RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameyakaribisha Makampuni ya Privinvest na
Advanced Marine Transport (AMT) kutoka nchini Dubai yanayotengeneza meli za
aina mbali mbali kuja kuekeza hapa Zanzibar.
Dk. Shein ameyakaribisha
Makampuni hayo wakati alipofanya mazungumzo na Mwakilishi wa Makampuni hayo
Jean Boustany Ikulu mjini Zanzibar aliyefuatana na Balozi mdogo wa Tanzania
nchini Dubai Ali Jabir Mwadini ambapo Mwakilishi huyo alieleza dhamira ya
Makampuni hayo ya kuja kuekeza Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo,
Dk. Shein aliyakaribisha Makampuni hayo na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wake mkubwa na kuweka mazingira mazuri
katika kuhakikisha azma ya Makampuni hayo inatimia.
Dk. Shein alieleza kuwa azma
ya Makampuni hayo imekuja wakati muwafaka ambapo Zanzibar imo katika mikakati
ya kutekeleza uchumi wa bahari ambapo hatua hiyo imeonesha mwanzo mzuri kwa
Zanzibar kufikia hatua hiyo.
Aidha, Dk. Shein alimuueleza
Mwakilishi huyo kuwa lengo la Makampuni hayo kuja kuekeza Zanzibar itasaidia
kuendeleza historia ya Zanzibar ya kuwa eneo na kituo kikuu cha biashara katika
ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati ambapo shughuli hizo zilianza tokea
miaka ya 1899 hapa Zanzibar.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari
kushirikiana na Makampuni hayo na kueleza hatua itakayofuata kwa viongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukaa pamoja na uongozi wa Makampuni hayo kwa
lengo la kuangalia utekelezaji wa azma hiyo.
Dk. Shein alimueleza
Mwakilishi huyo kuwa kikao hicho kitasaidia kutoa mwelekeo kwa pande mbili hizo
kutokana na fursa zilizopo sambamba na kuangalia ni uwekezaji wa aina gani utaanzishwa
na Makampuni hayo ambayo yanauzoefu mkubwa katika utengenezaji wa meli za aina
mbali mbali.
Sambamba na hayo, Rais Dk.
Shein alimueleza Mwenyekiti huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuhakikisha inaanzisha Shirika lake la uvuvi hatua ambayo
itaimarika zaidi baada ya uwekezaji wa Makampuni hayo hapa nchini pamoja na
kuimarisha sekta ya uvuvi na kupanua soko la ajira kwa vijana.
Alieleza kuwa uwamuzi wa
Makampuni hayo ni mzuri na umekuja katika wakati muwafaka ambapo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, hivyo
hatua hiyo itakuwa chachu katika kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Pia, Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kumueleza Mwenyekiti huyo mikakati ya mashirikiano katika
sekta za maendeleo iliyofikiwa katika mazungumzo kati yake na viongozi wa nchi
za Falme za Kiarabu aliokutananao katika ziara yake ya hivi karibuni aliyoifanya
huko UAE.
Nae Mwenyekiti wa Makampuni
ya Privinvest na Advanced Maritime Transport (ATM) Kanda ya Afrika Jean
Boustany alimueleza Rais Dk. Shein jinsi Makampuni hayo yalivyovutiwa kuja kuekeza
hapa Zanzibar.
Mwenyekiti huyo,
alieleza kuwa Makampuni hayo yanaamini kuwa kukamilika kwa lengo lao hilo
kutaipaisha Zanzibar kiuchumi sambamba na kukuza sekta za maendeleo zikiwemo
uvuvi, viwanda, ajira na nyenginezo.
Juean Boustany alimuhakikishia
Rais Dk. Shein kuwa Makampuni hayo yako tayari kuja kuekeza Zanzibar na kuahidi
kutoa mashirikiano makubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliongeza kuwa Makampuni
hayo yamevutiwa na mazingira mazuri ya Zanzibar hatua ambayo itakuwa chachu
katika kufanikisha azma yao hiyo.
Pamoja na hayo,
Mwenyekiti huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Makampuni hayo ni miongoni mwa
Makampuni yanayoongoza katika utengenezaji wa vyombo vya usafiri wa baharini na
uendeshaji wa Bandari na usafirishaji wa mizigo,pia yanatoa huduma kwa majeshi
ya wanamaji,ukodishaji wa ndege na meli na utandazaji na uedeshaji wa
miundombinu ya mafuta na gesi
Aidha, alieleza kuwa
katika Bara la Afrika Makampuni hayo yanafanya shughuli zake Afrika Kusini,
Angola, Cameroon, Congo, Equatorial Guinea, Ghana, Nigeria, Madagascar na
Msumbiji ambapo shughuli kuu za Makampuni hayo ni kutengeneza meli za aina
mbali mbali zikiwemo meli za uvuvi, ulinzi, meli za abiria, bishara na yoti
(yatch).
Mwenyekiti huyo amemuhakikishia Dk. Shein kuwa Makampuni
hayo yako tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Zanzibar na kusisitiza
kuwa azma yao hiyo itazidi kujenga na kuuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment