Habari za Punde

Ziara maalum ya kamati ya BLM kushughulikia migogoro na kero za wananchi Mkoa wa Kaskazini Unguja

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhio Zanzibar Nd. Ahmed Abdulrahman Radhid  akiionyesha ramani ya eneo la Uwekezaji liliopo Matemwe Kamati ya Baraza la Mapinduzi iliyoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Mwakilishi wa Jimbo la Kijini Mh. Juma Makungu Juma  akiionyesha Kamati ya Baraza la Mapinduzi eneo linalotumika  kwa shughuli za Mazishi katika Kijiji cha Matemwe ambao ukuta wa hifadhi umebomolewa kwa ajili ya shughuli nyengine.
Balozi Seif  akitoa nafasi kwa Wananchi wa Kijiji cha Matemwe Mbuyu Tende kutoa malalamiko yao juu ya mzozo wa ardhi ulioibuka katika eneo hilo hasa sehemu maalum ya Makaburi.
Waziri wa Fedha akitoa ufafanuzi katika kikao cha mwisho cha majumuisho na maamuzi hapo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja iliyopo Mkokotoni.
Waziri wa Ardhi, Nyumba, Mani na Nishati Mh. Salama Aboud Talib  akitoa ufafanuzi katika kikao cha mwisho cha majumuisho na maamuzi mwisho mwa ziara yao kukagua eneo la uwekezaji katika Kijiji cha Matemwe Mbuyu Tende.
Balozi Seif  akizungumza na wawakilishi wa Wanmanchi wa Matemwe Mbuyu Tende katika Mkutano wa majumuisho na maamuzi ya mgogoro uliojichomoza katika Kijiji hicho.
Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Mh. Vuai Mwinyi, Kushto ya Balozi Seif  ni Waziri wa Ardhi, Nyumba, Mani na Nishati Mh. Salama Aboud Talib na Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mh. Mahmoud Thabit Kombo.
Baadhi ya watendaji wa Taasisi zinazosimamia Uwekezaji Nchini na Wawakilishi wa Wananchi wa Kijiji cha Matemwe wakimsikiliza Balozi Seif hayupo pichani kuzungumzia uamuzi wa Serikali kuhusu  migogoro iliyopo katika Kijiji hicho.Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa maamuzi ya kuipatia eneo jengine la Uwekezaji Kampuni ya Sun Shine iliyokuwa ikiendesha Miradi yake katika Kijiji cha Matemwe Mbuyu Tende kufuatia Mradi wa Kampuni hiyo kutozingatia wala kufuata sheria na Taratibu za Uwekezaji Nchini.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia ikatoa maamuzi mengine ya kulitaka eneo la Makaburi la Kijiji hicho cha Matemwe Mbuyu Tenda liendelee kubakia kwa shughuli za Kuzikia kama zamani kufuatia Kampuni ya Uwekezaji wa Sekta ya Utalii ya Pololokutaka kulitumia kwa shughuli nyengine.
Uamuzi huo umekuja kufuatia Ziara Maalum ya Kamati ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar iliyoundwa na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein ikiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ya kulikagua eneo lenye mgogoro na kusikiliza kero za Wananchi wa Matemwe kuhusiana na kadhia hiyo.
Akizungumza katika Kikao cha majumuisho ya ziara hiyo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja iliyopo Mkokotoni Balozi Seif  alisema kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ya Utalii pamoja  na kuwapa moyo Wawekezaji Serikali Kuu inafikiria kuilipa fidia Kampuni ya Kampuni ya Sune Shine kutokana na majengo yake katika eneo hilo.
“ Serikali iko tayari kumpa eneo jengine Sun Shine kwa kuzingatia utaratibu wa upatikanaji wa Vibali na nyaraka za uwekezaji”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema kwamba migogoro yote  inayohusiana na masuala ya Ardhi iliyoibuka Zanzibar  kwa utafiti wa awali inathibitisha kukiukwa kwa Sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali katika matumizi ya Ardhi.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali isingependa kuona inajichomoza migogoro ya ardhi katika Sekta ya Uwekezaji kati ya Wananchi, Wawekezaji pamoja na Serikali yenyewe kwa ujumla.
Aliupongeza na kuushukuru Uongozi mzima wa Kampuni ya Sun Shine kwa kushirikiana vyema na Wananchi wa Kijiji cha Matemwe Mbuyu Tende kwa kusaidia Uchumi, Ustawi naMaendeleo ya Wananchi hao.
Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Kampuni hiyo kwamba ushirikiano uliyoonyesha kwa Wananchi hao ni vyema wakauendeleza katika eneo jengine watakalopewa hapo baadae na Serikali Kuu kwa ajili ya kuendeleza miradi yao waliyojipangia.
