Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) Zuhura Maganga akiomba kura kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Kampasi ya Tunguu, Mkoa Kusini Unguja.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa sita wa TAPSEA uliofanyika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar wakimpongeza Mwenyekiti Zuhura Magange baada ya kuchaguliwa kwa mara nyengine kuongoza Chama hicho kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Mwenyekiti wa TAPSEA Zuhura Magange (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti Marcella Komba (kulia) na Naibu Katibu Mkuu Rose Mwaima baada ya kuchaguliwa kuongoza Chama hicho kwa kipindi cha miaka mitatu katika mkutano uliofanyika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Tunguu Mkoa Kusini Unguja.
Mwenyekiti wa TAPSEA Zuhura Magange akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati waliyoiweka kukiongoza Chama hicho katika kuwasaidia na kuwaendelea Makatibu Mahsusi wa Tanzania baada ya kuchaguliwa tena kukiongoza Chama hicho katika Mkuu wa uchaguzi uliofanyika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Tunguu Mkoa Kusini Unguja.(Picha na Ramadhani Ali Maelezo Zanzibar.)
Na Kijakazi Abdalla - Maelezo Zanzibar - 14/05/2018
Mkutano Mkuu wa sita wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliomalizika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Tunguu, umemchagua tena Zuhra Magange kuwa Mwenyekiti wa chama hicho kwa kipindi chengine cha miaka mitatu.
Bi. Zuhura ambae ni Mfanyakazi wa Shirika la Bandari Dar es Salaam alimshinda Bi. Hadia mfanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es salaam kwa kupata kura 661 na mpinzani wake alipata kura 72.
Uchaguzi huo uliokabiliwa na changamoto ya mvua kubwa inayoendelea na kuharibu miundombinu ya barabara inayokwenda Tunguu ulipelekea baadhi ya wajumbe kushindwa kufika kwa wakati kwa ajili ya kupiga kura.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAPSEA walimpitisha kwa mara nyengine Marcella Komba kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kipindi chengine cha miaka mitatu baada ya kukosa mpinzani.
Wengine waliochaguliwa kuongoza chama hicho ni Aneth Mapima kuwa Katibu Mkuu, Rose Mwaima Naibu Katibu, Mshika fedha ni Mwajuma Luambano na wajumbe tisa wa Baraza Kuu la TAPSEA.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uchaguzi wa chama hicho, Zuhra Magange
aliwashukuru wajumbe kwa kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi
wanaowataka na kuwaomba walioshindwa katika uchaguzi huo kushirikiana na viongozi
waliopo katika kupigania maslahi na mazingira bora ya Makatibu Mahsusi Tanzania.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi atahakikisha kuwa kada ya makatibu mahsusi ni muhimu na yenye thamani kubwa Tanzania kinyume na inavyoonekana kama ni watu wa kawaida wenye taaluma ndogo.
Magange aliwasisitiza Makatibu mahsusi kuongeza bidii katika kutekeleza majuku yao ya kazi na kufuata maadili ya kazi zao ikiwapa moja na kutunza siri za ofisi ili kujenga imani na kuwa msaada kwa mabosi wao.
Aliwakumbusha Makatibu mahsusi kuwa TAPSEA imefanya juhudi ya kuanzishwa elimu ya juu ya kada hiyo katika chuo cha utumishi wa umma hivyo amewataka kujiunga na chuo hicho kujiendeleza kielimu.
alitoa ushauri wa kutekelezwa kauli mbiu ya mkutano mkuu wa sita wa TAPSEA mwaka huu usemao "Kuimarisha taaluma na uadilifu katika utendaji."
No comments:
Post a Comment