MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza
kuwa CCM inaendelea kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 na
kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajenga barabara
ya kisasa katika eneo la Mwanakwerekwe na daraja la kisasa katika eneo la Kibondemzungu.
Dk. Shein ambaye pia, ni
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo huko katika
ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein ulioko katika Kampasi ya Chuo Kikuu Cha Taifa
Zanzbar (SUZA), Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja wakati alipokuwa
akizungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Kati.
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa tayari Serikali imeshatenga fedha kwa
ajili ya ujenzi huo katika maeneo hayo ambayo yamekuwa hayapitiki wakati wa
mvua kubwa na kuleta usumbufu kwa wananchi hasa wa Mkoa wa Kusini na wale wa
Wilaya ya Magharibi.
Dk. Shein alisema kuwa ujezi
huo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu na fedha zake tayari
zimeshatengwa katika Bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019 ili ujenzi uweze kuanza
kwa haraka na kupelekea barabara hizo ziweze kupitika wakati wote.
Aliongeza kuwa tayari
wataalamu wako katika mchakato wa kuangalia namna ya ujenzi utakavyotekelezwa
katika maeneo yote hayo mawili ambayo yamekuwa yakileta usumbufu mkubwa kwa
wananchi wkati wa kipindicha mvua hasa za masika “Serikali imeamua kujenga na
pesa zipo”alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Makamo Mwenyekiti
huyo wa CCM Zanzibar aliwataka Mabalozi wa Wilaya ya Kati kuyaeleza mafanikio
makubwa yaliofikiwa ambayo yametekelezwa na Serikali yao chini ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Dk. Shein aliendelea
kusisitiza kuwa kuanzia Bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019 hatakiwa mzazi kuchangia
ada ya mwanawe kwa skuli ya Sekondari na Msingi na Serikali imeamua kwa
makusudi kutekeleza azma ya Marehemu Mzee Abeid Karume ya elimu bure.
Rais Dk. Shein aliwaeleza
viongozi hao kuwa kwa upande wa sekta ya afya pia, juhudi za makusudi
zimechukuliwa katika kuhakikisha huma za afya nazo zinatolewa kwa misingi hiyo hiyo
huku akiwaleza kuwa maelezo kamili yatasomwa katika Bajeti za Wizara katika
Baraza la Wawakilishi linalotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Akiwaeleza wajibu wao kwa
mujibu wa Katiba ya CCM, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuendelea kusimamia
amani na kuongeza kasi katika suala hilo kwani CCM ndio inayosimamia amani,
utulivu na mshikamano.
Alisisitiza kuwa Sera ya
CCM ni amani, utulivu na msikamano hivyo CCM ni lazima ishinde ili kuendeleza
amani, utulivu na mshikamano huo sambamba na kuendelea kuyaenzi na kuyatunza
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na Muungano wake wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema kuwa ndani ya CCM
kuna kundi moja tu, na kuwataka Mabalozi kuendelea kuwafahamisha wana CCM na
kuwataka kutoruhusu wale wanaoingia ndani ya chama chao hicho kwa kutaka
uongozi na baadae kutowatendea majukumu yao wananchi waliowachagua.
Pia, aliwataka viongozi
wa CCM kufanya wajibu wao kwa kila aliyepewa nafasi ya kuongoza na kuwataka
kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa na kusisitiza kuwa Malazolizi ni vyema
wakafanya kazi walizokabidhiwa na chama ikiwa ni pamoja na kutafuta ushindi wa
CCM na si ushindi wa mtu mmoja mmoja.
Aliwataka kuwatafuta
viongozi watakaowasaidia na kuiendeleza CCM na si wale ambao mara tu baada ya
kupata uongozi wanawakimbia wananchi waliowachagua jambo ambalo alisema si
sahihi hasa kwa wale viongozi wa ngazi za Ubunge na Wawakilishi ambao Mabalozi
hao wanawajua.
Aidha, alisema kuwa CCM
ni chama kinachopendwa katika maeneo yote duniani na kimekuwa na Mashina yake
ndani na nje ya Tanzania
Alisisitiza kuwa ushindi
wa CCM mwaka 2020 hauepukiki na lazima CCM ishinde kwani ni maelekezo ya chama
hicho kuwa ushindi ni jambo la lazima, ushindi ambao utaletwa bila ya nguvu
wala ubabe.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar umeimarika kwa kiasi kikubwa na umekuwa
kutoka asilimia 6.8 kutoka mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2017
pamoja na kuongezeka kwa pato la mtu binafsi kutoka TZS 1,800,000 hadi TZS 2,000,000.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Dk. Abdalla Juma Mabodi alieleza haja kwa viongozi hao kuwa
karibu na wananchi pamoja na kuwepo kwa mikutano ya viongozi na wananchi
ifanyike mara kwa mara pamoja na kufanya ziara za mara kwa mara ili kupata
kujua matatizo yanayowakabili.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Kusini Unguja Ramadhan Abdalla Ali (Kichupa),alitoa pongezi kwa Rais Dk.
Shein kwa juhudi zake za kuendeleza na kuimarisha miradi mbali mbali ya
maendeleo katika Mkoa huo ikiwa ni pamoja na barabara mpya ya Cheju- UngujaUkuu
aliyoizindua katika shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi.
Nao Mabalozi wa Wilaya
ya Kati katika risala yao iliyosomwa na Balozi Mkombe Vuai Khamis, walitoa
shukurani za dhati kwa Rais Dk. Shein
kwa kuendelea kukutana nao awamu kwa awamu hatua ambayo inadhihirisha wazi
mashirikiano yaliopo kati ya viongozi wa Chama na Serikali.
Walieleza kuwa vikao
vyake hivyo anavyokutana na Mabalozi ambavyo Dk. Shein alivianza tokea mwaka
2014 vimeweza kufanikisha kwa kiasi kikubwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 pamoja
na ule wa marejeo wa tarehe 20 Machi 2016 ambapo CCM ilipata ushindi mkubwa na Wilaya
yao pia, kupata ushindi kwenye nafasi zote.
Walimpongeza Rais Dk.
Shein kwa utekelezaji wake wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na uongozi wake imara,
ujasiri usiyoyumba na kuweza kushuhudia maendeleo makubwa yaliopatikana katika
Nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii zikiwemo elimu, afya, umeme,
maji safi na salama, miundombinu ya barabara, pencheni ya wazee kuanzia miaka
70 na nyenginezo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment