Habari za Punde

Rais Dk Shein afunga Kongamano la Kitaifa la Utawala Bora na Uchumi Zanzibar









 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati)alipokuwa akifunga  Kongamano la Kitaifa la Utawala Bora na Uchumi Zanzibar lililofanyika jana katika  Ukumbi wa zamani wa  Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar (kulia) Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, [Picha na Ikulu],16 Machi 2018.  

Waziri asiyekuwa na Wizara maalum Mhe,Said Soud Said akionesha Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM wakati alipokuwa akitoa mchango wake wakati wa  Kongamano la Kitaifa la Utawala Bora na Uchumi Zanzibar lililofanyika jana katika  Ukumbi wa zamani wa  Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar, [Picha na Ikulu],16 Machi 2018.  



STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                 16.03.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwaeleza wananchi mafanikio makubwa yaliopatikana kutokana na juhudi za Serikali yao.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati akifunga Semina ya Utawala Bora na Uchumi katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Zanzibar, iliyowashirikisha viongozi wa Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Akifunga Semina hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa mafanikio yaliopatikana ni makubwa sana hivyo ni vyema wananchi wakaelezwa kupitia vyombo vya habari, wanasiasa na hata viongozi wa Taasisi na Wizara za Serikali pia, wanapaswa kuwaeleza wananchi mafanikio hayo.

Alieleza kuwa hatua iliyofikiwa ni kubwa sana hivyo ni vyema viongozi wakawaambia wananchi kwa kila ngazi kuazia Shehia, Wilaya, Mikoa na Serikali yote kwa ujumla kuwaeleza wananchi jinsi Serikali yao ilivyopata mafanikio kwani viongozi hao wana haki ya kuongea na wananchi sehemu yoyote.

“Kuna mambo mengine tunacchukua muda mrefu kuwaeleza wananchi  hivyo ni vyema tukatumia mbinu na vyombo vya habari na hata sisi wenyewe kuwaeleza wananchi mafanikio ya Serikali……kwa vyoyote vile hatua tuliofikia ni nzuri na tusione tabu kuwaeleza wananchi kwani sisi tunawajika kwao, ndio waliotuchagua”,alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa uchumi wa Zanzibar uko vizuri, hivyo ni lazima ukaendelezwa sambamba na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa viongozi wote kuwa na nakala za Mipango Mikuu ya Serikali katika ofisi zao pamoja na kutumia nakala za semina hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi kama ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu yao.

Alieleza matumaini yake kwamba mafunzo ya semina hiyo yatakuwa na mchango mkubwa katika kujenga kasi na hamasa za utendaji kwa viongozi hao pamoja na wale walio chini ya dhamana zao.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa kasi iliyofikiwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar tokea mwaka 2010 hadi hivi leo ni kubwa hivyo ni vyema ikaendelezwa na wananchi wakaelezwa.

Alieleza kuwa viongozi wote wanawajibika kwa wananchi hivyo ni vyema wakajua kuwa wananchi wanamataraji makubwa kutoka kwao na si vyema wananchi wakalalamika hatua ambayo inatokana na kutojua na kutoelezwa mafanikio yaliofikiwa na Serikali yao.

Nae, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib ambaye pia, ni Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango akitoa neno la shukurani kwa Rais Dk. Shein, alimpongeza kwa ushiriki wake katika Semina hiyo ya siku moja ambapo Dk. Shein ndiye aliekuwa Mwenyekiti wa Semina hiyo.

Waziri Salama alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, Waziri huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa kila kiongozi aliyeshiriki katika semina hiyo atalitekeleza agizo lake la kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata ikiwa ni pamoja na kwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili chama hicho kiendeleze ushindi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Akitoa mada juu ya “Mwenendo wa Uchumi wa Zanzibar Kuelekea Mwaka 2020”, Dk. Rahma Salum Mahfoudh alieleza kuwa katika kipindi hichi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Saba Zanzibar imepata mandeleo makubwa katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ambayo ni matokeo ya utekelezaji mzuri wa Dira ya Maendeleo, MKUZA na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Aliwasisitiza viongozi wote wa Serikali kwa kutumia dhamana zao walizopewa kuendelea na kasi hiyo na kuimarisha mashirikiano ili kufikia malengo yaliopangwa katika Mipango ya Maendeleo ambayo mingi ya Mipango hiyo inamalizika katika kipindi cha mwaka 2020.

Hata hivyo, alisisitiza haja ya kutumia uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo katika kipindi kilichopita ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika kipindi hiki kiliopo.

Nao viongozi hao wakichangia mada saba zilizotolewa katika Semina hiyo, walieleza mafanikio ya kiuchumi yaliopatikana hapa Zanzibar na kusisitiza haja ya kuendelezwa ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana.

Sambamba na hayo, viongozi hao walieleza kuwa siri kubwa ya mafanikio hayo ni kuwepo kwa mashirikiano pamoja na amani na utulivu hapa Zanzibar na kusisitiza kuwa hawatokuwa tayari kuwaona watu wachache wakitaka kuivuruga amani iliyopo.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.