Habari za Punde

TRA: Wafanyabiashara Msiwaogope Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Msimamizi wa wiki ya elimu kwa mlipakodi katika Mikoa ya Kanda za Juu Kusini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Bi. Tubagile Namwenje akitoa elimu ya kodi kwa mteja aliyetembelea kituo maalumu kwa ajili ya wiki hiyo kilichopo katika Stendi ya Kabwe mkoani Mbeya. Wiki ya elimu kwa mlipakodi inafanyika nchi nzima na itamalizika tarehe 9 Machi, mwaka huu ikiongozwa na kaulimbiu isemayo "Karibu Tukusikilize na Tukuelimishe".
Afisa Mwandamizi wa Huduma kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Mkoa wa Mbeya Serapio Luanda akitoa elimu ya kodi kwa wateja waliotembelea kituo maalumu kwa ajili ya wiki ya elimu kwa mlipakodi kilichopo katika Stendi ya Kabwe mkoani Mbeya. Wiki ya elimu kwa mlipakodi inafanyika nchi nzima na itamalizika tarehe 9 Machi, mwaka huu ikiongozwa na kaulimbiu isemayo "Karibu Tukusikilize na Tukuelimishe".
Afisa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Mkoa wa Mbeya Evance Kiduko (wa kwanza kushoto) akitoa elimu ya kodi kwa mteja aliyetembelea kituo maalumu kwa ajili ya wiki ya elimu kwa mlipakodi kilichopo katika Stendi ya Kabwe mkoani Mbeya. Kushoto kwake ni Afisa Kodi Frank Tarimo wa TRA Mbeya.  Wiki ya elimu kwa mlipakodi inafanyika nchi nzima na itamalizika tarehe 9 Machi, mwaka huu ikiongozwa na kaulimbiu isemayo "Karibu Tukusikilize na Tukuelimishe". 
Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mbeya wakipata elimu ya kodi kutoka kwa Maafisa Kodi wakati wa wiki ya elimu ya mlipakodi inayofanyika katika Stendi ya Kabwe mkoani Mbeya. Wiki ya elimu kwa mlipakodi inafanyika nchi nzima na itamalizika tarehe 9 Machi, mwaka huu ikiongozwa na kaulimbiu isemayo "Karibu Tukusikilize na Tukuelimishe". (Picha zote na Veronica Kazimoto).

Na: Veronica Kazimoto. Mbeya,8 Machi, 2018.
Wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla wametakiwa kutowaogopa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwa watumishi hao wanafanya kazi kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria za Utumishi wa Umma na badala yake wametakiwa kuwa karibu nao ili kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayowakabili hususani yanayohusu kodi.

Hayo yamesemwa leo na Msimamizi wa wiki ya elimu kwa mlipakodi katika Mikoa ya Kanda za Juu Kusini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani kutoka TRA Makao Makuu Bi. Tubagile Namwenje alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya kuhusu mwitikio wa wananchi katika wiki ya elimu kwa mlipakodi.

"Inatakiwa walipakodi watambue kwamba, watumishi wa TRA ni maafisa wa Serikali na hakuna haja ya kuwaogopa kwa kuwa maafisa hawa ni watu wanaoisaidia nchi yetu isonge mbele na sisi sote tunataka nchi hii ipige hatua kimaendeleo," alisema Namwenje.

Namwenje alifafanua kuwa, lengo hasa la wiki hii ni kusogea karibu na wananchi pamoja na wafanyabiashara kwa ajili ya kuwaelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea mrejesho na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi hao.

Akizungumzia mwitikio wa wananchi mkoani humo, Namwenje alisema kuwa, mwitikio ni mzuri licha ya mvua za hapa na pale zinazonyesha lakini watu wengi wamefurahishwa na huduma zinazotolewa na TRA katika wiki hii ya elimu kwa mlipakodi.

"Mwitikio ni mzuri pamoja na kwamba mvua zinatusumbua kidogo lakini wananchi wanakuja kupata huduma kwenye vituo vyetu na hoja wanazoleta ni nzuri na sisi  tunawapatia ufafanuzi wa kutosha, alifafanua Namwenje.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Mbeya Davis Mongate alisema kuwa, mfanyabiashara yeyote ambaye anafanya biashara katika maeneo ambayo ni rasmi anatakiwa kusajiliwa na TRA kwa mujibu wa sheria.

"Kila mfanyabishara anayefanya  biashara katika maeneo rasmi ana wajibu wa kusajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa sababu hawezi kupata leseni bila kusajiliwa na TRA hivyo, ili aweze kupata leseni ya kufaya biashara katika Manispaa au Halmashauri hapa Mbeya ni lazima asajiliwe na Mamlaka na apate Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ambayo ni TIN kisha Afisa Biashara atampatia Leseni ya Biashara," alisisitiza Mongate.   

Naye mfanyabiashara anayefanya biashara ya mchele maeneo ya SIDO mkoani hapa Ester Ipembe alisema amefurahishwa na huduma aliyoipata kutoka kwa maafisa wa TRA na kuomba wafanyabiashara wenzake kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata elimu hiyo ya kodi.

"Mimi nilikuwa kwenye biashara zangu gafla nikasikia tangazo kwenye gari ikabidi nije, nimefika hapa nimepokelewa vizuri na nilikuwa nahitaji kueleweshwa zaidi juu ya makadirio ya kodi, nashukuru Mungu nimeelimishwa vizuri sana hivyo nawaomba wafanyabiashara wenzangu wajitokeze ili nao wapate elimu hii," alisema Ipembe.

Wiki ya elimu kwa mlipakodi inafanyika nchi nzima na itamalizika tarehe 9 Machi, mwaka huu ikiongozwa na kaulimbiu isemayo "Karibu Tukusikilize na Tukuelimishe".

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.