
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Jakarta,
Indonesia 03.08.2018

RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Zanzibar
ina mengi ya kujifunza kutoka Indonesia katika sekta ya uvuvi kutokana na nchi
hiyo kupiga hatua na kupata mafanikio makubwa katika sekta ya uvuvi.
Dk.
Shein aliyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha kusarifu samaki cha Perum
Perikanan kiliopo nje kidogo ya mji wa Jakarta nchini Indonesia ambacho kipo
chini ya mamlaka ya Serikali ya nchi hiyo.
Katika
hotuba yake fupi aliyoitoa mara baada ya kufika kiwandani hapo kabla ya
kutembelea katika vitengo mbali mbali vya kiwanda hicho, Rais Dk. Shein alipongeza
mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta yauvuvi mchini Indonesia.
Alieleza
kuwa kiwanda hicho kinaonesha jinsi ya Indonesia ilivyoweka mikakati madhubuti
katika kuhakikisha sekta ya uvuvi inaimarika na kuweza kuuimarisha uchumi wa nchi
hiyo pamoja na kuwanufaisha wananchi wake ambapo imekuwa chanzo kikubwa cha ajira
hasa kwa vijana.
Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kueleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uvuvi ambapo tayari
imeshaanzisha Kampuni ya Uvuvi ya (ZAFICO) kwa azma ya kuinua sekta hiyo.
Aliongeza
kuwa hatua zinazoendelea hivi sasa
katika kuimarisha sekta hiyo ni pamoja na ununuzi wa vifaa na boti kwa
ajili ya kuvulia pamoja na ujenzi wa bandari na hatimae kuwa na viwanda vidogo
vidogo vya samaki huku akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nchi
hiyo kuja Zanzibar kuwekeza katika viwanda vya samaki.
Pamoja
na hayo, Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa uongozi wa kiwanda hicho kwa
kumualika kwenda kuona mafanikio waliyoyapata na kusisitiza haja ya kuwepo
ushirikiano kwa lengo la kubadilishana uzoefu na utaalamu katika sekta ya
uvuvi.
“Nakushukuruni
kwa kunikaribisha vizuri kuja kuona maendeleo mliyoyafikia katika sekta hii ya
uvuvi…tumejivunza mengi hasa ikizingatiwa kuwa ikiwanda hichi ni cha serikali”alisema
Dk. Shein.
Katika
ziara hiyo kiwandani hapo, Rais Dk. Shein alitembelea sehemu zinazosarifu aina
mbali mbali za samaki ambao baadae husafirishwa
nje ya nchi na kueleza kuwa wanunuzi wakubwa wa samaki hao ni Marekani,
Japan pamoja na nchi za Mashariki ya Kati.
Aidha,
Rais Dk. Shein alipata kuona jinsi ya usarifishwaji wa samaki unavyofanywa
kiwandani hapo na kuweza kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa kiwanda hicho hatua
ambayo pia, imeonesha jinsi vijana walio wengi ambao wameweza kupata ajira.
Nao
uongozi wa kiwanda hicho ulieleza jinsi ulivyofarajika na ziara ya Dk. Shein
katika kiwanda chao hicho ambacho ni kiwanda kikubwa cha samaki nchini humo
ambapo uongozi huo ulieleza umuhimu wa kuwepo kwa mashirikiano katika sekta
hiyo kati ya Indonesia na Zanzibar hasa ikizingatiwa kufanana kijiografia kwa
pande mbili hizo.
Uiongozi
huo ulitumia fursa hiyo kueleza mafanikio makubwa yaliopatikana kwa muda mrefu tokea kuanzishwa kwa kiwanda
hicho ikiwa ni pamoja na mafanikio waliyoyapata tokea kuanzishwa kwa ufugaji wa
samaki.
Pia,
uongozi huo ulizitaja aina za samaki wanaosariwa kiwandani hapo wakiwemo samaki
wa jodari, kamba na wengineo pamoja na namna wanavyosafirishwa kwenda nje ya
nchi.
Pia,
uongozi huo ulieleza namna ulivyoweka mikakati katika kuhakikisha wananchi
wanapata fursa kutoka katika sekta hiyo ya uvuvi kwa kutoruhusu wageni kuvua
katika bahari ya nchi hiyo na kueleza namna ulivyoweka utaratibu wa kuwasaidia
wavuvi wa nchi hiyo.
Wakati
huo huo, Rais Dk. Shein akiwa na Mama Mwanamwema Shein na ujumbe wake alitembelea
Hospitali ya Harapan Kita ambayo ni hospitali kubwa nchini humo inayotibu maradhi
ya moyo na kupata fursa ya kuona vitengo mbali mbali vya vya hospitali hiyo.
Katika
hotuba yake fupi hospitalini hapo, Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa uongozi
wa hospitali hiyo kwa kumpa fursa ya kutembelea na kujionea namna ya huduma za
matibabu ya moyo yanavyofanywa kwa kutumia utaalamu wa kisasa wa matibabu ya
moyo kwa muda mfupi tena bila ya kufanyiwa upasuaji.
Rais
Dk. Shein alisema kuwa ziara yake hiyo hospitalini hapo itasaidia kujifunza
mambo mengi muhimu ambayo yatasaidia juhudi za serikali katika kukuza na
kuendeleza sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali mpya ya kisasa
ambayo pia itatoa mafunzo juu ya huduma za
sekta hiyoya afya.
Alieleza
kwamba hivi sasa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Tano
imechukua juhudi kubwa katika kuhakikisha huduma za afya pamoja na miundombinu
yake inaimarika.
Aliongeza
kuwa Serikali imeendelea na juhudi zake katika kupambana na maradhi yasiyo ya
kuambukiza ambayo yamekuwa yakiisumbua sana jamii.
Lakini
hata hivyo, Dk. Shein alieleza kuwa bado Zanzibar inahitaji kujifunza kutoka
hospitali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa kitengo cha maradhi ya moyo katika
hoapitali ya MnaziMmoja hakijawa na wataalamu wengi pamoja na vifaa vya kutosha
kama ilivyo hospitali hiyo.
Dk.
Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha
ushirikiano na hospitali hiyo hasa katika kubadilishana wataalamu, utoaji wa
mafunzo na utafiti.
Nao
uongozi wa Hospitali hiyo ulieleza azma yake ya kushirikiana na Zanzibar katika
kupambana na maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja na kuutumia uzoefu walionao katika
kutibu na kutoa huduma kwa maradhi hayo.
Sambamba
na hayo, uongozi wa hospitali hiyo ulieleza kufurahishwa kwao na ziara hiyo ya
Rais Dk. Shein ambaye na yeye pia ni bingwa katika fani hiyo na udaktari na kuahidi
kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.
Mapema
Rais Dk. Shein alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya Exim ya Indonesia
katika ukumbi wa Hoteli ya Borobudur mjini Jakarta, ambapo uongozi huo ulieleza
azma yake ya kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya
maendeleo kama ilivyofanya kwa nchi kadhaa za Afrika ikiwemo Ethiopia, Nigeria,
Algeria na nyenginezo.
Nae
Dk. Shein kwa upande wake aliipongeza azma ya Benki hiyo kubwa nchini humo na
kueleza jinsi alivyofarajika kwa uwamuzi huo na kutumia fursa hiyo kuukarisha
Zanzibar ili uje kuangalia fursa zilizopo pamoja na kushirikiana na serikali
kwa kuipatia mikopo yenye masharti nafuu ili kuendeleza miradi iliyopo na
inayojipangia kutekelezwa.
Akiendelea
na ziara yake nchini Indonesia, Rais Dk. Shein na ujumbe wake wameelekea kisiwa
cha Bali ambapo akiwa huko atapata fursa ya kukutana viongozi wakuu wa Bali
pamoja na kutembelea maeneo kadhaa aliyopangiwa na wenyeji wake katika kisiwa
hicho cha Bali ambacho ni maarufu kwa utalii duniani.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment