Habari za Punde

MAADHIMISHO YA KIMONDO CHA MBOZI KUFANYIKA MWEZI JUNI MKOANI SONGWE

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akiangalia Kimondo cha Mbozi alipotembelea kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimondo duniani yatakayofanyika Juni 28 hadi 30 mwaka huu. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.

Na Hamza Temba-WMU-Songwe
..........................................................................
Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine wa uhifadhi na maendeleo utafanya maadhimisho ya siku ya Kimondo cha Mbozi kwa mara ya kwanza katika historia kwenye Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali, wilayani Mbozi kuanzia Juni 28 hadi 30 mwaka huu .

Maadhimisho hayo yataenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Vimondo duniani ambayo yaliazimiwa kufanyika Juni 30 kila mwaka na kikao cha Umoja wa Mataifa cha tarehe 6 Desemba, 2016.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho pia kiliazimia tarehe hiyo kuwa siku ya kuelimisha umma kuhusu elimu ya anga na mafanikio ya tafiti mbalimbali yaliyopatikana kuhusu elimu hiyo, kutambua juhudi zilizofanyika, kuweka sheria za kimataifa na kutoa tahadhari juu ya athari zinazoweza kutokea endapo dunia itafanya uharibifu juu ya anga.

Taarifa hiyo imetolewa jana katika Kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Herman Tesha wakati akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya maadhimisho hayo kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ambaye alitembelea kituo hicho kwa ajili ya kukagua shughuli za maandalizi.

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutangaza Kimondo kama kivutio muhimu cha utalii mkoani Songwe pamoja na vivutio vingine vya mkoa huo kwa ujumla ili kutoa fursa ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii mkoani humo. 

Amesema maadhimisho hayo yataenda sambamba na kongamano la uwekezaji na sayansi ya vimondo, maonesho ya malikale, maonesho ya kiutamaduni, mashindano ya riadha (Kimondo Marathon), mashindano ya netiboli na mpira wa miguu (Kimondo Ligi).

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema Serikali kupitia Wizara yake itashiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo kwa kushirikiana na mkoa wa Songwe na wadau wengine ili kuhakikisha kivutio hicho cha Kimondo kinajulikana zaidi ndani na nje ya nchi na hatimaye kiongeze idadi ya watalii na mapato.

Amesema wizara yake ina mkakati maalum wa kuimarisha kituo hicho cha utalii ambapo hivi sasa imeshajenga kituo maalum cha taarifa ambacho kimegharimu zaidi ya Shilingi milioni 400 za Kitanzania. 

Aidha, amesema kupitia mkakati mpya wa wizara wa kuimarisha na kuvijengea uwezo vituo vya malikale nchini kwa kuzishirikisha taasisi za uhifadhi wa wanyamapori na misitu, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanapa litashirikiana na kituo hicho kwa kuimarisha miundombinu pamoja na utangazaji. 

Nao wananchi wa kijiji cha Ndolezi wakizungumza kwa nyakati tofauti hawakusita kuonyesha furaha zao kuhusu maendeleo ya eneo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika mipango na miradi mbalimbali itakayoanzishwa katika eneo hilo kwa faida ya pande zote mbili.

Katika hatua nyingine, baada ya kuhitimishwa kwa ratiba za Mwenge wa Uhuru wilayani Mbozi, wakimbiza Mwenge Kitaifa walilazimika kutumia fursa ya uwepo wao wilayani humo kwenda kutalii kwenye kivutio cha Kimondo wakati wa usiku wakiongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga. 

Kimondo cha Mbozi kilianguka mwaka 1840 kutoka kwenye obiti yake huko angani huku kikikadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11. Kimomdo hicho ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na cha nane duniani kati ya vimondo 600 vilivyodondoka maeneo mbalimbali ulimwenguni, sifa yake kubwa ni kuwa na ubaridi wakati wote hata mchana wa jua kali.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akikagua mpaka wa eneo la kituo cha kimondo na vijiji jirani alipotembelea kituo hicho cha utalii  katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimondo duniani yatakayofanyika Juni 28 hadi 30 mwaka huu. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akikagua kituo cha taarifa cha Kimondo cha Mbozi alipotembelea kituo hicho cha utalii  katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimondo duniani yatakayofanyika Juni 28 hadi 30 mwaka huu. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na baadhi ya watalii wa ndani waliotembelea kituo cha utalii cha kimondo katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana. Nyuma yao ni jengo jipya la kituo cha taarifa ambalo ujenzi wake umekamilika.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watalii wa ndani waliotembelea kituo cha utalii cha kimondo katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana. Nyuma yao ni jengo jipya la kituo cha taarifa ambalo ujenzi wake umekamilika. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (nyuma kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakimbiza Mwenge kitaifa, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ernest Palingo (kushoto) na waratibu wa Mwenge mkoa wa Songwe mbele ya Kimondo cha Mbozi katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana usiku baada ya shughuli za Mwenge. Kimondo hicho ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.