Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Afunga Mkutano wa Vyama Vya Kisiasa Afrika na CPC.

HOTUBA YA MHESHIMIWA BALOZI SEIF ALI IDDI, MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR ALIYOITOA KUFUNGA MKUTANO WA PAMOJA WA VYAMA VYA SIASA KUTOKA NCHI MBALI MBALI BARANI AFRIKA NA CHAMA CHA KIKOMUNISTI CHA CHINA (CPC) KATIKA HOTELI YA SERENA JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 18 JULAI 2018

Ndugu Song Tao, Waziri wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa
wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC),
Ndugu Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
Ndugu Xu Luping, Naibu Waziri wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC),
Ndugu Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa kutoka kote Barani Afrika,
Ndugu Mabalozi, Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia na kutuwezesha kuwa wazima na afya njema tukaweza kuhudhuria mkutano huu muhimu kwa kuimarisha ushirikiano wa kidugu wa Vyama vyetu vya siasa, na pia kuimarisha uhusiano kati ya nchi za Afrika na China. Hatuna budi kukumbuka na kuzitambua jitihada za Waasisi wa Vyama vyetu kwa juhudi zao za kupigania uhuru wa nchi zetu. Kabla sijaendelea mbele, naomba mzipokee salaam za Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.  Mheshimiwa Rais anautakia mkutano huu mafanikio makubwa.

Ndugu Wajumbe wa Mkutano,
Natoa shukurani zetu za dhati kwa utambuzi maalum uliotolewa  katika risala za Vyama vyote vya Siasa vilivyoshiriki kwa Waasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuitoa muhanga Tanzania na kuwa mlezi wa mstari wa mbele wa kusimamia  ukombozi wa Bara la Afrika mpaka imehakikisha kuwa Afrika yote imekuwa huru.  Lakini pia, Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka “kuwa pamoja na nchi yetu imekuwa huru, lakini uhuru huu haujakamilika na hauna maana kama nchi nyingine za Afrika bado zinatawaliwa.”  Sasa ni kweli tuko huru  kisiasa, kijamii na kiutamaduni, lakini ni ukweli usiopingika kuwa bado tunahitaji kuwa huru kiuchumi.

Ndugu Wajumbe wa Mkutano,
Madhumuni ya maamuzi ya awamu ya pili ya ukombozi ni safari ya kujikomboa kiuchumi ambayo haitakamilika kama hatutosimama imara kupiga vita rushwa, ufisadi, kusimamia uwajibikaji, utawala bora, juhudi za ubunifu na utendaji wenye kuleta matokeo mema na yenye tija kwa nchi zetu na watu wake.

Nami naungana na Mwenyekiti wetu wa Chama chetu cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa nchi yetu Dkt. John Pombe Magufuli kuwashukuru kwa dhati waandaaji wa Mkutano huu Ndugu zetu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) chini ya uratibu wa Chama cha Mapinduzi kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya ambayo yamesaidia mkutano huu kufanyika kwa ufanisi mkubwa.  Hongereni sana Ndugu zetu kutoka CPC na CCM.
Ndugu Washiriki wa Mkutano,
Ni kawaida kwa binaadamu kupenda kuhusishwa na mambo mema yenye mafanikio.  Hakika nimefarajika sana na kujisikia nimepewa heshima kubwa kualikwa  kuufunga mkutano huu muhimu ambao umefanyika katika mazingira ya uelewano, mshikamano, udugu na upendo wa hali ya juu, mambo ambayo yameufanya mkutano huu kuwa wa mafanikio makubwa na yenye matarajio makubwa katika mustakabali mzima wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nchi zetu.

Ndugu Washiriki wa Mkutano,
Katika suala la ukombozi wa kiuchumi tuna kila sababu ya kujifunza kutoka Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambacho kimeendesha Mapinduzi ya uchumi ya aina yake ambayo hayajapata kushuhudiwa duniani kote. Nchi ya China chini ya Chama cha CPC imeweza kuwakomboa wananchi wake wapatao 800 Milioni walipoanza mapinduzi ya kiuchumi kutoka katika dimbwi la umasikini katika kipindi kifupi.  Hivi sasa China watu wapatao Bilioni 1.2 ambao wanaendelea kunufaika mapinduzi hayo.  Juhudi hizi zilizochukuliwa na China zimeiwezesha dunia kupunguza umasikini uliokithiri kutoka asilimia 40 hadi 10 au zaidi.  Kama siyo China hali ya umasikini wa kupindukia duniani bado ingekuwa juu ya asilimia 10. Hivyo basi, kama kungekuwa na kombe la dunia la ushindi wa kuboresha uchumi imara basi kombe hilo lingekwenda kwa Jamhuri ya Watu wa China.
Hakika China ni ndugu, sio rafiki kwa Tanzania.  Nchi yetu chini ya udugu wetu imekuwa ikipokea misaada ya hali na mali kutoka China.  Kwa upande wa Tanzania Bara tumenufaika na miradi mikubwa mikubwa yenye kuacha alama za kudumu zenye kuashiria udugu wetu, kama vile  ujenzi wa reli ya TAZARA, majengo ya mikutano kama vile kumbi za Mwalimu Nyerere na Jakaya Kikwete.  Kwa upande wa Zanzibar tumekuwa tukipokea madaktari kutoka China tangu mwaka 1964, tumejengewa uwanja wa kisasa wa Amani na Mao Tse Tung, Kiwanda cha Sukari, Mahonda, nyumba za makaazi ya wananchi na miradi mbali mbali ya maendeleo.  Naamini miradi kama hii pia inatekelezwa na ndugu zetu wa China katika nchi nyingi za Afrika.  Ni wajibu wetu kuonesha utamaduni wa kiafrika kwa kukithamini unachotendewa na rafiki yako “A friend in need is a friend indeed”.

