Mkurugenzi
wa Vector Work Waziri Nyoni akijibu masuala alioulizwa na waandishi wa habari
katika mkutano huo (Picha na Abdalla Omar Habari – Maelezo).
Na Salum Vuai, MAELEZO
KIASI cha vyandarua
195,000 vilivyotiwa dawa ya kuulia mbu waenezao malaria, vinatarajiwa kugawiwa
kwa nyumba 38,884 Unguja na Pemba.
Akizindua kampeni ya kupambana
na malaria leo Aprili 4, 2018 katika uwanja wa Kisonge, Waziri wa Afya Hamad
Rashid Mohammed, amesema hatua vyandarua hivyo vitaelekezwa zaidi katika maeneo
yanayoonekana kuwa sugu wa maradhi ya malaria.
Hatua hiyo ni katika
mkakati endelevu wa kutokomeza malaria moja kwa moja, ambapo ugawaji wa
vyandarua hivyo umelenga zaidi kuwafikia akinamama wajawazito na watoto walio chini
ya umri wa miaka mitano.
Waziri Hamad amesema
dawa iliyotiwa katika vyandarua hivyo ina uwezo wa kudumu kwa miaka mitatu na
hivyo kusaidia maambukizi mapya ya malaria nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
wa ugawaji wa vyandarua hivyo, Waziri Hamad amesema kuwa malaria bado yapo na
juhudi za makusudi zinahitajika ili kuweza kuyatokomeza.
Amesema kuwa, wagonjwa 4,139
walithibitishwa kuugua malaria katika hospitali za Zanzibar mwaka 2017,
ikilinganishwa na wagonjwa 3,424 mwaka 2016 ambapo wagonjwa wanne walifariki
dunia mwaka jana kutokana na maradhi hayo.
Kwa mujibu wa Waziri
huyo, kiasi cha shilingi bilioni moja nukta tatu zitatumika katika kipindi cha
mwaka 2018 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo visiwani Zanzibar.
Amesema jukumu la
kumalizia maradhi hayo nchini halipasi kuachiwa Wizara ya Afya pekee, bali kila
mwananchi ana wajibu wa kutoa ushirikiano hasa katika kuweka mazingira safi ili
kuzuia mbu wa malaria kuzaliana.
“Inasikitisha kwamba
pamoja na juhudi za serikali katika kuilinda afya za wananchi wake, watu wengi
bado hawataki kubadilika kwani hata kusafisha mazingira ya majumbani mwao
wanaona ni kazi ya serikali. Hii ni hatari,” alieleza.
Aliwaomba wananchi
kushirikiana kwa pamoja katika kufukia madimbwi yanayotuwama maji kwa muda
mrefu kwenye maeneo yao badala ya kujipweteka wakitegemea nguvu za serikali.
Aidha
aliwataka wananchi watakaonufaika na vyandarua hivo kuvitumia katika njia bora
na salama ili viweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivokusudiwa.
Halikadhalika
aliwataka kuachana na kasumba zinazoenezwa na watu wasiokuwa na nia njema,
kwamba vyandarua hivyo pamoja na dawa za malaria zinazopigwa majumbani vinapunguza
nguvu za kiume na pia husababisha ugumba kwa wanawake, akisema huo ni uzushi.
Naibu
Meneja mradi wa malaria Zanzibar Faiza Bwanakheri Abbas alisema mpango wa
kumaliza malaria hautaweza kufanikiwa iwapo jamii haitajenga utaratibu wa
kuweka usafi katika maeneo yote yanayowazunguka.
Alisema kitengo
chake kimejiwekea utaratibu maalumu wa kupitia maeneo yote hatarishi na
kuwataka wananchi wajitokeze kusafisha mazingira yao.
Kiasi cha
shilingi bilioni 1.3 zinatarajiwa kutumiwa katika kipindi cha mwaka 2018 kwa
ajili ya kupambana na ugonjwa huo visiwani Zanzibar ukiwa msaada kutoka Shirika
la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID) na Mfuko wa Fedha wa Dunia (Global
Fund).
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment