Habari za Punde

Serikali kukisaidia Kiwanda cha Sukari Mahonda kujiendesha kibiashara


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAAMUZI YA SERIKALI YA KUKISAIDIA KIWANDA CHA SUKARI CHA MAHONDA KUKILINDA NA KUJIENDESHA KIBIASHARA

Ndugu Waandishi wa Habari
Kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa tukiwa wazima wa afya na tunaendelea vizuri na harakati za ujenzi wa taifa letu.

Kwa kipindi kirefu Serikali ya Mapinduzi imechukua hatua za makusudi za kuinua uchumi wa nchi katika sekta mbali mbali za kilimo, huduma na viwanda na hivi sasa Serikali inajitahidi kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika katika Sekta ya Viwanda.

Kwa mantiki ya kufikia lengo hilo Serikali imefanya jitihada kubwa ya Kukimarisha pamoja na viwanda vyengine kiwanda cha Sukari cha mahonda kwa kukipatia wawekezaji ambao watahakikisha wanakiimarisha, kukilinda na kuongeza uzalishaji.

Ndugu Waandishi wa Habari
Serikali imetafakari kwa kina haja ya kukilinda kiwanda hiki kwa madhumuni ya kulinda ajira za moja kwa moja za vijana wetu na zile ajira ambazo wananchi wengi watafaidika nazo kwa vile wataweza kuongeza uzalishaji wa miwa na kuwa na uhakika wa kupata soko. Hii inatokana na uzalishaji wote wa miwa utakaozalishwa ndani ya Zanzibar utauzwa katika kiwanda hicho.

Aidha, kiwanda hiki kimejikita katika mapinduzi makubwa ya kilimo cha kijani kwa kuwashirikisha vijana katika program zake mbali mbali. Kuongezeka kwa uzalishaji wa miwa itapelekea kiwanda kuzalisha umeme ambao baadhi utatumika kwa uzalishaji kiwandani na mwengine utatumika kwa wananchi.

Madhumuni ya Serikali kuweza kufikia lengo la kukisaidia na kulinda ajira za vijana wake, kwa hatua za muda mfupi Serikali itahakikisha Sukari yote ambayo inazalishwa na kiwanda cha Mahonda inapata soko lake ndani ya Zanzibar, hali hii itapelekea kiwanda kuendelea na uzalishaji na kuimarisha ajira na kipato kwa wananchi wapatao 4000 wanaoshiriki katika uzalishaji wa miwa.

Ndugu Waandishi wa Habari
Madhumuni makubwa ya kuwaiteni hapa leo tarehe 3/7/2018 ni kuwafahamisheni dhamira hiyo ya Serikali na kuwapa taarifa wafanya biashara wetu wakubwa (waagiziaji) wa Sukari kuwa Serikali imeweka utaratibu maalumu wa kuwapatia waagiziaji maalumu kibali cha uagiziaji wa Sukari kutoka nje kwa masharti kuwa watainunua sukari yote inayozalishwa na kiwanda cha Mahonda.

Aidha, Serikali imeamua utaratibu huo uanze mwaka huu wa fedha 2018/19 kuanzia tarehe 1 julai 2018. Kwa waagiziaji watatakiwa kuinunua sukari ya mahonda iliopo hivi sasa ndani ya kipindi hiki cha mienzi miwili ili kukiwezesha Kiwanda kuendelea na mipango yake ya uzalishaji. Napenda ifahamike pia uwongozi wa kiwanda cha mahonda hautoruhusiwa kuuza sukari hiyo kwa watumiaji wa mwisho, hii itasaidia kutengeneza mfumo mzuri wa uendeshaji wa biashara ya sukari.

Serikali imeunda kamati ya kulisimamia jambo hili ndani ya Tume ya Ushindani halali ya Kumlinda Mtumiaji wakishirikiana pomoja na waigizaji wa sukari na uwongozi wa kiwanda cha mahonda.

Ndugu Waandishi wa Habari
Nakuombeni muifikishe taarifa hii kwa wananchi ili waifahamu vizuri na kuwaomba wananchi kutokuwa na wasiwasi wa kupanda kwa bei ya sukari, kwani kilichofanyika hivi sasa ni mfumo mzuri tu wa usimamizi na kutatua changamoto iliyojitokeza kwa biashara hii ya sukari.

Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.