Ndugu Washiriki wa Mkutano,
Mkutano huu naamini ulifanya majadiliano ya kina kuhusu wapi Vyama vyetu vinatoka, wapi vipo na wapi vinakusudia kwaenda.  Kwa upande wa maazimio yaliyopitishwa kuhusu wapi Vyama vyetu vinapotaka kuelekea, nawaomba Ndugu Wajumbe twendeni tukatekeleze kwa vitendo yote yale tuliyokubaliana kutekeleza katika mkutano huu.   Nimeambiwa kuwa mada zote zilizotolewa ambazo zimezaa maazimio hayo, zilitolewa kwa makini, ukweli na uwazi. Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati watoa mada wetu wote hao.

Naamini tukiyatekeleza kwa dhati maazimio yote hayo, nchi zetu zitapata mafanikio makubwa.  Wahenga wa Kichina wanasema “Empty talk harms the country while hard work makes it flourish”.  Kwa tafsiri ya Kiswahili isiyokuwa rasmi usemi huu unasomeka “nchi hustawi kwa vitendo na siyo maneno matupu”.  Kwa hivyo, tukayatekeleze maazimio hayo kwa vitendo ili nchi zetu zistawi.



Ndugu Wajumbe wa Mkutano,
Uzoefu wetu wa kuja kwa Vyama vyengine visivyokuwa vya ukombozi katika jukwaa la kisiasa Barani Afrika unaonyesha kuwa Vyama vyetu vya kisiasa vilivyoleta uhuru hasa Barani mwetu vinapigwa vita na mabepari na mabeberu duniani.  Vita hivi vina lengo la kuviondoa madarakani Vyama hivi. Sisi Watanzania tunaamini vita hivi vitashindwa kama Vyama vyetu vitaendelea kuwa Vyama vyenye kutetea maslahi ya wanyonge kwa kupiga vita rushwa, kuhimiza utendaji kazi kwa maslahi ya wengi, kuhimiza elimu pamoja na kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani. 

Kwa bahati nzuri Chama cha Mapinduzi CCM tangu kuanzishwa kwake kimekuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa kwa nguvu zake zote. Chini ya Mwenyekiti wetu, Dkt John Pombe Magufuli vita dhidi ya rushwa vimeimarishwa nchini pamoja na kuongeza kasi ya usimamizi wa utendaji kazi wenye kuleta tija chini ya bango la Hapa Kazi tu.  Juhudi hizi za Mwenyekiti wetu zimezaa matunda na kama alivyoeleza katika hotuba yake ya ufunguzi uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kubwa.

Ndugu Washiriki wa Mkutano,
Tumekutana hapa pamoja na mambo mengine tukiwa na dhamira ya kudumisha na kuendeleza umoja mshikamano wa Vyama vya Ukombozi.  Ni matumaini yangu mkutano huu umeweka misingi imara ya kuendeleza umoja na mshikamano huu kwa maslahi ya wanachama wetu na nchi zetu na zote tunaondoka hapa tukiwa na nia ya kudumisha umoja wetu.

Kabla sijamalizia hotuba yangu sina budi kupongeza tukio muhimu sana la kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Chuo cha Mwalimu Nyerere.  Naamini Chuo hiki kitakuwa ni kielelezo tosha kwa ukombozi wa umoja wetu. Lakini pia kitakuwa ni tanuri la kuwafunda vizazi vyetu juu ya uzalendo, itikadi, ujasiri na maarifa ya kimapinduzi ya kiuchumi na kupambana na ukoloni mamboleo.  Chuo hiki kitachukua nafasi ya Chuo chetu cha zamani cha Kivukoni ambacho kilitumika kuwafunda vijana wetu na hata wazee kisiasa na kiitikadi.

Kwa kumalizia hotuba yangu hii, nawakaribisha  kwa mara nyengine tena kutembelea Tanzania katika mbuga za Ngorongoro, Manyara, Serengeti na mlima wa Kilimanjaro pamoja na Zanzibar Kisiwa cha viungo (Spices Island) na fukwe za mchanga mweupe.  Nawashukuru sana waandaaji wa mkutano huu ambao umevikutanisha vyama ambavyo vimezikomboa nchi zetu katika kipindi ambacho ukoloni ulishaota mizizi Barani Afrika.

Mwisho kabisa, nawatakia Wajumbe wote waliotoka nje ya Tanzania, warudi salama.
Baada ya maelezo hayo mafupi, sasa kwa heshima na taadhima natamka kwamba Mkutano wa Vyama vya Siasa vya ukombozi kutoka nchi mbali mbali za Afrika na Chama cha Kikomunisti cha China umefungwa rasmi.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika,
Mungu ubariki uhusiano wetu na Watu wa China,
Mungu ubariki uhusiano wetu wa Vyama vya ukombozi Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.