Habari za Punde

Hutuba ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Kuhusu Majumuisho ya Mjadala wa Bajeti ya Serikali Kwa Mwaka 2018/2019


Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Mhe. Mohammed Said Mohammed Dimwa akisoma Majumlisho ya Mjadala wa Bajeti ya Serikali Kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019.


UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba nitangulize shukurani za awali kwa Mola wetu Allah (S.W) kwa kutuwezesha kuidiriki siku ya leo katika hali ya uzima na afya. Aidha, nimshukuru tena Mwenyezi mungu kwa kutujaalia neema ya pekee ya kuwa miongoni mwa waliokamilisha mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramadhan, tunamuomba atulipe malipo ya funga zetu, na pia atuwafikishe tuione Ramadhani ya mwakani tukiwa wazima wa afya Amiin.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kukushukuru wewe binafsi na wasaidizi wako Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, pamoja na Wenyeviti wa Baraza Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma na Mheshimiwa Shehe Hamad Mattar kwa namna mnavyotuongoza katika kutekeleza majukumu ya chombo hichi kwa maslahi ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba tokea tarehe 9/05/2018 Baraza la Wawakilishi limekuwa katika mjadala wa Bajeti ya mwaka 2018/2019 ambapo bajeti za Wizara zote 14 zimejadiliwa na kupitishwa, Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa napenda kuchukuwa fursa hii, kuwapongeza Wajumbe wote wa Baraza lako kwa kukamilisha kazi hiyo kwa umakini na ufanisi  mkubwa, kutokana na namna walivyozichambua na kuzijadili bajeti za Wizara na kutoa maoni yao ambayo bila shaka yalilenga kuzifanya bajeti hizo ziwe bora zaidi na zenye kuleta tija inayostahiki kwa maslahi ya wanachi na taifa kwa ujumla, ili dhamira na malengo ya nchi yetu yaweze kufikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 100(2) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi inaelekeza kwamba, Serikali kwa kushirikiana na Kamati ya Bajeti itafanya majumuisho kuhusiana na hoja mbali mbali zitakazojitokeza wakati wa mjadala wa Makadirio ya bajeti za Wizara zote. Mhesh    imiwa Spika, naomba kuliarifu Baraza lako kwamba Kamati ya Bajeti imetimiza masharti ya Kanuni hiyo, kwa kufanya  kikao cha majumuisho kwa muda wa siku mbili tarehe 18/06/2018 na 19 /06/2018, na kufanikiwa kupitia hoja mbali mbali za kibajeti zilizoibuliwa na Wajumbe wakati wakichangia bajeti za Wizara pamoja na maoni ya Kamati za kisekta yaliyowasilishwa Barazani kupitia hutuba za Kamati zao. 

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Bajeti kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kutekeleza majukumu ya Kamati. Aidha, napenda kuwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuchukua hoja mbali mbali za Wajumbe zilizotokana na mijadala ya bajeti, ambazo ndio msingi wa Hotuba hii. Mheshimiwa Spika, ili kuzipa nguvu shukurani zangu naomba kuwatambua kwa kuwataja kwa majina kama ifuatavyo;-

1.      Mhe. Mohamed Said Mohamed                     Mwenyekiti
2.      Mhe. Bahati Khamis Kombo                          Makamo Mwenyekiti
3.      Mhe. Simai Mohammed Said                         Mjumbe
4.      Mhe. Zulfa Mmaka Omar                               Mjumbe
5.      Mhe. Shehe  Hamad Mattar                            Mjumbe
6.      Mhe. Abdalla  Ali Kombo                              Mjumbe
7.      Mhe. Asha Abdalla Mussa                              Mjumbe

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuwatambuwa na kuwashukuru Makatibu wa Kamati ya Bajeti ambao wamekuwa na msaada mkubwa kwa Kamati yangu, ambao ni  
1.      Ndg. Abdalla Ali Shauri
2.      Ndg. Asha Said Mohamed
3.      Ndg. Kassim Tafana Kassim

Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya majumuisho ya Mjadala wa Bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa kushirikiana na Serikali, kwa kushauriana kuhusu hoja mbali mbali za kibajeti zilizojitokeza wakati wa mijadala ili kuangalia maeneo ambayo yanaweza kufanyiwa marekebisho au kuwekewa mazingatio maalum katika utekelezaji wake, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa Bajeti. Hivyo nitaiwasilisha  taarifa hii ambayo  ni matokeo ya mashauriano hayo baina ya Kamati ya bajeti na Serikali kwa Baraza lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, Katika kukamilisha kazi ya majumuisho ya mijadala ya Bajeti, Kamati ilikaa na Mawaziri wa Wizara zote zilizohusika na hoja ambao pia waliambatana na watendaji wakuu wa taasisi zao, ili kuweza kusaidia ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa. Aidha, kwa kuzingatia nafasi ya Wizara ya Fedha katika mchakato mzima wa Bajeti, kikao hicho pia kilimjumuisha Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndg. Khamis Mussa Omar pamoja na baadhi ya Watendaji wakuu wa Wizara hiyo. Kamati inapenda kuwashukuru Mawaziri pamoja na watendaji wao wote kwa ushirikiano mkubwa walioipatia Kamati katika kukamilisha zoezi hilo.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia umuhimu wa Kamati za Kisekta katika kazi ya majumuisho ya mijadala ya bajeti, Kamati pia iliwaalika Wenyeviti wa Kamati za Kudumu kwa lengo la kushauriana nao juu ya hoja na changamoto za kibajeti hususan katika sekta wanazozisimamia. Kamati ya Bajeti inawashukuru sana Wenyeviti wa Kamati kwa ushrikiano wao walioipatia Kamati kwa kutoa maoni ambayo yamesaidia sana katika kufanikisha majukumu ya Kamati kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimwa Spika,
Hoja zilizojitokeza wakati wa mjadala ni nyingi na kimsingi Kamati inazitambua zote kuwa ni muhimu. Hata hivyo, naomba ieleweke kwamba Hotuba hii imejumuisha baadhi tu ya hoja hizo kwa kuzingatia uhusianao wake na vifungu vya bajeti, ufafanuzi wa hoja hizo uliotolewa na Serikali wakati wa mjadala pamoja na matokeo ya mashauriano baina ya Kamati na Serikali kuhusu hoja hizo wakati wa kikao cha majumuisho.

