Habari za Punde

Wakala wa chakula na dawa ZFDA wazindua mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya elektroniki

Mkurugenzi Mtendaji ZFDA Burhani Othmani Simai akitoa maelezo mafupi kuhusiana na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa ZFDA, (ZFDA MANAGEMENT INFORMATION SYSTEM) katika hafla iliofanyika Hoteli ya GOLDEN TULIP Kibweni Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji TRADE MARK EAST AFRICA John Kulanga akichangia katika uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa ZFDA, (ZFDA MANAGEMENT INFORMATION SYSTEM) katika hafla iliofanyika Hoteli ya GOLDEN TULIP Kibweni Mjini Zanzibar.
Mtaalamu wa TEHAMA kutoka TRADE MARK EAST AFRICA Michael Mitheu akitoa maelekezo namna ya kujiunga na mfumo huo.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria wakifuatilia  namna Mfumo huo wa kielektroniki utakavyofanya kazi.
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akitoa hutuba yake katika uzinduzi huo.
Viongozi mbalimbali wakifurahiya mara baada ya uzinduzi kufanyika.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya ZFDA Mayasa Ali Salum akitoa neon la shukurani baada ya Uzinduzi huo.
Washiriki wa uzinduzi Mfumo wa Kielektroniki wa ZFDA, (ZFDA MANAGEMENT INFORMATION SYSTEM).Picha na Abdalla Omar Maelezo – Zanzibar. 

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar ZFDA umezindua mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya Kielektroniki ikiwa ni hatua muhimu ya kujiimarisha katika utoaji wa huduma zake kwa jamii.
Kufuatia uzinduzi huo Wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wataweza kununua na kuhakikiwa bidhaa zao kwa njia ya kimtandao bila hata kufika katika Ofisi za ZFDA.
Akizindua mfumo huo Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman amesema hatua hiyo ni muhimu kwa vile itawarahisishia wananchi wanaofuata huduma hizo Ofisini.
“Kwa hakika itapunguza gharama, na kuokoa raslimali fedha, muda na makaratasi. Kinachohitajika sasa ni uwepo wa internet tu” Alisema Naibu Waziri
Amesema kufuatia huduma hizo hakutokuwa na ulazima wa wananchi kwenda Ofisini badala yake huduma hizo watazipata kwa njia za kimtandao.
Naibu Waziri huyo amesema ZFDA kwa kiasi kikubwa imeimarika katika utoaji wa huduma na hatua hiyo imezidi kuipaisha hadhi yake na kuzidi kutoa huduma katika mfumo wa kimataifa.
Amesema Zanzibar kupitia ZFDA inaungana na nchi nyingine nne za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini ambazo tayari zimeshafikia hatua ya kutoa huduma kwa njia ya kimtandao.
Bi Harusi alitumia muda wake pia kuwanasihi Watendaji wa ZFDA kupambana na uzushi ambao hutolewa katika mitandao ya kijamii kuhusu bidhaa mbalimbali zinazoingizwa Zanzibar ambazo hazina viwango.
Aliwataka wananchi kutoa mashirikiano kwa ZFDA ikiwemo taarifa pale wanapokuwa na shaka kuhusu bidhaa zilizotengenezwa au kuingizwa nchini zikiwa chini ya kiwango.
Amesema Wananchi wana nafasi kubwa kuisaidia serikali kudhibiti ubora na usalama wa bidhaa kwa njia ya kuwataarifu ZFDA ili kubaini bidhaa duni na bandia kwenye soko.
Naibu Waziri huyo amewataka Watendaji wa ZFDA kuhakikisha kuwa mafanikio waliyoyapata yanakuwa chachu ya ufanisi kiutendaji ili kufikia dira ya Taasisi hiyo muhimu katika maisha ya Wazanzibari.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ZFDA Burhan Othman Simai amesema bidhaa zote zinazodhibitiwa na ZFDA ni bidhaa muhimu kwa maisha hivyo hawawezi kuruhusu bidhaa feki kuingia nchini.
Dkt Burhan alitoa wito kwa Serikali kuwajiri wafanyakazi wapya hasa wenye ujuzi wa TEHAMA ili kurahisisha utendaji kazi wa ZFDA
Aidha alishukuru mashirikiano anayoyapata kutoka kwa wadau mbalimbali na kusisitiza kuwa ushirikiano wa kila mdau ni muhimu ili kuhakikisha chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba katika soko la Zanzibar ni bora na salama kwa afya za wananchi wote.
Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Trade Mark East Africa John Kulanga alisema uboreshaji wa ufanisi na utendaji kazi utaongeza ushindani wa kibiashara na kuifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Amesema taasisi yao ilikuwa msitari wa mbele kuchangia mafanikio ya uzinduzi huo na kuahidi kuendelea kuinga mkono Zanzibar ili kupiga hatua zaidi. 
Kabla ya uzinduzi huo Wadau mbalimbali wakiwemo Wafanyakazi wa ZFDA na Wafanyabiashara walipatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo.
Hatua hiyo ya ZFDA kuzindua mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya Kielektroniki ni hatua muhimu ya kujiimarisha katika majukumu yake ya kusimamia udhibiti wa bidhaa za chakula dawa na vipondizi ambapo katika siku za karibuni ZFDA ilipatiwa cheti cha ithibati cha kimataifa ISO 9001;2015.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.