Habari za Punde

Wanaondeleza makundi CCM wachukuliwe hatua - Wito

NA Takdir Ali,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi kichama Muhammed Rajab Soud amewataka wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kuacha muhali na badala yake kuwafichuwa wanaoendeleza makundi ili chama kiweze kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Akifunguwa kikao cha Halmashauri kuu ya Chama hicho Mkoa wa Magharibi kichama huko katika Hoteli ya ‘’Z’’ Ocean view Chuwini amesema uchaguzi umekwisha na tayari viongozi wamepatikana kilichobakia ni kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi sio kuendeleza makundi.
Amesema Uongozi umechoka kusikia mgawanyiko wa makundi na kupelekea kukwamisha maendeleo ya Wananchi licha ya hatua mbali mbali zinazochukuliwa na chama hicho.
“Nawomba wajumbe kama kuna watu wanataka Jimbo muda huu tupeni majina yao tuweze kumpa Jimbo sasa hivi tumechoka hali hiyo,”Alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Aidha amewataka wajumbe hao kutekeleza wajibu na kazi kwa ufanisi ili waweze kuwaletea maendeleo wananchi katika maeneo yao.
Amesema wananchi wanakabiliwa na matatizo mengi kama vile Ajira, Migogoro ya Ardhi, Miondombinu ya Maji,Hospitali na Skuli, Hivyo ni vyema kuchukuwa juhudi za kuwatatulia wananchi hao.
Pia Mwenyekiti huyo amewataka wananchi kushirikiana na viongozi wao wa Majimbo ili waweze kutatuliwa matatizo yanayowakabili ikiwemo tatizo la maji safi na salama linalowakumba katika maeneo yao.
Akiwasilisha mada katika kikao hicho Kaimu Katibu wa Chama Cha Mapinduzi katika Mkoa huo Mgeni Mussa Haji amesema hali ya kisiasa katika mkoa huo kwa kipindi cha miezi 6 ni nzuri na kuwaomba wajumbe hao kuendelea kuhamasisha suala la amani na utulivu hapa nchini.
Hata hivyo ameeleza kusikitishwa kwake na ujenzi na uhamiaji holela na uvamizi wa maeneo ya Ardhi jambo ambalo linaweza kuhatarisha ushindi wa Chama Cha Mapinduzi ifikapo mwaka 2020 na kuwataka viongozi wa Serikali  kuyasimamia masuala hayo.
Nae Sada Salum Mkuya Mjumbe wa halmasuri kuu ya mkoa huo amesema tatizo kubwa linalowaumiza Vichwa ni ukosefu wa maji safi na salama kwa baadhi ya wananchi wao na kueleza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya mfuko wa maendeleo wa mbunge na mwakilishi unatumika katika masuala ya maji.
Machano Othman Said ni mjumbe wa halmashauri ya mkoa huo amesema migogoro ya Ardhi inawakwamisha katika kuwaletea maendeleo wananchi wao katika majimbo na kuiomba halmashauri kuu ya mkoa huo kuisimamia Serikali kuhakikisha tatizo hili linapatiwa ufumbuzi hasa katika maeneo ya Bumbwisudi na Kama.
Kikao hicho cha halmashauri kuu mkoa wa Magharibi kichama kwa kauli moja imepitisha azimio la kughairisha kikao hicho hadi tarehe 2-8-2018 ili kuweza kukaa na Waziri anahusika masuala ya maji ili kuweza kupata maelezo ya kina juu ya kadhia hiyo.
Imetolewa na Idara ya Habar Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.