MAENEO YALIYOCHANGIWA NA WAJUMBE WENGI
Mheshimiwa Spika, maneo ambayo yalichangiwa na Wajumbe wengi ni kama ifuatavyo;
  1. Uimarishaji wa Maslahi ya Walimu pamoja na ajira za walimu wakujitolea
  2. Changamoto  katika Utekelezaji wa Mfumo wa Ugatuzi
  3. Changamoto za Miundombinu ya Barabara
  4. Tatizo la kuongezeka kwa vitendo vya Udhalilishaji wa kijinsia
  5. Kusuasua kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi mikubwa ya Maendeleo
  6. Umuhimu wa kutumia mifumo ya kisasa katika kukusanya mapato
  7. Nidhamu katika Matumizi ya Fedha za Serikali
  8. Changamoto za kuchelewa kwa ripoti za mwaka za ukaguzi za Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
  9. Changamoto katika Utaratibu uliopo wa kukabiliana na maafa
  10. Changamoto za Huduma katika sekta ya afya
  11. Changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji
  12. Changamoto za Uendeshaji wa Meli ya M.V Mapinduzi II
  13. Changamoto za Biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara


UFAFANUZI WA HOJA ZILIZOTOKANA NA MAJADILIONO YA MAJUMUISHO BAINA YA SERIKALI NA KAMATI YA BAJETI
Mheshimiwa Spika, Baada ya maelezo hayo ya Jumla sasa naomba niingie kwenye hoja 31 kutoka katika mafungu na Wizara tofauti ambazo zilijadiliwa  na hatimae kutolewa ushauri na Kamati kwa lengo la kuhakikisha tunapata bajeti iliyo bora zaidi.
Mheshimiwa Spika, Naomba niwasilishe ufafanuzi wa Hoja hizo kwa njia ya Bango Kitita ambalo limegawika Sehemu Tatu; sehemu ya kwanza inahusu Hoja za Kisekta, Sehemu ya Pili inahusu, majibu ya Serikali na sehemu ya Tatu ni Maoni ya Kamati ya Bajeti. Mheshiwa Spika, baada ya maelezo hayo sasa naomba niwasilishe Hoja hizo kwa mpangilio wa Wizara kama ifuatavyo:  

HOJA ZILIZOTOKANA NA MJADALA WA BAJETI KWA MWAKA 2018/2019
  1. OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS
HOJA
MAJIBU YA WIZARA
MAONI YA KAMATI
1. TUME YA UCHAGUZI: Wajumbe walipendekeza Bajeti ya Tume ya Uchaguzi iongezwe kutokana na unyeti wa majukumu yake, ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilipangiwa Tsh bilioni1,695,500,000 na mwaka wa fedha 2018/2019 imepangiwa Tsh. bilioni 1,774,100,000. Aidha,  Majengo ya Tume ya Uchaguzi yako katika hali mbaya ikiwemo jengo  la ghorofa la Wilaya ya Kaskazini “A” ambalo miundombinu yake haiwawezeshi watu wenye ulemavu kulitumia  kwa wepesi. Kwa Afisi za Wilaya ya Kaskazini “B” kuna changamoto ya ufinyu wa ofisi kiasi cha kushindwa kuhudumia watu watatu kwa wakati mmoja.
Wizara imeiarifu Kamati kuwa bajeti iliyopangwa ya Tsh. bilioni 1,774,100,000 inatosheleza katika kutekeleza majukumu ya kuhudumia Ofisi na pia wamekiri kuwa wamepata ongezeko la asilimia 5 ya  fedha za bajeti ya 2018/2019, kulinganisha na Bajeti ya 2017/2017 na hivyo hakuna changamoto ya fedha. Aidha, kuhusiana na majengo ya Tume kuwa hali mbaya, Wizara imeeleza kamati kuwa imeshaomba maeneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya za Tume katika Wilaya ya Kaskazini A, Wilaya ya Kaskazini B, Wilaya ya Magharib A na Wilaya ya Magharibi B.
Kamati ilikubaliana na kiwango ambacho Wizara wameridhia kupatiwa kwa kuwa wamekiri fedha inayotolewa inatosheleza katika kutekeleza majukumu yao.
2. MFUKO WA MAENDELEO YA JIMBO CDF: Wajumbe wengi walichagia kuhusiana na Fedha chache zinazotolewa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF)  ambapo kwa sasa zinatolewa jumla ya Tsh milioni 20 na imependekezwa ziongezwe Tsh milioni tano (5).
Serikali imekiri kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF) katika majimbo ni chache na imeahidi kulifanyia kazi suala hili kuhakikisha kuwa zinaongezeka kwa mujibu wa uchumi utakavyoimarika katika bajeti zijazo.
Wajumbe wamesisitiza juu ya kuongezwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF) kwa kuwa majimboni kuna shughuli nyingi ambazo zinatakiwa kutekelezwa na pia kufanyiwa uchambuzi wa kina kuhusiana na fedha hizo zilivyotumika majimboni.
  1. OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI
1. IDARA YA URATIBU NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA URATIBU WA WAZANZIBARI WANAOISHI NJE YA NCHI
Kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wataalamu wa sekta mbali mbali kushindwa kushiriki katika mikutano ya mashirikiano ya kikanda tokea hatua za awali kutokana na ufinyu wa fedha, licha ya  baadhi Mawaziri kushiriki katika mikutano hiyo na kupelekea kushindwa kuiwakilisha Zanzibar ipasavyo. Kwa msingi huo, Wajumbe wamependekeza Idara hii kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 itengewe fedha za kutosha na pia zipatikane kwa wakati ili utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohusu Zanzibar ipate uwakilishi wa wataalamu tokea  hatua za awali. Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Idara hii imepangiwa bajeti ya Tsh 537,965,000
Kamati iliarifiwa kuwa, Bajeti iliyotengewa kwa Idara hii inatosheleza kwa mujibu wa watendaji wanaotarajiwa kusafiri kwa kuzingatia kuwa Idara hii kazi yake ni kuratibu tu. Aidha, fedha iliyotengwa ni kwa ajili ya safari za watendaji kama ilivyo kwa Wizara nyengine ambazo nazo kila moja ina bajeti yake kwa shughuli za kuhudhuria mikutano ya kikanda.
Kamati imeridhika na ufafanuzi wa Wizara, na kwakuwa Wizara imekiri kuwa Bajeti hiyo inatolesheleza, Kamati imeridhia fungu hilo kubakia kama lilivyo.
3. OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA NA IDARA MAALUM ZA SMZ
1. Kuhusiana na mradi wa CCTV Camera ambao kwa mwaka wa fedha 2018/2019 umetengewa Tsh bil. 20. Wajumbe walishauri kati ya fedha hizo zipunguzwe bil. 5 na zielekezwe kwenye kuimarisha barabara za ndani, mbazo bado zinauhitaji mkubwa wa fedha ukilinganisha na uwezo halisi wa kifedha uliopo hivi sasa. Aidha,  kwa kipindi cha miaka mitatu Wizara imepokea shilingi bilioni 4,600,000,000/- tu kwa ajili ya uendelezaji wa barabara za ndani (Feeder road).
Kamati imearifiwa kuwa, Mradi huu ni wa miaka mitano na Serikali inalazimika kulipa kwa mujibu wa mkataba wa mradi huo. Kwa hivyo inashauriwa fedha hizo zisipunguzwe.
Fedha kwa ajili ya barabara za ndani zinatokana na Mfuko wa Barabara. Ambapo katika mgao wa mfuko huo asilimia 15 zinapelekwa Halmashauri kwa ajili ya kuendeleza bararabara za nadani. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mtaa na Idara Maalum za SMZ, pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji zitakaa pamoja kuangalia namna ya kuongeza asilimia ya mgao wa mapato ya Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kuimarisha barabara za ndani.
Kamati imeridhika na Maelezo ya Wizara na imekubali fedha za Mradi wa CCTV zibakie kama zilivyo. Aidha, Kamati imeunga mkono wazo la kuongeza mgao wa fedha za mfuko wa Barabara kwa ajili ya kuimarisha barabara za ndani. Hivyo, Kamati ya Bajeti inaitaka Kamati husika ya Sekta kulifuatilia suala hilo.
2.Wajumbe wengi hawakuridhishwa na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato katika masoko ikiwemo mapato ya maegesho (parking), kulinganisha na huduma zinazopatikana pamoja na mazingira ya  masoko hayo.
Kamati imearifiwa kuwa mfumo wa ukusanyaji wa Mapato unatarajiwa kuwa kwa njia ya kielektroniki baada ya kipindi cha miezi miwili hadi mitatu. Aidha, Wizara imekiri kwamba miundombinu katika masoko hairidhishi. Hivyo, Wizara imeahidi kuwa itafanya maboresho baada ya kumalizika kwa kipindi cha mvua.
Kamati imependekeza wananchi wapatiwe elimu   kuhusu maeneo yanayoruhusiwa na ambayo hayaruhusiwi kwa ajili ya maegesho “parking”.   Kamati pia imeshauri kuanzishwa maeneo ya maegesho ya ghorofa ambayo yanakwenda sambamba na ukuaji wa mji. Pia Kamati imependekeza utakapoanza mfumo wa elektroniki kuwepo na utaratibu wa ukaguzi wa malipo ya maegesho ili kudhibiti uvujaji wa mapato.
  1. OFISI YA RAIS KATIBA , SHERIA, UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA
1. Katika bajeti ya mwaka 2018/19 Mahakama imepangiwa matumizi ya uendeshaji wa ofisi shilingi bilioni 1,515,100,000/=  na Tsh bilioni 1,113,800,000 za ruzuku. Wajumbe walishauri kuongezwa kwa fedha hizo kwa kuwa mara nyingi Mahkama imekuwa ikishindwa kuwawezesha mashahidi kuhudhuria mahkamani na kusababisha kusuasua kwa kesi.
Wizara imekiri kuwa bajeti iliyotengwa kwa mahkama kuu haitoshelezi katika kutekeleza majukumu yake. Fedha za matumizi mengineyo (Other charges) za kila mwezi hazitoshelezi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa mahkama. Hata hivyo, bajeti hiyo ni kwa mujibu wa ukomo “ceiling” waliyowekewa. Hivyo, Mahkama inafanya kazi kwa mujibu wa vipaumbele vyake kulingana na fedha walizoidhinishiwa.
                                                                   
Kutokana na changamoto zilizopo katika Mahkama, Kamati inapendekeza Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kukaa pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango na kuangalia namna ya kutatua changamoto zilizopo katika Mahkama ili kuleta utendaji ulio na ufanisi.
2. Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum imeshauri Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA) kupitia bajeti ya mwaka 2018/2019, ipatiwe vyombo vya usafiri hususani Afisi za Pemba ambazo zinatumia gari moja tu kwa Mkoa wa Kusini na Mkoa wa Kaskazini, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limekua likiathiri utendaji wao na kukosa ufanisi katika maeneo yao ya kazi.
Wizara imekiri ni kweli wana tatizo la usafiri ambalo linapunguza ufanisi wa shughuli za ZAECA Pemba. ZAECA wameshindwa kuweka mpango wa ununuzi wa gari kutokana na ukomo wa bajeti “ceiling” walio wekewa. Kwakuwa taratatibu zinaruhusu, Wizara ya Fedha imewashauri ZAECA, ikiwa suala la gari ndio kipaumbele chao waombe kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa ajili ya kununua gari kwa kuhaulisha fedha ndani ya vifungu vya bajeti yao.
Kamati inapendekeza ZAECA wauchukue ushauri wa kuhaulisha vifungu vya bajeti ili waweze kununua gari. Pia Kamati imependekeza Wizara ya Fedha iangalie uwezekanao wa kuwapatia ZAECA gari miongoni mwa gari zilizo rejeshwa na Taasisi nyengine.
3. Kamati ya PAC haikuridhishwa na kuchelewa kwa ripoti za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambazo zipo nyuma sana, wakati tupo katika bajeti ya mwaka 2018/2019 ndio kwanza Ofisi hii imekamilisha ukaguzi wa mwaka wa fedha 2015/2016. Aidha, Kamati ilionesha kutoridhishwa na kutoletwa Barazani Ripoti za Ukaguzi wa Miradi na Programu za Maendeleo ambazo zingeliwasaidia Wajumbe wa Baraza kupima ufanisi wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Kamati imearifiwa kuwa, kwa mujibu wa taratibu za ukaguzi ripoti hizo hazijachelewa kama inavyoelezwa kwakuwa ni lazima kwanza yafanyike matumizi kabla ya kufanywa ukaguzi na baada ya miezi mitatu ya matumizi ndio ukaguzi unapaswa kufanyika. Aidha, Serikali imekiri ni kweli kuna mashirika hayajawasilisha ripoti zao Barazani na kuahidi italifanyia kazi suala hilo ili Mashirika hayo yawasilishe ripoti zao kwa mujubu wa Sheria.
Kamati imeitaka Serikali ilifanyie kazi suala la ucheleweshwaji wa ripoti za CAG kwa kuyaainisha mashirika yote yanayopaswa kuleta  ripoti zake Baraza la Wawakilishi na kuhakikisha ripoti hizo zinawasilishwa kama ulivyo utaratibu.
Aidha, imependekezwa pia kuwe na uwazi zaidi katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali “CAG”  ili jamii ifahamu kinachoendelea.
  1. WIZARA YA HABARI UTALII NA MAMBO YA KALE
1. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya TSh. 4,344,000,000/= ambazo zitaingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Pia ilipangiwa kukusanya Sh. 3,113,600,000/= ambazo zitatumika na taasisi husika. Katika utekelezaji halisi, Wizara ilikusanya Sh. 2,924,572,780/= sawa na asilimia 61 zilizoingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Lakini kwa upande wa makusanyo yanayobakia katika Taasisi, Wizara ilifanikiwa kukusanya Sh. 3,515,703,680/= sawa na asilimia 113 ya malengo kama ilivyoelezwa katika utekelezaji. Wajumbe walihoji juu ya makusanyo yanayobakizwa kwa taasisi kuvuka malengo na kuzorota  kwa makusanyo yanayopelekwa katika mfuko mkuu wa Serikali.
Wizara imekiri ni kweli haikuvuka malengo ya makusanyo yanayoingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali,  kutokana na kuwekewa malengo makubwa ya makusanyo kwa bajeti ya mwaka 2017/2018 kulingana na uwezo wao wa kukusanya. Aidha, Kutokana na historia yao ya nyuma ya ukusanyaji mapato, shabaha waliyowekewa mwaka huu pia ni kubwa sana. Hivyo, kiuhalisia kiwango hicho walichokusanya sio kidogo kulinganisha na uwezo wa Wizara.
Kamati imeridhika na majibu ya Wizara. Aidha, Kamati inapendekeza Wajumbe wapatiwe  mafunzo kuhusu masuala ya bajeti ili dhana ya kubakiza mapato (retention) kwa tasisi zinazokusanya mapato ieleweke.
2. Kamati ya Maendeleo, Wanawake, Habari na Utalii, haikuridhiswa na uendeshaji wa ZBC 2 kupitia mkataba uliofungwa baina ya Shirika la Utangazaji la ZBC na Kampuni ya Azam Media LTD kwa ajili ya uendeshaji wa channel hiyo, kutokana na kutoonekana mapato yanayotokana na matangazo ya ZBC 2 kupitia mkataba huo.

