Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Akabidhi Zawadi Kwa Wafanyakazi Bora Zanzibar. Maadhimisho ya Mei Mosi Pemba.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwachukulia hatua kali wawekezaji au waajiri wote wanaokwenda kinyume na sheria za Serikali.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana mashirikiano ya Sekta binafsi na kusisitiza kuwa wawekezaji au waajiri wanaodharau sheria au maslahi ya wananchi hawatovumiliwa hata kidogo.   

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ukumbi mdogo wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo Zanzibar inaungana na nchi nyengine duniani katika maadhimisho hayo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa inasikitisha kwamba kuna baadhi ya wawekezaji na waajiri ambao wafanyakazi kuzikwamisha juhudi za Serikali ambapo walijaribu kuupinga uwamuzi uliotolewa na kutishia kuwafukuza wafanyakazi na kuweka visingizio mbali mbali ili waendelee kulipa mishahara wanayoitaka bila ya kuzingatia sheria za nchi.

Hata hivyo, Dk. Shein alisema kuwa amefurahi kuona kwamba hivi sasa wananchi wengi wanaofanya kazi katika sekta binafsi, wameanza kufaidika na kiwango cha mshahara kilichotangazwa na kutoa wito kwa taasisi ambazo bado hazijatekeleza agizo hilo zitetekeleze kwa haraka.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kupima afya kwa wafanyakazi wote na kuwashajiisha kufanya mazoezi kupitia vikundi mbali mbali vilivyoanishwa ili kuwakinga na maradhi huku akisisitiza kuwa UKIMWI bado upo hivyo tahadhari badozinahitajika.

Kutokana na wanawake wengi hivi sasa kukumbwa na vifo vinavyotokana na ongezeko la maradhi ya Saratani ya Shingo ya Kizazi, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kumuunga mkono Mama Shein kwa kuzindua kampeni hiyo kwa upande wa Zanzibar na Makamo wa Rais Mama Samia aliyezindua kwa upande wa Tanzania Bara mnamo tarehe 10 mwezi uliopita.

Kadhalika, Dk. Shein aliwahimiza wafanyakazi kuunga mkono juhudi za Serikali na jamii katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia jambo ambalo limekuwa ni  tatizo kubwa nchini hasa katika miaka ya hivi karibuni.

Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba vyama vya wafanyakazi lazima vitekeleze majukumu yao ya msingi kwa kuzingatia haki na wajibu wa pande mbili na kueleza kuwa hatochoka kuvihimiza vyama vya wafanyakazi, ili vizingatie kwamba haki na wajibu ni watoto pacha.

Hivyo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa vyama mbali mbali vya wafanyakazi kupitia Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi kwa juhudi wanazozichukua katika kuyatetea na kuyalinda maslahi ya wafanyakazi ambao ndio wanachama.

“Nakusisitizeni viongozi wa vyama vya Wafanyakazi muendelee kushirikiana na Serikali katika kuimarisha uwajibikaji, maadili pamoja na kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma”,alisema Dk. Shein.

Aidha, kuhusu tatizo la ajira kama ilivyo katika mataifa mbalimbali duniani, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa vikundi mbali mbali vya wajasiriamali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwaajiri vijana katika sekta mbali mbali kwa kadri nafasi zinavyopatikana huku akieleza kuvutiwa na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Njia Pekee ya Kukuza Uzalishaji na Kuimarisha Huduma, ni Kujadiliana na kujali Ushirikishwaji”, alisema Dk. Shein.
  
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.