Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong alipofika Ikulu Zanzibar leo kwa mazungumzo pamoja na Ujumbe aliofuatnana nao.09 Machi 2018.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein(kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong wakati alipofika Ikulu Zanzibar leo akiongozana na Viongozi mbali mbali wa Shirika hilo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein(kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong (wa pili kulia)wakati alipofika Ikulu Zanzibar leo akiongozana na Viongozi mbali mbali wa Shirika hilo ,[Picha na Ikulu.]
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kuiunga mkono Zanzibar katika
kutekeleza azma yake ya kuimarisha viwanda vidogo vidogo na vya kati ili kufikia
dhima ya uchumi wa viwanda na kukuza soko la ajira nchini.
Rais Dk.
Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Li
Yong Ikulu mjini Zanzibar.
Katika
maelezo hayo Rais Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi Mkuu huyo mikakati iliyowekwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya viwanda
inaimarika.
Dk. Shein
alimueleza Mkurugenzi Yong kuwa Serikali tayari imeandaa mipango na kutekeleza
mikakati ya kuimarisha sekta ya viwanda kwa kutambua umuhimu wake katika kuchangia
uchumi, kuimarisha sekta nyengine za uzalishaji na biashara, kuimarisha
upatikanaji wa bidhaa mbali mbali na kutoa fursa kubwa ya ajira.
Aidha,
Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana
ushirikiano na uhusiano mwema na wa muda mrefu kati yake na (UNIDO) na kuahidi
kuuendeleza.
Dk. Shein
alimueleza Mkurugenzi Mkuu huyo kuwa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka
2015-2020 imezielekeza Serikali zake mbili kuelekea katika uchumi wa Viwanda,
ili iwe ni ukombozi halisi wa kuwapatia fursa zaidi za ajira vijana sambamba na
kuimarisha uchumi wa Tanzania.
Alisema
kuwa hatua za UNIDO kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya
viwanda ina umuhimu mkubwa na itasaidia katika kufikia lengo lililokusudiwa.
Rais Dk.
Shein alisema kuwa miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha
kilimo kikiwemo kilimo cha mwani ambacho kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi
lakini bado kumekuwepo baadhi ya changamoto zinazokikabili kilimo hicho, hivyo
kuna haja kwa UNIDO kutoa ushirikiano wake katika eneo hilo ili kusaidia kilimo
hicho hasa kwa akina mama ambao ndio wengi wanaojishughulisha na kilimo hicho.
Aidha,
Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imezungukwa na bahari na pia, ni
mwanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA),
lakini bado haijazitumia vyema rasilimali zinazotokana na bahari kwa kutokuwa
na viwanda vinavyotegemea mali ghafi na rasilimali za bahari.
Hata hivyo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo hatua na
juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha Zanzibar inaanzisha
Kampuni yake ya Uvuvi na kueleza haja kwa UNIDO kuunga mkono jitihada hizo.
Rais Dk. Shein alimueleza Mkururugenzi Yong kuwa Zanzibar
inawakaribishwa wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda, vikiwemo
viwanda vya samaki na rasilimali za bahari.
Sambamba na hayo, alieleza kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa
na utajiri wa viungo vya chakula na kusisitiza kuwa iwapo vitaongezwa thamani
mafanikio makubwa yatapatikana huku akitumia fursa hiyo kueleza hatua
zilizofikiwa na Zanzbar katika kuimarisha Mfumo wa Teknolojia ya Kisasa
(TEHAMA), hatua ambayo itasaidia katika kuimarisha sekta ya viwanda.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Li Yong alimuhakikishia
Rais Dk. Shein kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuhakikisha inafikia malengo iliyojiwekea katika kuimarisha sekta ya viwanda.
Mkurugenzi
Li Yong alimueleza Dk. Shein kuwa UNIDO imeamua kwa makusudi kuiunga mkono
Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa kutambua kuwa tayari kuna mipango na mikakati
kabambe imewekwa katika kuimarisha sekta ya viwanda.
Aidha,
Mkurugenzi Mkuu huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa UNIDO itaendeleza uhusiano
na ushirikiano wake na Zanzibar na kupongeza mashirikiano mazuri yaliopo kati
ya Shirika hilo na Wizara ya Bishara na Viwanda ya Zanzibar.
Katika
maelezo yake Mkurugenzi Mkuu huyo alieleza haja ya kuimarisha teknolojia katika
kuimarisha sekta ya viwanda, biashara na masoko.
Alieleza
kwamba nchi nyingi duniani zimeweza kuwatafutia masoko wajasiriamali wake kwa
kuwawekea mkazo katika uendeshaji wa Biashara kwa njia ya mitandao. Kwa hivyo,
alisema kuwa itakuwa ni vyema ikiiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaweka
mkazo katika eneo hilo ili kuweza kukabiliana na changamoto ya kuwepo masoko ya
uhakikika ya bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa nchini.
Mkurugenzi
Mkuu huyo alimueleza Rais Dk. Shein mikakati aliyowekwa na UNIDO katika
kuhakikisha inaongeza miradi iliyopo sambamba na kuimarisha miradi iliyopo kwa
upande wa Tanzania Bara na Zanzibar na kuitaka Zanzibar kujiandaa vyema
kuipokea miradi hiyo
Kiongozi
huyo wa UNIDO alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Shirika hilo litahakikisha
linatoa kipaumbele chake katika kuiamrisha kilimo cha mwani ili kuhakikisha
akina mama wananufaika na kilo hicho huku akiahidi kuvifanyia kazi vipaubele
vyote vilivyowekwa na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya viwanda ili kwenda
sambamba na uchumi wa viwanda
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment