Habari za Punde

Bomoa Bomoa Tunguu yaondoka na nyumba 16

Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja imezibomoa nyumba kumi na sita katika eneo la Tunguu ambazo zimejengwa kinyume na utaratibu katika eneo lililotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo za miradi ya serikali ikiwemo upanuzi wa majengo ya chuo kikuu cha Taifa Suza.

Akishuhudia tukio la kuvujwa kwa nyumba hizo Mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja mhe Hassan Khatib Hassan amesema serikali mkoani humo imeamua kuchukua hatua hiyo ya kuzivunja nyumba hizo kutokana na wananchi wa eneo hilo kushindwa kutii agizo  lililotolewa miezi mitatu nyuma la kuvunja na kuhama katika maeneo hayo ili kupisha serikali kuendelea na zoezi la usafishaji wa eneo hilo kwa ajili ya matumizi yaliokusudiwa.

Nao baadhi ya wananchi ambao wamebomolewa nyumba zao wanaoishi karibu na maeneo hayo wamelalamikia hatua iliyochukuliwa na serikali ya kubomoa nyumba hizo walizokua wakiishi kwa muda wa takriban miaka 45.

Wamesema hatua iliyochukuliwa na serikali ya kubomolewa nyumba hizo imewapa wakati mgumu kwa sasa kwani hawana sehemu nyengine ya kwenda kuishi na watoto wao na hawana uwezo wa kumudu gharama ya ujenzi wa makaazi mapya kutokana na hali zao za umasikini hivyo wameiomba serikali kuu kuangalia uwezakano wa kuwapatia fidia ili waweze angalau kutafuta sehemu nyengine ya kujihifadhi na watoto wao.

Nae Kaimu Makamo Mkuu wa chuo cha Suza dkt Haji Mwevura haji amesema ni vyema kwa wananchi kuhakikisha kwamba wanafuata taratibu za uhaulishaji wa ardhi kabla ya kununua maeneo ili kuepukana na matatizo yanayoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.