Wizara imekiri ni kweli hakukuwa na mapato yaliyopatikana kupitia Mkataba huo, ingawaje Mkataba huo ulikuwa umejikita zaidi katika suala la mashirikiano, kwa kuandaa na kurusha vipindi vya pamoja na kugawana mapato. Aidha, Wizara imeiarifu Kamati kuwa mkataba wa awali umemalizika tokea tarehe 15/03/2018, na kwa sasa wapo kwenye utaratibu wa kujadiliana  kuhusu mkataba mpya. Wizara imeomba ipewe muda ili kuhakikisha kasoro zilizojitokeza awali hazijirejei tena katika mkataba mpya wanaojiandaa kuingia.
Kamati imeishauri ZBC na Serikali kwa ujumla kuwa makini katika kusimamia mikataba ili kuhakikisha ufanisi wa mikataba hususan katika masuala ya mapato.Aidha, Kamati imeagiza kupatiwa kivuli cha Mkataba huo wa makubaliano baina ya ZBC na Azam Media LTD ili ijiridhishe.
3. Wajumbe wengi walichangia kuhusu umuhimu wa kuitangaza zaidi Zanzibar Kiutalii hasa ikizingatiwa kwamba ni moja kati ya maeneo ya vipaumbele vya nchi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Programu ya Utangazaji na Uhamasishaji wa Utalii imetengewa Tsh milioni 533,145,000 tu. Aidha, Wajumbe walichangia kuhusu kuimarisha maeneo ya kihistoria na vivutio vya ndani ambavyo iwapo vitaimarishwa mapato ya sekta hii yataongezeka mara dufu.

Wizara imekiri, ni kweli bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kuutangaza Utalii ni ndogo, hata hivyo, kutokana na ukomo wa bajeti “ceiling” na uwezo wa Serikali kiwango hicho kinatosha kutekeleza majukumu waliyojiwekea. Aidha, Wizara imesisitiza kulingana na fedha wanayopatiwa utendaji wao ni mkubwa hasa ikizingatiwa kiwango cha watalii wanaoingia nchini kinaridhisha kulinganisha na bajeti wanayotengewa kwa ajili ya kuutangaza Utalii.
Kamati imeridhika na majibu ya Wizara na kuipongeza kutokana na kazi kubwa wanayoifanya. Hata hivyo Kamati, imeisisitiza Wizara kuitangaza zaidi Zanzibar kupitia balozi zilizopo nje ya nchi pamoja na kuweka taarifa muhimu zinazohusiana na Zanzibar ambazo zinakosekana katika balozi . Kamati pia imeshauri Wizara ifanye utafiti katika visiwa vilivyopo Zanzibar ili zijulikane rasilimali zilizopo ambazo zinaweza kusaidia na kuwa na mchango mkubwa katika kuwavutia watalii.
6.      WIZARA YA KAZI, UWEZESHAJI, WAZEE, WANAWAKE NA WATOTO
1. Wajumbe wengi walijenga hofu na kuomba ufafanuzi kuhusu fedha za Programu ya Kukuza Maendeleo ya Wanawake na Kupinga Udhalilishaji ambayo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 imetengewa Tsh bilion 1.7 kwakuwa inaonekana fedha hizo zimeongezeka maradufu ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2017/18, licha ya ukweli kwamba vitendo vya udhalilishaji bado vinaendelea kuongezeka.
Kamati imearifiwa kuwa sababu ya  Bajeti ya Fungu la Programu ya Kukuza Maendeleo ya Wanawake na Kupinga Udhalilishaji kuwa  kubwa ni kutokana na mikakati iliyowekwa ya kupambana na vitendo vya  udhalilishaji, ikiwa ni pamoja na  kulipia malipo ya waratibu  wa vitendo vya udhalilishaji. Aidha, fungu hili linaonekana kubwa kutokana na kuunganishwa Programu ndogo mbili, yaani Programu ya Uratibu wa Masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uendelezaji wa Wanawake na Programu ya Mapambano dhidi ya Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto. Kuhusu hoja ya kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji, Wizara imeeleza kuwa vitendo vya udhalilishaji havijaongezeka isipokuwa kwa sasa wananchi wamehamasika kuripoti matukio ya vitendo hivyo katika Mamlaka husika.
Kamati imependekeza kwa bajeti ya mwaka 2019/2020 Wizara itoe ufafanuzi zaidi kwa programu ambazo zimefanyiwa mabadiliko makubwa ya fedha kupitia kitabu cha Hotuba cha Mheshimiwa Waziri ili Wajumbe wajuwe matumizi halisi ya fedha hizo badala ya kuzichanganya.
2. Wajumbe walihoji kuhusu kutofautiana kwa malengo ya utoaji wa Mikopo kwa mwaka 2018/2019 baina ya Kitabu cha Hutuba ya Mhe. Waziri na Kitabu kikubwa cha Bajeti ambacho Wajumbe wanaidhinisha. Katika Kitabu cha Hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeelezwa kuwa Wizara inatarajia kutoa Mikopo 600 lakini kwenye Kitabu kikubwa Wizara inaonekana kupanga kutoa Mikopo 500. Aidha kwenye utekelezaji wa mwaka 2017/2018 pia kunatofauti ya Idadi ya Mikopo iliyotolewa baina ya Kitabu cha Hutuba na Kitabu kikubwa. Kwenye Kitabu cha Hutuba imeripotiwa kuwa Wizara ilitoa jumla ya Mikopo 279 lakini kwenye Kitabu kikubwa imeripotiwa kuwa Wizara ilito mikopo 300.
Wizara imeeleza kuwa tofauti ya Malengo ya  Idadi ya Mikopo itakayotolewa kwa mwaka 2018/2019 ilitokana na makosa ya kiuchapaji.  Aidha, kuhusu tofauti ya Idadi ya Mikopo iliyotolewa kwa mwaka 2017/2018 inatokana na kutofikiwa Utekelazaji wa malengo ya mikopo hiyo.

