Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Aendelea na Ziara Yake Wilaya ya Kusini Unguja Kuzungumza na Mabalozi wa Wilaya Hiyo.

MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na Mabalozi wa Wilaya ya Kusini Unguja katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Makunduchi na kutumia fursa hiyo kuwaeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha CCM inaendelea kushika Dola.

Aidha, Dk. Shein Dk. Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwataka Mabalozi hao kutowaunga mkono wale wote wanaofanya mambo kinyume na maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kujitangazia kugombea nafasi za uongozi kabla ya wakati uliowekwa ndani ya chama hicho.

Aidha, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar katika suala zima la ajira kwa vijana licha ya kuwepo kwa vijana wengi wanaomaliza elimu ya juu na kuhitaji ajira ambapo inakisiwa karibu vijana 42,000 wamemaliza kutoka vyuo vikuu vitatu vya Zanzibar wamemaliza masomo ndani ya miaka saba ya uongozi wake.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa agizo kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji, na Nishati kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo la maji katika kijiji cha Kajengwa Makunduchi.

Nao Mabalozi wa Wilaya ya Kusini Unguja walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa jinsi anavyotekeleza vyema Ilani ya  Uchaguzi ya CCM na kutumia fursa hiyo kumpongeza kwa hotuba yake ya Mei Mosi mwaka huu aliyoitoa huko Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Pia walimpongeza kwa nyongeza ya mishahara aliyoitoa mara nne ndani ya kipindi cha miaka saba ya uongozi wake na kueleza kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyoweza kufanya hivyo hatua ambayo inatokana na usimamizi mzuri wa mapato ya serikali anayoiongoza.

Mbali ya mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya hiyo, Mabalozi hao pia, walieleza changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi, uvamizi wa maeneo ya kilimo na misitu huku wakiiomba Idara ya Ardhi kutoa taaluma kwa wananchi katika suala zima la uhakiki wa ardhi unaoendelea hivi sasa.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.