Habari za Punde

Tanzania Yanufaika na Mradi wa Uchumi wa Buluu

Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI) Prof. Tumaini Gurumo akiwasilisha Mradi wa Uchumi wa Buluu na Kituo cha Mafunzo unaolenga kuimarisha rasilimaliwatu, teknolojia safi na ustawi wa jamii katika sekta ya bahari, wasilisho alilofanya kwenye banda la maonesho la Tanzania kwenye Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.

Serikali ya Tanzania kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) imenufaika na Mradi wa Uchumi wa Buluu na Kituo cha Mafunzo unaolenga kuimarisha rasilimaliwatu, teknolojia safi na ustawi wa jamii katika sekta ya bahari.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo cha DMI Prof. Tumaini Gurumo alipowasilisha mradi huo wakati wa mkutano wa pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo wenye thamani ya dola milioni 65.26 Prof. Tumaini amesema matumizi ya boti za umeme yatapunguza gharama za uendeshaji kwa wavuvi kwa takriban asilimia 50 kutoka wastani wa dola 12,800 hadi 6,400 kwa mwaka.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huu, Chuo cha DMI kitapata meli ya kisasa ya mafunzo yenye ukubwa wa 7,500 GT, kituo cha ubunifu na ujenzi wa boti za umeme, pamoja na mtandao wa vituo 15 vya huduma baada ya mauzo na vituo vya kuchaji boti za umeme.

“Kwa kipindi cha miaka mitano, mradi unatarajiwa kutoa zaidi ya wataalam 3,000 wa mabaharia, wahandisi na mafundi baharini, ujenga na kupeleka boti 750 za kijani (green boats) zenye injini za umeme na kupunguza hewa ya ukaa kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka kwenye boti ndogo za kisasa,“ amesema.

Halikadhalika, Prof. Tumaini amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kaya 100 kwa mwaka katika kilimo cha mwani na ufugaji wa viumbe baharini kwa njia rafiki kwa mazingira pamoja na kujenga uwezo kwenye jamii kupitia mafunzo ya teknolojia safi, utafiti na ubunifu.

Amesisitiza kuwa mradi huo unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Uchumi wa Buluu 2024, Malengo ya SDGs 4, 8, 13 na 14, pamoja na malengo ya IMO ya kupunguza uzalishaji wa kaboni katika sekta ya bahari.

Aidha, Uchumi wa buluu ni eneo lenye fursa kubwa ambazo hazijatumika na zikitumika ipasavyo zitakuwa ni uti wa mgongo wa mageuzi ya maendeleo ya taifa kutokana na kuwepo kwa maeneo makubwa ya vyanzo vya maji.

Halikadhalika, Naibu Katibu Mkuu Mitawi alisema tayari Idara ya Uchumi wa Bluu imeanzishwa chini Ofsi ya Makamu wa Rais kwa lengo la kuratibu sekta zote zinazohusika na uchumi wa buluu.

Kutokana na umuhimu huo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeanzisha Kitengo mahsusi kwa ajili ya kuratibu uchumi wa buluu na pia Serikali ilizindua Sera ya Uchumi wa Bluu (2024) na Mkakati wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.