Kamati imeridhia ufafanuzi uliotolewa na Wizara juu ya utafauti wa taarifa baina ya vitabu viwili vya bajeti. Aidha, Kamati inasisitiza kuwepo kwa umakini zaidi wakati wa  kuandaa vitabu ili makosa kama hayo yasijirejee tena.
  1. WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI
1. Kutokana na changamoto nyingi katika sekta ya elimu ikiwemo ukosefu wa vifaa, ubovu wa madarasa, uhaba wa walimu, uchache wa vitabu vya kusomea na vikalio, Kamati ya Ustawi Jamii imependekeza fedha za bajeti ya Programu ya Elimu ya Sekondari TZS bilioni 95.6 zilizotengwa kwa mwaka 2018/2019, zipatikane kwa wakati ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Programu hii ilitengewa Tsh 63.5 bilioni, Hadi kufikia machi 2018  jumla ya tsh 27.4 bilioni tu ndizo zilizopatikana sawa na asilimia 43.
Fedha zilizochelewa kupatikana ni fedha za wahisani  tu, kwa upande wa fedha za SMZ za Maendeleo pamoja na fedha za matumizi ya kawaida zote zimepatikana kwa wakati na kwa kiwango kizuri . Aidha, changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika sekta ya elimu zinaendelea kufanyiwa kazi.
Kamati imekubaliana na hoja bila ya marekebisho yoyote.
2. Kamati ya Ustawi wa Jamii imearifu kuwepo kwa madeni ya walimu yanayotokana na malimbikizo ya stahiki za mishahara kama vile posho za likizo, masawazisho ya stahiki baada ya kumaliza masomo ya juu (mishahara) na posho za nauli. Kutokan na changamoto hiyo ambayo ni ya muda mrefu. Kamati imetowa wito kwa Wizara kuchukua hatua za kusawazisha malimbikizo hayo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa walimu.
Wizara imearifu kwamba madeni yote ya malimbikizo ya walimu pamoja na wastaafu yameshalipwa hadi kufikia mwaka 2016.
Kamati inashauri Wizara kuendelea kulifuatilia zaidi suala la malipo ya madeni ya walimu ili kuwaondoshea usumbufu. Kamati inasisitiza suala hilo kwakuwa bado kuna malamiko kwa baadhi ya walimu kuhusu madeni hayo. Aidha, iweke utaratibu mzuri ambao hautowapa usumbufu waalimu katika kufuatilia stahiki hizo.
3. Wajumbe wengi wameonesha kutoridhishwa na maendeleo ya Ujenzi wa vituo vya elimu Amali vya Daya-Mtambwe na Makunduchi. Kwakuwa kuna ongezeko la fedha kwenye Programu ya Elimu Mbadala na Mafuzno ya Amali, ambapo  kwa mwaka 2017/2018 Programu hii ilitengewa Tsh bilioni 17.1 na kwa mwaka  2018/2019 imetengewa Tsh bilioni 24.5. Wajumbe wameitaka Wizara kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa ndani ya mwaka huu wa fedha, kwa kuhakikisha majengo hayo yanendelezwa na kufikia hatua inayoridhisha.
Wizara imekiri kuwepo kwa matatizo yanayohusiana na mkandarasi katika mkataba wa mwanzo ambao umekwisha muda wake na kwasasa wamesaini mkataba mpya kwa ajili ya utekelezaji kazi. Aidha, Wizara imeahidi kufanya jitihada ili changamoto zilizojitokeza kwa mkandarasi wa awali zisijitokeze tena.
Kamati imeishauri Wizara kuendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa vituo vya  Elimu ya Amali na pia kuanzisha kitengo cha majenzi katika Wizara ili kitakacho saidia kutatua baadhi ya changamoto za miradi ya ujenzi.
4.Kamati haikuridhishwa na fedha zilizotengwa katika Programu ya Ubora wa Elimu, ambapo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 imetengewa Tsh bilioni 7.7 tu, licha kuwa  Programu hii inahusisha taasisi nyingi kama vile Taasisi ya Elimu Zanzibar, Baraza la Mitihani, Mrajis wa Elimu, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu, Shirika la Huduma za Maktaba, elimu mjumuisho, Vituo vya Mafunzo ya Walimu, TEHAMA na michezo.
Wizara imeiarifu Kamati kuwa bajeti iliyotengwa ambayo ilionekana kuwa ni ndogo ni fedha za ruzuku kutoka Serikalini lakini pia kuna fedha nyengine za miradi zinazochangiwa na washirika wa maendeleo.
Kamati imeridhishwa na majibu ya Wizara na kupitisha hoja hii bila ya mabadiliko yoyote.
8.WIZARA YA BIASHARA NA VIWANDA
1. Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo haikuridhishwa na bajeti ndogo iliyotengwa kwenye Programu ndogo ya Ukuzaji Viwanda (SR010201), ambayo kwa mwaka wa fedha  2018/2019 imetengewa jumla ya shilingi 3,665,290,000. Kiwango hicho kinaonekana ni kikubwa ikilinganishwa na fedha zilizotengwa mwaka 2017/2018 ambazo ni shilingi 644,987,000. Lakini kiuhalisia  fedha hizo hazitoshelezi hata kuanzisha kiwanda kimoja na kwa msingi huo imependekezwa programu ndogo hiyo iongezewe fedha zaidi kwa nia ya kuanzisha viwanda na kuvifanya na  kuwa endelevu.
Wizara imekiri kuwa fedha zilizotengwa kwa Programu ndogo ya ukuzaji viwanda (SR010201) ni ndogo na hivyo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019 imejipangia kuimarisha Taasisi ya SMIDA ambayo imeanza kazi zake rasmi mnamo tarehe 1 Julai 2018. Aidha pia Wizara itaimarisha maeneo tengefu ya viwanda kwa ajili ya wajasiriamali wadodo wadogo ambao watazalisha bidhaa zitakazokuwa na viwango stahiki.
Wajumbe wameridhika na majibu ya Wizara na hakukuwa na mabadiliko yeyote. Aidha, Kamati imeshauri Serikali kuwa na mkakati wa kuendeleza maeneo tengefu yaliyotengwa pamoja na maeneo ya uwekezaji ya Micheweni, Amani na Fumba.
2. Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo imeshauri kusitishwa kwa mkataba baina ya Kampuni ya Jabal Kilimanjaro ya Dubai na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) inayohusiana na huduma ya ukaguzi wa magari yanayotaka kuingizwa nchini kutoka Dubai. Mkataba huo unaeleza kuwa asilimia 70 ya mapato ya shughuli hiyo yanaingia kwa Kampuni hiyo na asilimia 30 tu ndio inarudi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kamati imependekeza kusitishwa kwa Mkataba huo kwakuwa  Kiwango kinachoingia nchini ni kidogo mno.
Wizara imekiri juu ya kuwepo kwa matatizo katika mkataba uliofungwa baina ya Kampuni ya Jabal Kilimanjaro ya Dubai na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) na kuomba kuwa mkataba huo usivunjwe kwasasa, kwa kuwa  unatarajiwa kumaliza muda mnamo 2020 na Wizara imeahidi kurekebisha kasoro zilizojitokeza pindi watakapofunga mkataba mwengine.
Hoja imekubaliwa na wajumbe wa Kamati na pia kuomba kupatiwa nakala ya mkataba uliofungwa kwa lengo la kujiridhisha. Aidha, Kamati inasisitiza umuhimu wa kushirikishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika kufunga mikataba ili kuepukana na mikataba isiyo na manufaa na Serikali.
9.WIZARA YA VIJANA UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO
1. Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii, haikuridhishwa na bajeti inayotengwa katika kuendeleza michezo hapa nchini. Kwa msingi hu Kamati imeomba Serikali kuongeza bajeti ya Michezo, ili kuondokana na tabia ya kuomba omba hasa pale timu zetu zinaposhiriki mashindano ya Kimataifa.Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Programu Ndogo ya Ukuzaji na uendelezaji wa Michezo imetengewa Tsh 368,400,000/-.
Wizara imeiarifu Kamati kuwa imejipanga vyema kwa bajeti ya Michezo na hivyo kwa mwaka huu wa fedha timu ya taifa itahudumiwa vizuri na kasoro zilizojitokeza katika kipindi cha nyuma zitarekebishwa.
Kwa kuwa Idara ya Michezo imetenga bajeti ya milioni 290 kwa ajili ya Timu ya Taifa, Kamati inasisitiza fedha hizo zitumike kama zilivyokusudiwa kwa ajili ya kuleta ufanisi katika sekta ya michezo na hivyo Kamati imeridhika na hoja hiyo.
2. Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii haikuridhishwa na kiwango cha Bajeti iliyotengwa kwa Idara ya Maendeleo ya Vijana, kulingana na Idadi ya Mabaraza ya Vijana yaliyopo nchini, ambapo Kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 Programu ya Maendeleo ya Viajana imepangiwa Tsh 457,448,000/ pekee.  Kamati imeshauri Bajeti hii iongezwe kwa kiwango kikubwa zaidi katika miaka ya usoni ili Idara iweze kuendesha Mabaraza mengi zaidi pamoja na miradi ya maendeleo inayoanzishwa kupitia mabaraza hayo pamoja na kuiwezesha kutatua changamoto zao ikiwemo kukosa ofisi  na kupata sehemu ya kufanya vikao vyao.
Wizara imeiarifu Kamati kuwa katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 fedha walizopatiwa Baraza la Vijana zimefikia asilimia 70, ambalo miongoni mwa majukumu ya Baraza la Vijana ni kuratibu shuguli za vijana  ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo ya vijana ikiwemo ukosefu wa ajira, hivyo Bajeti hiyo inatosha kwa shughuli zilizopangwa.
Hoja imekubaliwa na Kamati bila ya marekebisho yoyote.
10.WIZARA YA  UJENZI MAWASILIANO NA USAFIRISHAJI
1. Wajumbe wengi wamehoji kuhusu ubora wa Barabara zinazojengwa kutokana na kuharibika mara kwa mara hususan kipindi cha mvua, ambapo ukarabati unaofanywa kila zinapoharibika  unaigharimu Serikali fedha nyingi. Aidha, Wajumbe wamelalamikia kuchelewa kulipiwa fidia kwa baadhi ya barabara licha ya agizo la Mhe. Rais la kutaka barabara zote zilipiwe fidia.
Wizara imeieleza Kamati kuwa kuharibika kwa barabara kunatokana na matumizi mabaya ya barabara hizo ikiwemo kuongezeka kwa magari yenye uzito mkubwa ukilinganisha na uwezo wa barabara na pia barabara zinazoharibika nyingi zao zilijengwa zamani. Aidha, Wizara imejipanga kuunda Kamati Maalum ambayo itajihusisha na usimamizi wa ujenzi wa Barabara.
Kuhusiana na Fidia Wizara itajitahidi katika kulipa fedha hizo na kumalizia madeni katika mwaka huu wa fedha.
Kamati inaisisitiza Wizara juu ya kusimamia ujenzi wa barabara bora na imara. Aidha, Kamati imeshauri Wizara kuwa makini katika kuingia mikataba na kamapuni zinazojenga barabara hizo kwa kuhakikisha kuwa zinajengwa katika kiwango stahiki.
2. Kamati ya Ardhi na Mawasiliano imependekeza kuharakikisha kuifanya Karakana ya magari kuwa Mamlaka ili iweze kuwa na maamuzi na kuimarisha utendji kazi wake, hatua ambayo itaipunguzia Serikali gharama kutokana na hali iliyopo sasa ambapo magari mengi hupelekwa Gereji za watu binafsi kutokana na ukosefu wa vifaa vya kutosha katika karakana ya Serikali.
Wizara kwa hatua ya awali imelekezwa na Serikali kuwa Karakana zote za Mawizara zitaunganishwa na kuwa chini ya Karakana kuu. Aidha, kwa sasa Serikali imeagiza kuwa gari zote za Serikali zinatakiwa kufanyiwa matengenezo katika karakana za Serikali badala ya kupelekwa kwenye karakana za watu binafsi.
Kamati inashauri kuwepo na mkakati mzuri wa kusimamia malipo ya gari za Serikali zinapopelekwa karakana kwa ajili ya matengenezo ili kudhibiti matmizi mabaya ya fedha.
11. WIZARA YA AFYA
1. Kamati ya Ustawi wa Jamii haikuridhishwa na bajeti iliyopangiwa Programu ya Kinga na Elimu ya Afya ambayo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 imetengewa Tsh bilioni 19,669,126,000/- sawa na asilimia 19.4 ya bajeti ya Wizara. Hivyo, Kamati imependekeza kwa mwaka ujao wa fedha bajeti ya Programu hii iongezwe ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kutekelezwa kwa ufanisi.

