Habari za Punde

‘Utamu’ wamaliza meno ya watoto Zanzibar

Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi na Kati ya Uzi Khamis Omar Issa wa kwanza kulia Dawa pamoja na Miswaki kwa ajili ya Wanafunzi  katika matibabu ya kinywa na Meno yaliotolewa na Madaktari wa kujitolea kutoka Austria wakishirikiana na madaktari wazalendo katika Kijiji cha Uzi  Mkoa wa Kusini Unguja.kushoto ni Daktari dhamana kanda ya Unguja Dkt,Muhidini Mohammed.
 Daktari wa Kinywa na Meno kutoka Hospitali binafsi Dkt,Najat Abdalla akitoa mafunzo ya usafi wa kinywa na meno kwa Wanafunzi wa Skuli ya Msingi na Kati ya Uzi katika matibabu ya kinywa na Meno yaliotolewa na Madaktari wa kujitolea kutoka Austria wakishirikiana na madaktari wazalendo katika Kijiji cha Uzi Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Madaktari wa kujitolea kutoka Nchini Austria wakimpatia huduma kijana Mohammed Husein Mwanafunzi wa Skuli ya msingi ya Uzi ambae anasumbuliwa na Jino katika matibabu ya kinywa na Meno yaliotolewa na Madaktari hao katika Kijiji cha Uzi  Mkoa wa Kusini Unguja.

 Muakilishi wa Jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said akizungumza na Wanafunzi wa Skuli ya Uzi kuhusiana na  matibabu ya meno na Utunzaji wa Kinywa na meno katika matibabu ya kinywa na Meno yaliotolewa na Madaktari wa kujitolea kutoka Austria wakishirikiana na madaktari wazalendo katika Kijiji cha Uzi  Mkoa wa Kusini Unguja. 
Daktari dhamana kanda ya Unguja Dkt,Muhidini Mohammed,akizungumza na Waandishi kuhusiana na matibabu ya Kinywa na Meno yaliotolewa na Madaktari wa kujitolea kutoka Austria wakishirikiana na madaktari wazalendo katika Kijiji cha Uzi  Mkoa wa Kusini Unguja.

Na Salum Vuai, MAELEZO
IMEGUNDULIKA kuwa asilimia 80 ya wanafunzi wa skuli za Zanzibar, wanakabiliwa na matatizo ya meno ikiwemo kuoza na kutoboka.
Daktari dhamana kanda ya Unguja Muhidin Abdalla Mohammed, akiwa katika skuli ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja kutoa huduma za meno kwa wanafunzi, alisema kuwa hali hiyo husababishwa na ulaji wa mara kwa mara wa vitu vya sukari.
Ameitaja sababu nyengine kuwa ni, ama kutokupiga msuaki kabisa au kutokusafisha meno vizuri kwa utaratibu unaoelekezwa na wataalamu wa afya ya kinywa na meno.
Dk. Muhidin alifahamisha kuwa, watoto wanane kati ya kila watoto kumi, wanaugua meno, mengi yao yakiwa na matundu, hali aliyosema ikiachwa iendelee kuna hatari kwa watoto hao kupoteza meno mengi vinywani.
“Mathalan mtoto akipewa shilingi 100 kwao, basi ama atanunua pipi, chakileti, malai, juisi, kashata au vitu vyengine vyenye sukari. Na wakishakula, hawasukutui na hukaa bila kupiga msuaki hadi wanapoamka asubuhi kwa wale wanaopiga. Tabia hii inaozesha meno haraka,” alieleza.
Alisema, hali waliyoikuta katika skuli ya Uzi, inafanana na takriban skuli zote walizokwenda kutoa huduma kisiwani Unguja zikiwemo za mjini, akisisitiza haja ya kuwa na utaratibu maalumu wa kufanya ukaguzi kila baada ya kipindi ili kuwajengea watoto afya bora ya kinywa na meno.
Kwa ujumla, alisema elimu ya afya ya kinywa na meno visiwani Zanzibar, haijafikiwa kwa kiasi kinachohitajika.   
“Watoto wanapotiliwa dawa katika msuaki lazima wazazi wawasimamie kuhakikisha wanasafisha meno vizuri kwani wengine wanaweza kufyonza dawa na kusukutua, ikidhaniwa wamepiga msuaki,” alieleza Dk. Muhidin.
Akizungumza wakati wa zoezi la kutoa huduma na matibabu ya meno kwa wanafunzi wa skuli hiyo katikati ya wiki, Dk. Muhidin alisema uko umuhimu mkubwa kwa wazazi kuwasimamia watoto wao kikamilifu ili kuhakikisha wanasafisha vyema meno yao mara mbili kwa siku.
Mwalimu mkuu wa skuli hiyo Khamis Omar Issa, aliishukuru timu ya madaktari hao, akisema itasaidia sana kuwafundisha watoto mbinu bora za kupiga msuaki na hivyo kulinda afya ya meno.
Alikiri kuwa watoto wengi skulini hapo wana meno yaliyooza, akisema hiyo ni dalili kwamba hawafuati taratibu za afya ya kinywa na meno, huku akiwasisitiza wazazi kutimiza wajibu wao kwa kuwanunulia misuaki na dawa ili kunusuru afya zao.
Naye Mwakilishi wa jimbo la Tunguu aliyewaalika madaktari hao skulini hapo Simai Mohammed Said, alieleza kushtushwa kwake na takwimu za watoto wanaougua meno, akiwakumbusha wazazi kuangalia vyema afya za watoto wao na kuchukua hatua pale kunapojitokeza hitilafu.
“Meno ni miongoni mwa vitu muhimu kwa binadamu, yanapokosekana atashindwa kuchakua chakula vizuri, na pia akiwa na harufu mbaya ya kinywa atakimbiwa na watu na kukosa marafiki,” alieleza.
Alitumia nafasi hiyo kuiomba Wizara ya Afya kurejesha mpango wa kufikisha huduma na matibabu ya meno vijijini kwa kutumia gari maalumu (Mobile Dental) hasa katika vijiji vya mbali kama Uzi ambako kutokana na jiografia yake ya kujaa na kutoka kwa maji ya bahari, kunakosa kufikiwa.
Aidha, Mwakilishi huyo aligawa misuaki na dawa kwa ajili ya wanafunzi wa skuli hiyo, na kuwataka wazazi, vitu hivyo vitapomalizika wawanunulie vyengine.
Katika zoezi hilo lililoshirikisha madaktari wa kujitolea kutoka nchini Austria na wazalendo kupitia jumuiya yao (HIPZ), wanafunzi wa skuli hiyo walifanyiwa ukaguzi wa meno, na wale waliobainika na tatizo hilo walipewa matibabu ikiwa ni pamoja na kung’olewa meno.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
23 MACHI, 2018  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.