ya Pili ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Watu wa China chini ya Kampuni ya ZTE zimekubaliana kutoa fursa nzuri kwa Zanzibar kutumia mfumo wa Teknolojia ya kisasa (TEHAMA).

Kiongozi huyo alieleza matarajio yake kuwa Zanzibar itakuwa ni miongoni mwa nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati itakayokuwa na mafanikio makubwa katika mfumo wa Teknolojia ya Kisasa (TEHAMA).

Aidha, kiongozi huyo aliunga mkono wazo la Rais Dk. Shein la kutoa mafunzo kwa watendaji husika katika mradi huo na kueleza kuwa Kampuni yake imelichukua na italifanyia kazi ili kuona utekelezaji wake.

Mradi wa awamu ya pili wa Serikali Mtandao (e-Government) utahusika na ujenzi wa mfumo wa miundombinu ya mawasiliano “Access Network” ambao unakusudia kuleta ufanisi katika matumizi ya (TEHAMA) ambapo utapeleka huduma za mawasiliano katika majengo ya serikali pamoja na hospitali zilizoteuliwa na taasisi husika.

Pia, utahusika na mfumo wa huduma za afya kwa njia ya kielektroniki (e-Health) kwa  lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya hapa Zanzibar na kukabiliana na matatizo mbali mbali ambayo yamekuwa yakijitokeza katika utoaji wa huduma hizo pamoja na kupata vifaa kadhaa vitakavyosaidia kuimarisha utoaji wa huduma hizo.

Mradi huu unategemewa kuanzisha mfumo wa utunzaji wa taarifa za afya katika Hospitali zote kuu zilizopo Zanzibar ili kutunza kumbukumbu katika hospitali hizo.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mradi wa Serikali Mtandao (e-Government) imeona kuna haja kubwa ya kuwa na mradi utakaosimamia ukusanyaji wa Kodi za Zanzibar kwa mfumo wa teknolojia ya Habari na mawasiliano (e-Tax) ambapo lengo kuu la mradi huo ni kuiwezesha Serikali kukusanya kodi kwa kiwango kikubwa kwa njia salama na kwa ufanisi zaidi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.