Wizara imeihakikishia Kamati kuwa fedha iliyotengwa kwa Programu ya Kinga na Elimu ya Afya inatosheleza katika kutekeleza majukumu ya programu hiyo. Aidha, programu ya Huduma ya Afya ya Msingi ambayo ilikuwa katika programu hiyo imegatuliwa katika Halmashauri na kwa msingi huo fedha zilizopo zinatosheleza. 

Kamati imeridhia na ufafanuzi wa majibu ya Wizara.
2. Pamoja na juhudi zilizochukuliwa na Serikali za kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya hasa katika ununuzi wa dawa, bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa katika Hospitali na vituo vya Afya. Kutokana na changamoto hiyo, Wajumbe wengi wamelihoji juu ya usimamizi na utaratibu mzima unaotumika katika usambazaji wa dawa kutoka Bohari kuu kwenda katika vituo vya Afya.
Wizara imeeleza kuwa Utaratibu uliokuwepo sasa ni kwamba dawa zinapelekwa katika kila kituo cha afya kwa mujibu wa maombi yanayopelekwa Bohari ya madawa kwa mujibu wa mahitaji yaliyopo. Utaratibu huo unatumika kwa vituo vyote na Hospitali kubwa kama ya Mnazi mmoja ambayo kwa kawaida huwa wanaagiza dawa mara moja au zaidi ya mara 15 kwa mwezi. Aidha, kwa sasa bohari wanatumia mfumo wa M-system ili kufahamu dawa zilizotoka, kiwango chake na  hospitali iliyopokea dawa hizo. Lakini pia kunatumika Mfumo wa Electronic Logistic Management  Information System (eLMIS) kuagiza madawa bohari.
Hivyo, kuna dawa za kutosha katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na japo kuna changamoto ndogo ndogo, kwa sasa Serikali imefikia zaidi ya asilimia 80 ya upatikanaji wa dawa katika mahospitali japokuwa kuna changamoto ndogo ndogo zinazoendelea kufanyiwa kazi.

Kamati imeridhika na majibu ya Wizara na pia inaitaka Kamati husika ya Kisekta kufuatilia kwa karibu suala hili.
3. Kamati ya Ustawi wa Jamii imeishauri Serikali kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni kutokana na ukweli kuwa kwa bajeti iliyotengwa mwaka huu wa fedha hazitotosha kuanza ujenzi mkubwa wa hospitali hiyo ambayo inatarajiwa kuwa ya kisasa na yenye vifaa vingi vya gharama kubwa.Mradi huu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 umepangiwa bajeti ya Tsh 14,000,000,000/- bilioni.
Fedha zilizotengwa kwa mradi wa ujenzi wa hospitali hii ni Tsh bilioni 4, lakin pia kumetengwa jumla ya Tsh. bilioni 15 kutoka kwa washirika wa maendeleo, hivyo  ni imani ya wizara kuwa fedha hizo zitatosha kwa awamu ya mwamzo “phase one” ya mradi huo, Aidha Kamati Maalum imeundwa ili kuhakiksha mradi huo unakwenda vizuri katika utekelezaji wake.
Kamati imeridhika na ufafanuzi uliotolewa na Wizara na kuagiza Kamati ya kisekta ifuatilie suala hilo zaidi.
12. WIZARA YA ARDHI, NYUMBA, MAJI NA NISHATI
1.Wajumbe walihoji juu ya gharama kubwa wanayoibeba wananchi wakati wa kuunganishiwa  huduma za umeme. Pamoja na utaratibu unaotumika wa kuunganishwa na huduma hiyo kwa mkopo kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama hizo papo kwa papo, ambapo wamelalamikia utaratibu huo kuwa hauwapi wananchi unafuu katika kupata huduma hiyo.
Kamati imeelezwa kuwa gharama wanazoingia wananchi ni gharama za mwisho za kuunganishwa (Point of end user) hatua ambayo Shirika limefikisha miundombinu ya umeme kuelekea eneo ambalo wananchi wanahitaji kutumia huduma hii.
Hivyo, kwa wananchi ambao wanahitaji huduma kutoka (Point of end user), hulazimika kuchangia gharama za kuufikisha umeme huo sehemu anayohitaji, lakini kwa kuzingatia hali za wananchi kunakuwepo na punguzo la gharama hizo. Shirika pia lina utaratibu wa kuwaunganishia wananchi na huduma ya umeme kwa mkopo usiokuwa na riba kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo.
Kamati imeshauri kuwa mkakati wa kusambaza umeme vijijini usiwe umeelekea eneo moja tu bali uzingatie mikoa na maeneo yote kwa ufanisi zaidi. Aidha Kamati ilisisitiza kuwa Shirika liendelee kutoa unafuu wa huduma za umeme hususan kwa kaya maskini ambazo mara nyingi inakuwa ni vigumu kuunganishwa na huduma hii.

