Habari za Punde

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na usafirishaji Pemba yatakiwa kuzifanyia matengenezo barabara

 Mhandisi Khamis Massoud akitoa maelezo ya kiufindi katika barabara ya Mangwena kuelekea Gando ambayo iliharibiwa na mvua za masika mwaka jana mbele ya Mshauri wa Rais Pemba Mauwa Abeid Daftari alipofanya ziara ya kuitembembelea barabara hiyo
 Hili ni eneo la barabara ya Mangwena ambalo hapo mwaka jana liliharibiwa na mvua za masika   
 Hili ni eneo la barabara ya Mangwena ambalo hapo mwaka jana liliharibiwa na mvua za masika   

Mshauri wa Rais Pemba Mauwa Abeid Daftari akieleza jambo mbele ya uongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Pemba wakati alipofanya ziara ya kutembelea barabara huko Mgelema
(PICHA NA SAID ABDULRAHMAN PEMBA

Na Said Abdulrahman  Pemba


Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na usafirishaji Pemba imeombwa kuzifanyia matengenezo ya haraka bara bara zote ambazo kwa sasa haziko vizuri.

Akizungumza baada ya ziara yake aliyoifanya ya kutembelea baadhi ya barabara za Kusini na Kaskazini Pemba,Mshauri wa Rais Mauwa Abeid Daftari, alisema ni vyema Wizara hiyo kuchukua hatua za makusudi ili kuzifanyia matengenezo ya haraka ili ziweze kupitika njia hizo katika kipindi hichi cha mvua zinazokuja.

Alifahamisha kwa upande wa barabara ya Kipapo -Mgelema alisema hali siyo mbaya sana ila kuna baadhi ya maeneo yanatakiwa kufanyiwa matengenezo madogo madogo ili  wananchi wa maeneo hayo waweze kusafiri bila ya usumbufu wowote.

“Madhumuni ya kutembelea maeneo haya ni kutokana na  sasa tunakabiliwa na mvua mkubwa,hivyo basi ziara hii itatupa muamko ni sehemu gani ambayo inatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka ili mvua zitakapokuja wananchi wetu wasipate shida ya usafiri,”alisema Mshauri huyo.

Mauwa , alieleza kuwa nia ya Serikali ni kuitengeneza barabara hiyo ya Mgelema kwa kiwango cha lami ,ila kwa sasa Wizara hiyo inamalizia kazi za maeneo mengine ambayo tayari wameshaanza.

Akizungumzia barabara ya Mangwena ambayo iliharibiwa na mvua za mwaka jana, Mshauri huyo alisema kwa sasa barabara hiyo ni hatari na hivyo aliwaomba wenye vyombo vya moto kupita katika njia iliyotengenezwa kwa muda ili kuwapa nafasi wajenzi kuishughulikia.    

“Kwa sasa tuwaombe wananchi wetu kuacha kutumia barabara hiyo hasa wale wenye vipando vikubwa ili kuwapa nafasi wenzetu wa Mawasiliano kufanya kazi zao kwa urahisi,”alifamisha Mshauri huyo.

Sambamba na hayo Mshauri huyo ,aliiomba Wizara hiyo kutengeneza mitaro ya maji na kuiweka usafi katika hali ya usafi. ili wakati wa mvua maji yaweze kwenda sehemu inayohusika.

Kwa upande wa barabara ya Chake Chake – Wete kongwe,alisema   tayari imo mbioni kutengenezwa kwani mambo yote yameshakaa sawa na kuwataka wananchi kuwa na moyo wa subra.

Kwa upande wake , Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Pemba, Ahmed Hamad Baucha alisema kuwa barabara ya Kipapo-Mgelema imo katika harakati za kujengwa kwa kiwango cha lami ila kwa sasa wanalizia barabara ambazo tayari wameshazianza kuzifanyia kazi.

Alifahamisha kwa upande wa barabara ya Mangwena ambayo iliharibika mwaka jana kwa mvua za masika,alieleza kuwa walikuwa wanasuburi majibu kutoka kwa wataalamu ambao wamechukua udongo wa hapo na kwenda kulifanyia vipimo ili kujua tatizo lake.
 Mshauri huyo wa Rais Pemba alitembelea Barabara ya Kipapo-Mgelema,barabara ya Chake Chake –Wete kongwe, barabara ya Mangwena, Kuungoni pamoja na kuangalia barabara ya kuingilia Ikulu ndogo Micheweni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.