Habari za Punde

Balozi Seif afunga maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Tanzania

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Viongozi wa Wizara za Viwanda na Biashara na ule wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tan Trade} wakiingia kwenye majengo ya Maonyesho Mjini Dar  es salaam kabla ya kuyafunga rasmi.
 Balozi Seif akipata maelezo katika banda la bidhaa mbali mbali zinazotokana na Viungo kutoka Zanzibar kwenye Maonyesho ya Biashara Mjini Dar es salaam.
  Balozi Seif na ujumbe wake wakitembelea Banda la Shirika la Viwanda Vidogo vidogo Tanzania {SIDO} kabla ya kuyafunga Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashaara Tanzania.
 Mkufunzi wa Kiwanda Darasa cha washonaji wasioona Tanzania Dr. Abdullah Nyangaho akifanya vitu vyake huku akishangilia na Balozi Seif wakati alipofika kukagua shughuli zao kwenye Banda lao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif akipata maelezo kutoka kwa afisa wa Shirika la Viwango Tanzania {TBC} kabla ya kuyafunga Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Tanzania.
Picha na – OMPR – ZNZ

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaomba Watanzania wanaobahatika kuyatembelea Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es salaam kutumia ujuzi na maarifa wanayoyapata kwa kuanzisha Biashara itakayozingatia uzalishaji wa bidhaa za Kimataifa ili kukuza uchumi wa Taifa.
Alisema Watanzania hao wanapaswa kuyachukulia Maonyesho hayo kama Shamba Darasa la Biashara kwa kuanzisha Makampuni ya biashara yenye uhakika na kiwango.
Akiyafunga Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara katika Uwanja wa Maonyesho wa Mwalimu JK. Nyerere  Bara bara ya Kilwa Dar es salaam Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora na rafiki kwa lengo la kuifanya Sekta ya Biashara na Viwanda inakua na kuvutia Wawekezaji.
“ Serikali itahakikisha mazingira ya Biashara yanaimarika ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha Vijana, Wanawake na Watu waliopo katika Makundi Maalum kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa Sekta ya Biashara na Viwanda”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alisema hatua hiyo inayoelekea kuifanya Tanzania kuwa na Uchumi wa Kati kupitia Viwanda ifikapo Mwaka 2025 hatimae itasaidia kuongeza Mapato ya Taifa sambamba na kupunguza changamoto ya ajira inayolikumba kundi kubwa la Vijana.
Balozi Seif aliziomba Taasisi zinazojihusisha na Tafiti mbali mbali zizingatie Tafiti zinazotoa suluhisho kwa Changamoto zinazoikabili Sekta ya Viwanda na Biashara Nchini ili kuongeza Tija na ufanisi katika Maendeleo ya Taifa na Watu wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezipongeza juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tan Trade} kwa kushirikisha wadau wa Sekta ya Umma na hata Binafsi jambo ambalo limeleta mafanikio makubwa kwenye Maonyesho hayo.
Alisema mafanikio hayo yamejidhihirisha kutokana na ongezeko kubwa la Washiriki wa Maonyesho hayo yaliyoonyesha upevukaji mkubwa hasa ikizingatiwa kwamba Maonyesho hayo yamekuwa Jukwaa linalotegemewa na Wazalishaji pamoja na wadau wa Biashara ndani na nje ya Nchi kutangaza na kupanua wigo wa Masoko ya biadhaa na huduma zao.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na Maonyesho hayo kuzinduliwa muongozo wa kusimamia Ujenzi na Maendeleo ya Viwanda kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wenye lengo la kutoa utaratibu kwa Viongozi na Watendaji kusimamia ujenzi wa Viwanja kwenye maeneo yao wakiwa na uelewa mmoja.
Aliwanasihi Viongozi wa Mikoa, Wilaya pamoja na Halmashauri zote kupata makala ya muongozo huo na kuhakikisha unatumika ipasavyo katika kufanikisha Malengo ya Serikali Kuu ya kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya Viwanda.
Akizungumzia Kliniki ya Biashara itakayokuwa ikishughulikia na kutatua changamoto mbali mbali za Wafanyabiashara iliyoundwa na hatimae kuzinduliwa kwenye Maonyesho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wafanyabiashara kuitumia fursa hiyo katika kuzipatia suluhu kero zinazowakabili.
Balozi Seif aliwaomba waendeshaji wa Kliniki hiyo kuwatembelea wafanyabiashara Mikoani, Wilayani na Vijijini pamoja na Zanzibar kwa vile wafanyabiashara walio wengi bado hawajapata nafasi ya kuyatembelea Maonyesho ya saba saba kwa sababu tofauti.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tan Trade} Bwana Fransis Lukwalu alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara Tanzania  mwaka huu kuokana na ongezeka la washiriki mbali mbali kutoka ndani na nje ya Nchi.
Bwana Lukwalu alisema jumla ya Kampuni za Ndani ya Nchi 2,956, Kampuni za nje 508 ambapo zaidi ya Nchi 33 zimeshiriki maonyesho hayo ikilinganishwa na Makampuni ya ndani 2,500, Kampuni za nje 505 na Nchi 30 zilizoshiriki Mwaka 2017.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tan Trade} alieleza kwamba Uongozi wa Bodi hiyo umeamua Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara Tanzania kumalizia siku mbili za Mwisho ya Wiki hii ili kuwapa fursa Wananchi kukamilisha mahitaji yao ya kupata bidhaa kwenye mabanda mbali mbali ya Maonyesho.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuyafunga Maonyesho hayo Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhandisi Stela Manyanya aliwashukuru washiriki wa Maonyesho hayo kwa kuyaunga mkono jambo ambalo dhana ya uwepo wake imefikiwa Kimataifa.
Mhandisi Stela alisema Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tan Trade} itaendelea kuboresha Maonyesho hayo kwa kuangalia fursa za Uwekezaji katika Sekta ya Biashara na Viwanda Nchini.
Alielezea faraja yake kutokana na Uongozi wa Maonyesho hayo kuweka utaratibu muwafaka wa siku maalum kwa Makundi maalum kueleza malengo na mikakati yao kwenye maonyesho hayo yaliyoanza Tarehe 13 Juni hadi 13 Julai Mwaka huu wa 2018.
Alifahamisha kwamba washiriki hao wa maonyesho kupitia Makundi Maalum wameweza kutumia soko kwa kuuza bidhaa zao ndani ya maonyesho ya saba saba na kuwawezesha kujitanga zaidi kwa wateja.
Kwenye kilele cha Maonyesho hayo ya Kimataifa ya Biashara  Dar es salaam Makamu wa Pili wa Rais wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kukabidhi vyeti kwa Washindi wa vitengo mbali walioshiriki kwenye Maonyesho hayo.
Mshindi wa Kwanza wa Jumla ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania {NSSF}, wa Pili ni Shirika la Bima la Taifa Tanzania {NIC} wakati mshindi wa Tatu ni Shirika la Viwanda vidogo vidogo Tanzania { SIDO}.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.