Habari za Punde

Rais Dk Shein: Kuna kila sababu ya kumuenzi Marehemu Mzee Karume kwa kuikomboa ZanzibarSTATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                              05.04.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa kuna kila sababu ya kumuenzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kwa kuikomboa Zanzibar na kuwaachia Wazanzibari Serikali yenye mfumo madhubuti unaozingatia Utawala wa Sheria.

Dk. Shein aliyasema hayo, leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Kongamano la Kumbukumbu ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, huko katika ukumbi wa Chuo hicho Bububu, Wilaya ya Magharibi “A”, Unguja.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa bado wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla wanathamini sana hekima, busara na misingi imara ya maendeleo aliyowaachia Mzee Karume.

Alisisitiza kuwa Zanzibar itabaki kuwa na Serikali madhubuti ya kidemokrasia yenye utawala wa sheria kama ilivyoasisiwa na Mzee Karume ambaye alikuwa kiongozi mstahamilivu na ambaye alifuata falsafa ya kuwa ustahamilivu na uvumilivu sio udhaifu bali ni sifa ya uongozi

Alieleza kuwa mchango Mzee Karume kwa maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla ni mkubwa sana na hapana atakayethubutu kulikanusha jambo hilo yakiwemo Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo kila mmoja anafaidika.

Rais Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa mambo muhimu aliyoyasisitiza Mzee Karume ni kwua Zanzibar lazima iwe na wataalamu wazalendo wenye uwezo na ujuzi wa kutosha na wenye kujiamini katika kupanga na kusimamia mipango ya maendeleo.

Dk. Shein aliongeza kuwa Mzee Karume alichukia sana ubaguzi wa kidini na kusisitiza kuwa katika kumuenzi kiongozi huyu ni vyema wananchi wakaendelea kuepuka ubaguzi wa kidini na badala yake waendeleze upendo miongoni mwao pamoja na kuheshimiana.

Katika suala zima la uwajibikaji na ufuatiliaji wa kazi, Dk. Shein alisema kuwa Mzee Karume aliongoza kwa kuonesha njia na kuzikagua kazi zinazifanywa na kutoa maelekezo ili kuongeza ufanisi kwani pia, alikuwa kiongozi wa mfano aliezingatia maadili ya uongozi hasa katika suala la uadilifu, busara na uwajibika.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika kutekeleza wajibu wake Mzee Karume aliongoza kwa ushauri na ridhaa ya Baraza la Mapinduzi, jambo ambalo linaendelea kutekelezwa hadi hivi leo ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa Dikrii ambazo ziliendeleza utawala wa sheria, Demokrasia, Usawa, Umoja na Maridhiano.

Alisisitiza kuwa Marehemu Mzee Karume alionesha ushujaa katika kupinga dhuluma za aina zote walizofanyiwa wanyonge wa Unguja na Pemba na watawala wa Kisultani na Wakoloni kwa muda wa miaka mingi ambapo wananchi wa Zanzibar walinyimwa haki zao za maisha katika kuendelesha maisha yao.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Mzee Karume akiwa ni Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar pamoja na mambo mengineyo ilifanikiwa kutekeleza mambo kadhaa yaliyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya ASP.

Miongoni mwa hayo ni pamoja na kutangazwa kutaifishwa kwa skuli zote zilizokuwa zikiendeshwa kwa misingi ya ubaguzi na kutangaza elimu bure mnamo Septemba 23, 1964, kutangaza matibabu bure, kutangaza kutaifisha ardhi, kuondosha utaratibu wa kuwadhulumu wanyonge kwa kuweka vitu vyao rahani (poni).

Jengine ni kujenga nyumba za kisasa Unguja na Pemba mjini na vijijini, kuwajengea makaazi bora wazee na wengine ambao hawakuweza kukaa kwenye nyumba za wazee walipatiwa posho la kila mwezi, kuanzishwa Wizara za Serikali na kuwaeleza wananchi hali halisi ya fedha za Serikali ilivyo kila mwaka.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kumualika pamoja na maandalizi mazuri ya Kongamano hilo lenye mada isemayo “Mchango wa Maremu Mzee Abeid Karume katika Maendeleo ya Zanzibar”

Dk. Shein pia alitoa zawadi kwa washindi wa Insha bora zilizoeleza juu ya Kumbukumbu ya Marehemu Mzee Karume.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa  Rais Mohammed Aboud Mohammed  alitoa pongezi kwa Chuo hicho kuandaa Kongamanon hilo litakalokuwa endelevu huku akitumia fursa hiyo kueleza kuwa juhudi za Mzee Karume yeye na wenzake zimepelekea kuwepo kwa amani na utulivu mkubwa hapa nchini.

Waziri Aboud alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Rais Dk. Shein kwa jinsi wanavyokwenda sambamba na yale yote yaliyoanzishwa na waasisi wa Taifa hili.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa Mark Mwandosiya alieleza azma ya Chuo hicho kuandaa kongamano hilo huko akitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa jinsi alivyoiletea maendeleo makubwa Zanzibar kutokana na sifa zake mbali mbali za uongozi ikiwemo uvumilivu, usikivu, ustahamilivu, usimamizi, utawala bora na matumizi mazuri ya lugha aliyonayo Dk. Shein.

Nae Mkuu wa Chuo hicho Profesa Shadrack Mwakalila alieleza maendeleo makubwa yaliopatikana katika chuo hicho mara baada ya kuundwa Kampasi ya Chuo hicho hapa Zanzibar na kuanzisha masomo ya Cheti, Shahada na Stashahada.

Profesa Mwakalila alieleza kuwa Kongamano hilo litakuwa endelevu kwa lengo la kumuenzi Marehemu Mzee Karume na kueleza mashirikiano makubwa yaliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chuo hicho huku akitumia fursa hiyo kueleza changamoto za Kampasi ya Chuo hicho hapa Zanzibar.

Mada mbili Kuu zimewasilishwa katika Kongamano hilo ikiwa nipamoja na mada ya ‘Fikra za Abeid Karume katika Kujenga Umoja na Mshikamano wa Kijamii Zanzibar” iliyotolewa na Dk. Muhammed Seif Khatib na mada ya “Fikra za Abeid Amani Karume na Mapinduzi ya Uchumi Zanzibar”,aliyotolewa na Balozi Amina Salum Ali.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali walihudhuria katika Kongamano hilo.

  Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.