Habari za Punde

Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Jumba la Treni Darajani leo.

 Muonekano wa Jumba la Treni darajani litavyokuwa likiwa katika hatua za mwisho za kukamilika matengenezo makubwa yanayofanywa chini ya Wahjandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CRJE kutoka China.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifanya ziara fupi ya kukagua maeneo mbali mbali yaliyomo ndani ya Jumba la Treni Darajani linalotarajiwa kukamilika hivi karibuni.


Balozi Seif akisisitiza umuhimu wa kuzingatia utunzaji wa mazingira katika eneo la Jumba la Treni Darajani ambalo ndilo sura halisi ya muonekano wa Mji wa Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Huduma za kibiashara katika Nyumba Maarufu  iliyopo kati kati ya Kitovu cha Biashara Zanzibar hapo Darajani Maarufu Jumba la Treni zinatarajiwa kuanza Rasmi wakati wowote mara baada ya kukamilika kwa matengenezo ya Jengo hilo sambamba na upembuzi wa majina ya Wafanyabiashara walioomba nafasi katika jengo hilo.
Ujenzi wa jengo hilo unaosimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} chini ya Wahandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya CRJ kutoa  Jamuhuri ya Watu wa Nchini China unatarajiwa kukamilika Wiki ya Pili ya Mwezi ujao wa Nane Mwaka huu.
Kaimu Meneja Mipango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Ndugu Abdul -aziz Ibrahim Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa ziara fupi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya kukagua hatua za mwisho za matengenezo makubwa ya Jengo hilo la Kihistoria Zanzibar.
Akimtembeza Balozi Seif  pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali katika maeneo tofauti ndani ya Jengo hilo Meneja Mipango huyo wa ZSSF Nd. Ibrahim alisema ushauri wa Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni {Unesco} wa kuagiza mbao maalum zinazopaswa kutumika katika jengo hilo ndio ulioongeza muda kidogo wa kukamilika kwa kwa wakati kwa Matengenezo hayo.
Nd. Ibrahim alisema mbao za Milango inayokusudiwa kufungwa ndani ya Maduka yaliyomo kwenye Jumba hilo zimeshawasili Bandarini Malindi anzibar na kazi ya kuzifunga katika maduka hayo itaanza wakati wowote kuanzia sasa.
Alisema Jumba hilo litakuwa na Maduka 58 ambayo kati yake Matano yatarejeshwa kwa wamiliki wa mwanzo waliokuwa wakifanya biashara kwa mujibu wa kanuni za Mikataba na 53 yaliyobakia ndio yaliyotangazwa kukodishwa kwa Wafanyabiashara waliojitokeza kuomba.
Alieleza kwamba zipo Nyumba 10, sehemu ya kufanyia mazoezi {Gims}, Mkahawa pamoja na Super Market ambavyo vyote hivyo vimo katika mtiririko huo wa kutolewa matangazo ya kukodishwa kwa Wananchi mbali mbali.
Meneja Mipango huyo wa ZSSF alisisitiza kwamba Wafanyabiashara wa mwanzo waliokuwa wakiendesha huduma za Biashara kwenye Jengo hilo lililotengenezwa kuhimili uzito wa Watu watakaoingia humo kupata huduma mbali mbali watapewa upendeleo wa kwanza.
Alieleza kwamba wale wafanyabiashara watakaobahatika kupata milango ya duka katika jumba hilo wanapaswa kufahamu kwamba huduma za Biashara zitaanza siku litakapofunguliwa rasmi.
Akitoa shukrani zake kwa Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar na Kampuni ya wahandisi wa Ujenzi huo CRJ, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha umuhimu wa kutunzwa kwa Jengo hilo katika azma ya kuzingatia mazingira halisi ya eneo hilo.
Balozi Seif alisema Serikali kupitia Taasisi zake mbali mbali imekuwa ikiimarisha ujenzi wa Majengo mbali mbali  kwa lengo la kuwarahisisha Wananchi walio wengi Mjini na Vijijini kupata huduma za msingi ikiwemo zile za Biashara.
Aliwanasihi Wafanyabiashara watakaobahatika kupata nafasi katika eneo hilo kuzingatia ulipaji wa Kodi kwa wakati  na kuushauri Uongozi wa ZSSF kupanga utaratibu utakaowapa fursa nzuri  Wafanyabiashara hao kulipa Kodi kila baada ya miezi sita badala ya mpango wa kwanza wa Mwaka Mmoja ili kuwapunguzia mzigo mkubwa Wafanyabiashara hao.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliitaka ZSSF isisite kuvunja Mkataba kwa Mfanyabiashara ye yote atakayekiuka masharti yaliyowekwa kwenye Mkataba husika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.