Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Amaliza Ziara Yake Kisiwani Pemba leo.

 
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alkizungumza na Viongozi wa Serikali, Kisiasa na Vyombo vya Ulinzi wa Mikoa Miwili ya Pemba baada ya kumaliza ziara yake ya siku Tatu Kisiwani humo.
 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdulla Juma Saadala {Mabodi} akiwashukuru Watendaji wa Taasisi za Serikali Kisiwani Pemba kwa ushirikianowao na Viongozi wa CCM pamoja na kutekeleza Ilani ya Chama Tawala.
Baadhi ya Viongozi wa Kisiasa na Serikali wa Mikoa Miwili ya Pemba wakimshangiria Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  hayupo picha wakati wa kumaliza ziara yake ya Siku Tatu Kisiwani humo.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba udhibiti wa Misumeno ya Moto Nchini lazima uhusishwe pia na vyomvo vya Dola katika kuona utunzaji wa Mazingira unazingatiwa ipasavyo katika pembe zote za Visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema ukataji ovyo wa Miti kwa kutumia misumeno ya Moto hivi sasa unaonekana kama ni jambo la kawaida kwa baadhi ya Wananchi katika sehemu mbali mbali bila ya kujali kwamba iko siku tabia hiyo inaweza kuleta  Majanga ya Maisha.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Viongozi Waandamizi wa Taasisi za Serikali, Kisiasa na vyombo vya Ulinzi katika Mkutano wa kutathmini ziara yake ya Siku Tatu aliyoifanya Kisiwani Pemba Mkutano uliofanyika hapo katika Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.
Alisema zipo athari za Kimazingira  zinazoshuhudiwa  na Wananchi katika maeneo mengi Nchini akizitolea Mfano zile za kupanda kwa kina cha Maji ya Bahari katika Kijiji cha Sipwese Mkoa wa Kusini Pemba kutokana na kukatwa ovyo kwa Misitu ya Mikoko.
Balozi Seif alieleza kwamba  athari hiyo  inakwenda sambamba na ile ya uchimbwaji wa Mchanga usiozingatia utaratibu wa Kimazingira katika  Mkoa wa Kaskazini Unguja ambayo ilimsikitisha Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan wakati alipofanya ziara kuangalia hali ya Mazingira Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwaeleza Viongozi hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutekeleza ahadi na malengo yake iliyojipangia katika kuwahudumia Wananchi wake kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM kilichopata ridhaa ya Wananchi walio wengi kuongoza Dola.
Balozi Seif  ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema katika kuona Taifa linapiga hatua  za haraka za Maendeleo aliyatahadharisha yale makundi yaliyokuwepo wakati wa Kampeni kwenye mchakato wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu ni vyema yakaendelea kushirikiana pamoja katika kuwaletea Maendeleo Wananchi walio wengi Nchini badala ya kuendeleza majungu na malumbano yasiyoleta tija kwa pande zote husika.
Alisema makundi yaliyoshinda na yale yaliyoshindwa  yaelewe kwamba yana kjazi moja tuu hivi sasa ya kujenga mazingira ya kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza Dola wakati wa uchaguzi mwengine wa Mwaka 2020.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba tabia mbaya ndani ya Chama cha Mapinduzi ya kuchukiana sambamba na kuhasimiana itaendelea kujenga chuki na kutoa fursa kwa kambi ya upinzani kupata nguvu ya kujiimarisha na hatimae kuleta changamoto kwa Chama Tawala.
Alisema huu ni wakati mzuri kwa Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kuongeza nguvu ya uimarishaji katika kutafuta wanachama wapya hasa Kisiwani Pemba ili ifikapo Mwaka 2020 iwe kazi rahisi katika kuelekea mapema kwenye ushindi wa Chama chao.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa  CCM Zanzibar Dr. Abdullah Juma Sadala {Mabodi} alisema Chama cha Mapinduzi hakina vikwazo vyovyote endapo watendaji wa Serikali wanaendelea kutekeleza vyema wajibu wao katika kuwatumikia Wananchi.
Dr. Mabodi alisema kitendo cha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kufanya ziara ya mara kwa mara katika kukagua Miradi ya Maendeleo ya Wananchi pamoja na kujua changamoito zinazowakabili Wananchi hao ni utekelezaji sahihi wa Ilani ya CCM.
Alisema Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 179 imeweka wazi utaratibu mzima kwa Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kushirikiana na Viongozi Wakuu kuwajibika katika kutekeleza masuala hayo Kikatiba.
Dr. Abdulla Juma Mabodi aliwahimiza na kuwaagiza pia Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa ngazi zote ni lazima washuke kwa Wananchi wote kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kilichopewa dhamana ya kuongoza Dola.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar alishukuru na kupongeza Ushirikiano mkubwa na wa karibu uliopo baina  ya Viongozi wa ngazi zote za Chama na wale wa Serikali zote mbili nchini.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Viongozi wa Chama na  Serikali wa Mikoa Miwili ya Pemba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa Hamad Mberwa alisema ushindi wa CCM katika chaguzi zozote Nchini ni lazima ili Nchi iendelee kutawaliwa na Amani itakayotoa fursa kwa Wananchi kuendelea na harakati zao za Kimaisha za kila siku.
Mzee Mberwa alisema Viongozi wa Mikoa hiyo watahakikisha kwamba hilo linafanikiwa vyema katika mustaakabali wa kuiona Tanzania na Watu wake wanabakia kuishi kwa upendo na heshima.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.