2.Wajumbe wengi walihoji juu ya kadhia inayowakabili watendaji wa Mamlaka ya ZAWA kulipwa mishahara ya kima cha chini ambayo ni chini ya Tsh. 300,000 kinyume na agizo la Serikali lililotokana na ahadi ya Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambalo lilielekeza kuanza kulipa mishahara ya 300,000 kwa watendaji wa kima cha chini. Aidha, Wajumbe walihoji juu ya kadhia ya upatikanaji wa maji licha ya kuwa kumekuwa na miradi mingi ya maji na fedha nyingi zinatengwa kwa ajili ya kuimarisha huduma hiyo.
Mamlaka imeeleza Kamati kuwa ilishindwa kulipa mshahara wa kima cha chini cha laki tatu kutokana na kutoongezewa ruzuku yake ya 2.5 bilioni kwa mwaka 2017/2018. Aidha, pamoja na kuwaandikia Kamisheni ya Utumishi wa Umma mara tatu bado hawajapatiwa muungozo wa kulipa mishahara hiyo. Kwakuwa kwa mwaka 2018/2019 ruzuku ya Mamlaka imeongezwa wanategemea kuweza kulipa mishahara hiyo, baada ya kupata Muungozo kutoka Kamisheni ya Utumishi wa Umma pamoja na Idhini ya Bodi ya Shirika. Kuhusu malimbikizo ya mishahara ya ZAWA kwa mwaka 2017/2018 ZAWA kwa kuwa wanapokea karibia 80 asilimia ya fedha zake kutoka Serikalini, hivyo kwa sasa hawataoweza kulipa malimbikizo ya wafanyakazi kwa mwaka 2017/2018
 Kuhusu changamoto ya maji, Mamlaka imeelezea kuwa miradi mingi ipo katika hatua nzuri isipokua miundimbinu ya maji mingi ni chakuvu na hivyo kupelekea upotevu mkubwa wa maji.
Kamati imemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara afuatilie suala la mishahra ya kima cha chini kwa mujibu wa agizo la Serikali katika kamisheni ya Utumishi wa Umma. Aidha kuhusu changamoto ya maji Kamati  imemuagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Kisekta afuatilie miradi ya ZAWA ambayo haijakamilika
13. WIZARA YA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI
1.      Wajumbe wengi walichangia juu ya kilimo cha mwani ambacho kimeajiri wanachi wengi katika maeneo ya pwani, licha ya kukabiliwa na changamoto ya bei ambayo haiendani na uhalisia wa ugumu wa kilimo chenyewe.Wajumbe walihitaji kufahamu Serikali ina mipango gani ya kuimarishaa zao hilo ili kuwanufaisha wananchi waliojiajiri kupitia sekta hiyo.
Wizara imeiarifu Kamati kuwa, inashajihisha wakulima wa mwani kujihusisha zaidi na kilimo cha mwani mnene katika kina mrefu cha bahari ambao una bei kubwa zaidi badala ya kulima mwani mwembamba ambao una bei ndogo katika soko la dunia. Aidha, Wizara wanashajihisha wawekezaji kuekeza viwanda vya kusarifu mwani kwa matumizi mbali mbali na pia inatoa taaluma kwa wananchi kufanya matumizi tofauti ya bidhaa zinazotokana na mwani ili kuongeza matumizi ya ndani ya nchi badala ya kusafirisha mali ghafi nje ya nchi.
Katika kuwahamasisha wananchi kusarifu zao la mMwani, Wizara iwawezeshe kwa kuwapatia taaluma pamoja na vifaa vya kuweza kusarifu. Aidha, Wizara iwafutoia wakulima wa mwani soko la uhakika ili waweze kuhamasika katika kukiendeleza kilimo hicho.
14.WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
1. Licha ya kuwepo mahitaji makubwa ya matengenezo ya barabara, fedha zilizotengwa kwa bajeti ya 2017/2018 kupitia Mfuko wa Barabara zilitumika kwa kiwango kidogo sana (asilimia 26). Changamoto kama hiyo pia ilijitokeza katika Utekelezaji wa Programu ya Kuimarisha mambo ya Kale ambapo marekebisho ya Makumbusho ya Bihole na Makumbusho ya Dunga hayakufanyika kutokana na kutokamilika kwa utaratibu wa manunuzi (procurement). Changamoto hizi za manunuzi hazileti taswira nzuri katika utekelezaji wa bajeti na pia zinaweza kuathiri mipango ya maendeleo tunayojipangia kwa kuchelewa kutekeleza kwa wakati miradi inayopangwa.
Kuhusu changamoto iliyojitokeza ya fedha za mfuko wa barabara kutokutumika Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais, tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji watakaa pamoja kuzitatua changamoto zilizojitokeza za Mfuko wa Barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha hizo.
Kamati imeridhika na ufafanuzi uliotolewa na Wizara na imeitaka Serikali kuhakikisha kuwa changamoto hii inapatiwa ufumbuzi.
2. Wajumbe walitaka kupatiwa ufafanuzi juu ya fedha za mauzo ya zao la karafuu kwa mwaka 2017/2018 yaliyofikia jumla ya Tsh. bilioni 118.7 kwa tani 8,508.45 ambazo kimsingi zimekua hazionekani katika mzunguko wa fedha katika mabenki hususan kwa upande wa Pemba.
Wizara imeeleza kuwa itaiomba Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kufanya utafiti utaolenga kufaham mzunguko wa fedha za mauzo ya karafuu unavyokwenda
Kamati imeridhia na majibu ya hoja. Aidha, inapendekeza suala la kufanya malipo ya mauzo ya karafuu kwa njia ya benki yazingatiwe.

USHAURI WA JUMLA WA KAMATI
Mheshimiwa Spika,
Kamati ya Bajeti inaendelea kutoa wito kwa Afisi ya Baraza na Serikali kwa ujumla kuzifanyia kazi changamoto za Kamati ya Bajeti ikiwemo changamoto ya kutokuwepo Sheria ya Bajeti pamoja na Ofisi ya bajeti kwa ajili ya kuisaidia Kamati katika utekelezaji wa majukumu yake. Mheshimiwa Spika, uzoefu unaonesha kuwa, katika mabunge mengi Kamati ya Bajeti inawekewa Sheria ya Bajeti ambayo inatoa Mamlaka kwa Kamati juu ya kuongeza au kupunguza fedha katika mafungu ya bajeti kutokana na mapendekezo ya Wajumbe na Kamati za kisekta katika mijadala ya Bajeti. Aidha mabadiliko ya Kanuni yaliyofanyika hayajajitoshelaza katika kuipa nguvu na kuiwekea utaratibu mzuri wa kazi Kamati hii katika kushughulikia masuala ya bajeti.
Mheshimiwa Spika, kupitia marekebisho ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi ya mwaka 2016, tumeanzisha mfumo mpya wa upitishaji wa bajeti pamoja na kuunda Kamati ya Bajeti ambapo kwa sasa bajeti kuu hupitishwa mwisho baada ya mijadala ya Wizara zote, tofauti na ilivyokuwa awali. Hata hivyo, mabadiliko hayo hayajasaidia Wajumbe wako pamoja na Kamati ya Bajeti kuweza kufanya mabadiliko ya vifungu baada ya Kamati ya Matumizi kuidhinisha. Hivyo kuna kila sababu ya kujifunza zaidi ili dhamira ya kuanzisha mfumo huu iweze kufikiwa.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika,
Baada ya uwasilishaji wa hoja naomba nimalizie kwa kukushukuru tena kwa kunipatia nafasi hii ya kuwasilisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya bajeti ya mwaka 2018/2019. Aidha, napenda pia kuwashukuru wajumbe wote kwa kunisikiliza kwa utulivu na umakini.
Naomba kuwasilisha.
Ahsante,

Mohamed Said Mohamed,
Mweyekiti,
Kamati ya Bajeti,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.