Habari za Punde

Waziri: Blogi zinaamsha ushindani kihabari


WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo (Kushoto), akimkabidhi kiongozi kuu wa blogi ya Zanzibar 24 Suleiman Juma Is-haka nyaraka zenye taarifa za kihistoria na mambo ya kale kwa ajili ya kuzitangaza ili kuvutia watalii zaidi hapa nchini. Uongozi wa Zanzibar 24 ulimtembelea Waziri huyo Juni 6, 2018 katika ratiba yake ya maadhimisho ya kutimiza miaka mitatu tangu kuasisiwa kwa blogi hiyo.  
Na Salum Vuai, WHUMK

KUNA umuhimu mkubwa wa kuisaidia mitandao ya kijamii zikiwemo televisheni za kimtandao (Online TV’s) inayochipukia hivi sasa, ili ziweze kutimiza wajibu wa kuwajuvya wananchi na dunia habari za matukio mbalimbali kwa haraka.

Akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa blogi ya Zanzibar 24 ofisini kwake Kikwajuni mjini Zanzibar, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, amesema mitandao ya kijamii ni tegemeo kubwa sasa kutokana na uwezo wa kuwafikia wananchi haraka hata katika simu zao za mkononi.

Uongozi wa Zanzibar 24 ulimtembelea Waziri huyo kwa lengo la kubadilishana mawazo na kupata ushauri chanya, ikiwa sehemu ya programu zake za kusherehekea miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa blogi hilo.

“Sasa watu hawana haja ya kusubiri saa mbili usiku kusikiliza taarifa za habari katika televisheni, kwani kukua kwa teknolojia kumerahisisha mawasiliano na kila kitu kimo kiganjani,” alieleza.

Alifahamisha kuwa, katika dunia ya sasa iliyojaa ushindani, haijuzu mwandishi wa habari kuchelewa kufika kwenye matukio kwa kisingizio cha kutokuwa na usafiri bali anapaswa kutumia maarifa na kuwa na moyo wa kujituma, vyenginevyo wenzake watamkimbia na kumuacha nyuma.

Waziri Kombo alisema, ni juu ya mamlaka,  taasisi za umma na binafsi pamoja na wafanyabiashara, kuitumia mitandao na blogi za kihabari katika kutangaza shughuli zao endapo zinataka kuifikia dunia kwa kasi na kutambulika kikamilifu.

Hata hivyo, aliushauri uongozi wa Zanzibar 24 kuhakikisha wanamaliza mchakato wa kujisajili rasmi wanaoendelea nao, ili kuhalalisha shughuli zake, ambazo amesema tayari zimekubalika licha ya changamoto kadhaa zinazohitaji kufanyiwa kazi.

“Mkifuata taratibu, mkawafuata wakongwe wa tasnia ya habari kwa ajili ya kupata miongozo mizuri, mna nafasi kubwa ya kupanda ngazi na kuwa mfano kama wamiliki wengine maarufu wa blogi Tanzania na duniani kwa jumla,” alieleza.

Aidha Waziri Kombo alisema Zanzibar ina mambo mengi yanayohitaji kuandikiwa na kutangazwa, kazi aliyosema inaweza kufanywa vizuri na blogi za kihabari na mitandao ya kijamii.

Alitoa mfano wa vivutio vya kihistoria vilivyotapakaa kila pembe ya visiwa vya Unguja na Pemba yakiwemo magofu ya kale, fukwe za kuvutia, historia za viongozi wa dini, siasa na kijamii pamoja na rasilimali za bahari, misitu na mapango.

Aliwaahidi viongozi hao kuwapa kila aina ya msaada ulio katika uwezo wake, kuhakikisha blogi yao inasimama kwa miguu yake katika kipindi kifupi kijacho ili iendelee kuwanufaisha wao na nchi yao Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Aliwashauri kuunda safu ya uongozi makini utakaokuwa na muundo unaokubalika na unaokidhi matakwa ya sheria ya uanzishaji wa vyombo vya habari na kampuni.    

Mapema, kiongozi mkuu wa Zanzibar 24 Suleiman Juma Is-haka, alisema blogi yao imepiga hatua kubwa katika kipindi hicho kifupi, kwa kuwa kila siku inatembelewa na  wasomaji wasiopungua 10,000.

Hata hivyo, alikiri kuwa bado wanahitaji nguvu za ziada kutoka katika mamlaka na kampuni za biashara ili azma yao ya kuwa taasisi rasmi na kubwa iweze kufanikiwa haraka iwezekanavyo.

Blogi ya Zanzibar 24 imetimiza miaka mitatu Julai 7, 2018, na miongoni mwa mambo waliyofanya katika maadhimisho hayo, ni pamoja na kukutana na Waziri wa Habari, na kutembelea nyumba za kurekebisha tabia kwa vijana wanaoacha dawa za kulevya (Sober Houses) iliyoko Mombasa kwa Mchina na kuwakabidhi misaada.

IMETOLEWA NA WIZARA YA HABARI, UTALII NA MAMBO 
YA KALE-ZANZIBAR
7 JULAI, 2018

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.