NA/
ZUHURA JUMA, PEMBA
KUKOSEKANA
kwa huduma rafiki na ufaragha kwa baadhi ya vyombo vya sheria, kunakwamisha juhudi
za wanawake kupeleka malalamiko yao wakati wanapodhalilishwa kutokana na kuona
aibu.
Hali hiyo inapelekea kuongezeka kwa vitendo
vya ukatili kwa wanawake na watoto, kwani wao ndio wanaoathirika zaidi, ingawa
wanasuasua kuvifikia Vyombo vya sheria kuripoti pale wanapodhalilishwa,
kutokana kutokuwepo kwa huduma rafiki katika vituo hivyo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa
nyakati tofauti wanajamii wa shehia sita
zilizofikiwa wa Mradi wa kukuza Usawa wa Kijisia na kuwawezesha Wanawake
(GEWE), walisema ni vyema kwa Serikali kuweka wahudumu wanawake katika sehemu za
kupeleka malalamiko ya akinamama, ili kuweza kuelezea kwa uwazi yanayowakumba.
“Sehemu nyingi ukienda unawakuta wanaume tena
kwenye matatizo kama haya ya udhalilishaji, sisi kama wanawake tunahitaji
sehemu iliyofaragha tena kuwe na wanawake wenzetu, maana tunaona aibu”,
anashauri.
Sharifa Said Hamad (45) mkaazi wa shehia ya
Kangagani, alisema kuwa ili wanawake
waweze kuripoti baada ya kudhalilishwa, zinahitajika huduma rafiki katika Vyombo
vya sheria, kwani wanapomkuta mwanaume huona aibu na kushindwa kupeleka
malalamiko yake.
“Kwa kweli mtu anaona aibu, huku
ameshadhalilishwa, halafu anakwenda kwenye vyombo husika anawakuta wanaume, hii
inavunja moyo”, alisema mama huyo.
Nae, Mama mwenye umri wa miaka (30) mkaazi wa
Shengejuu ambaye mtoto wake (16) alibakwa mwaka jana, alieleza kuwa, mwanamke
anapodhalilishwa, wanaume wengine wote huwaona maadui, ambapo anapokimbilia
katika vyombo vya sheria na kumkuta tena mwanamme, huona aibu zaidi kuelezea
alivyodhalilishwa.
“Kesi
ya mtoto wangu sijui imefikia wapi, kwani tokea siku hiyo mimi sijaenda tena,
anakwenda mume wangu tu, na huyo mtuhumiwa juzi amebaka mtoto mwengine maeneo
ya hapa hapa mtaani, kwa kweli inaumiza”, alihadithia.
Nao, waratibu wa Shehia sita za GEWE, ambazo
ni Shengejuu, Mchangamdogo, Kinyikani, Kiungoni, Kangagani na Mjini Ole walieleza
kuwa, kuna baaadhi ya wanawake bado ni wagumu kuripoti kwa kile wanachodai
kuona aibu, ingawa baada ya elimu, wamekuwa wakiripoti angalau kwa waratibu.
Jumla ya kesi 20 wameripoti wanawake wenyewe
katika shehia hizo kuanzia mwaka 2015, hadi Oktoba mwaka jana kati ya kesi 51
za udhalilishaji walizopokea waratibu wa wanawake na watoto.
Mussa Suleiman Said, mkaazi wa Kinyikani, alisema
kuwa ni vyema katika maeneo ya kupeleka malalamiko ya wanawake, kuwepo na
wanawake wa kupokea malalamiko hayo, ili wasione aibu zaidi ya kile walichodhalilishwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji
Khamis Haji, alisema baadhi ya wanawake
wamekuwa wagumu kuripoti, jambo ambalo limesababisha kwa Wilaya ya Wete Dawati
la kijinsia Mkoa huo kupokea kesi 78
walizoripoti wanawake kati ya kesi 209 za udhalilishaji zilizofikishwa hapo
kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka jana.
Mratibu wa kituo cha Mkono kwa Mkono Wilaya
ya Wete, Asma Mohamed Fasihi, alisema wanawake wamekuwa wakipoteza ushahidi kwa
kushindwa kufika kwenye vyombo vya sheria kuripoti, ambapo alipokea kesi moja
(1) iliyofikishwa na mwanamke wenyewe mwaka 2015 hadi mwaka jana kati ya kesi
165 za udhalilishaji zilizofikishwa kituoni hapo.
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete, Haroub
Suleiman Hemed , alisema kwa upande wake wanawake huripoti kwa kiwango
kikubwa kesi za madai kuliko jinai na kuwataka wawe mstari wa mbele kutetea haki zao kwa
kufika katika vyombo vya sheria.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, sura ya
tatu kifungu cha 12 (3) kinaeleza ‘haki za raia, wajibu wa maslahi ya kila mtu
yatalindwa na kuamuliwa na mahakama pamoja na vyombo vyengine vilivyomo ndani
ya nchi… ’ ingawa wanawake wamekuwa wakijisahau kuripoti kesi za udhalilishaji
na kujiona hawawezi.
Mkataba wa haki za kimataifa wa kupunguza
aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake wa mwaka 1979, Ibara ya 2, inalazimisha
nchi wanachama kuchukua hatua madhubuti zinazofaa zikiwemo za kisheria kupinga
udhalilishaji dhidi ya wanawake.
Mratibu wa TAMWA, Mzuri Issa Ali, alisema udhalilishaji kwa wanawake na watoto bado upo
Zanzibar, hivyo wanajamii wawe tayari kudhibiti vitendo hivyo kwa kwenda
kuripoti na kuzisimamia ipasavyo kesi za matendo hayo.
Hata hivyo pamoja na elimu inayotolewa kwa
wanajamii katika kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, ingawa bado vinaongezeka
kutokana na baadhi ya wanawake kuona aibu kwenda kuripoti
No comments:
Post a Comment