Akigusia eneo la Makaburi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi hao wa Matemwe kwamba Serikali Kuu itatafuta njia muwafaka itakayosaidia kulihifadhi eneo hilo la Makaburi lenye ukubwa wa Hekta 2.9 ili liendelee kutumiwa kwa shughuli za Mazishi pekee.
Akitoa ufafanuzi katika Mkutano huo wa Maamuzi Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed alisema nia ya kukaribishwa kwa Wawekezaji Nchini ni kuungana pamoja na Serikali katika kuchangia mapato ya Serikali.
Dr. Khalid alisema hata hivyo bado Wawekezaji wanawajibika kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za Uwekezaji mfumo utakaowasaidia katika uwekezaji salama kwa kuepuka  kushawishiwa na matapeli ambao hatimae  husababisha ugomvi  kati ya Wawekezaji na Wananchi wa maeneo husika.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mh. Mahmoud Thabit Kombo alisema Sekta ya Utalii imesaidia kumvua Mwananchi katika dimbwi la maisha duni hasa katika maeneo yanayoendelezwa Uwekezaji wa Sekta hiyo.
Hata hivyo Waziri Mahmoud alisema Jamii isifikie pahali ikajikuta inasahau kuendeleza Utamaduni, Mila, Silka na desturi zake kwa hisia na Mvuto wa  uwepo wa Sekta ya Utalii hapa Nchini.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Mh. Salama Aboud Talib alitahadharisha kwamba tabia ya baadhi ya Watu kuwapitisha njia ya Mkato Wawekezaji ndio chimbuko la migogoro inayoibuka mara baada ya kuanza kwa mradi.
Mh. Salama alisema wakati umefika kwa Wataalamu wa Sekta zinazohusika na masuala ya Uwekezaji kuanza kutoa Taaluma  kwa Umma ili pale anapotokea Muwekezaji taratibu husika zianzne kufuatwa katika hatua za awali.
Waziri wa Ardhi katika Mkutano huo alitahadharisha wazi kwamba kuanzia sasa   hakuna ruhusa kwa Taasisi yoyote kutia saini Mikataba inayohusiana na Uwekezaji katika Masuala ya Ardhi bila ya idhini ya Wizara inayohusika na jukumu hilo.
Kamati hiyo ya Baraza la Mapinduzi iliyoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ilipata fursa ya kukagua maeneo yaliyopo majengo ya Kampuni ya Sun Shine pamoja na lile la Makaburi ambalo kwa sasa tayari limeshazunguushwa uzio.
Wakitoa malalamiko yao Wananchi wa Matemwe Mbuyu Tende walisema hawakatai uwepo wa Utalii katika Maeneo yao lakini kinachojichomoza kuleta migogoro kati yao ni baadhi ya Watu kuwa na tabia ya kuendekeza Ubinafsi.
Wananchi hao walisema mgogoro wa Kijiji hicho kati ya Wananchi na Wawekezaji umeibuka tokea Mwaka 2009  kitendo kilichofikia maamuzi ya kuandika Barua ya kukataa eneo lao la Makaburi kutumiwa kwa shughuli nyengine.
Mzee Ali Haji Ali {Mchule} akiongoza Wananchi hao katika kulalamikia kadhia hiyo alisema Wazee wa Kijiji hicho walikataa kabisa fedha zilizowataka kuridhia kutoa eneo hilo lakini badala yake baadhi ya Vijana wa Kijiji hicho wakaamua kuwaendea kinyume kwa kuridhia kutia saidi mkataba wa kulitoa eneo hilo.
Mapema Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar Nd. Ahmed Abdulrahman Rashid aliieleza Kamati hiyo ya Baraza la Mapinduzi kwamba Matemwe ni eneo kubwa kuliko yote kwa maeneo ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar.
 Nd. Ahmed alisema zipo baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika uanzishwaji wa Miradi ya uwekezaji wa vitega uchumi kwenye eneo hilo ikiwemo baadhi ya majengo kujengwa ndani ya maeneo ya Bara bara pamoja na Fukwe za Bahari jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria na Mikataba.
Katibu Mtendaji huyo wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar alifahamisha kwamba Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1992 imeweka wazi kwamba eneo la Fukwe lenye urefu wa Mita 30 usawa wa yanapofikia maji ya Bahari haliruhusiwi kujengwa  jengo lolote ndani ya Mikataba ya Uwekezaji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahi kufanya ziara mnamo Tarehe 8 Febuari 2018 katika eneo hilo  na kusisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Wananchi katika Miradi ya Kiuchumi kwenye maeneo yao ambapo alisema ndio njia pekee inayoleta utulivu wa kudumu katika kuendesha miradi ya Uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.