Habari za Punde

Hotuba Ya Balozi Seif Ali Iddi Aliyoitoa Kwenye Ufunguzi Wa Kongamano La Maadili Ya Mtanzania, Wilaya Ya Mjini Unguja - Tarehe 05 Agosti, 2018

Wazazi Wenzangu, Mabibi na Mabwana.

Assalamu Alaykum,

Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema tukaweza kuhudhuria kwenye kongamano hili juu ya maadili ya Mtanzania.

Naushukuru sana uongozi wa Jumuiya ya Wazazi, Wilaya ya Mjini kwa uamuzi wenu wa kufanya kongamano hili muhimu kwa uhai wa Taifa letu kwani Taifa lisilokuwa na maadili ni sawa na mwili wa binaadamu usiokuwa na roho. Nawashukuru pia kwa kunialika kuwa Mgeni rasmi wa shughuli yetu ya leo.

Kongamano hili linafanyika katika kipindi ambacho Wazazi tuliokuwa wengi hatuna amani kwa mambo tunayoyashuhudia yanafanyika katika jamii yetu.  Ukisikiliza radio habari za wizi wa kutumia nguvu, utumiaji wa madawa ya kulevya, ubakaji, kulawiti, kunyanyasa watoto na akina mama ni mambo ambayo tunayasikia kila mara.  

Halikadhalika, ukisoma magazeti au ukiangalia televisheni habari ndio hizo hizo. Matukio haya ni baadhi tu ya mambo yanayotendeka katika jamii yetu yanayoonyesha wazi hali si shuwari tena kwa upande wa maadili yetu. Taratibu maadili yetu yanaondoka na pahala pake panachukuliwa na matendo maovu. Kwa hivyo, kongamano hili limekuja wakati muwafaka.

Ndugu Wanakongamano,

Hali hii ya mmon’gonyoko wa maadili inayoendelea hivi sasa katika jamii yetu yatupasa tujiangalie wapi tumekosea ili tujirekebishe na maeneo gani tunafanya vizuri ili tuyaimarishe zaidi. Naomba basi nieleze japo kwa muhtasari mambo yanayochangia kumon’gonyoka kwa maadili nchini.

Taifa linatokana na mkusanyiko wa familia. Familia imara siku zote hujenga Taifa imara.  Kinyume chake familia dhaifu hujenga Taifa dhaifu. Kwa hivyo basi, mkusanyiko wa familia nyingi zenye maadili mema hujenga Taifa lenye maadili mema yanayokubalika Kitaifa.

Kwa bahati mbaya siku za hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia mtikisiko mkubwa wa maadili katika ngazi ya familia unaosababishwa na uvunjikaji wa ndoa. Taarifa za hivi karibuni kutoka Mahakama ya Kadhi ya Wilaya ya Mwanakwerekwe, zinasema kipindi cha miaka mitatu kuazia Januari, 2016 hadi Julai, 2018 jumla ya kesi za talaka 1,819 zilipokelewa. 

Kwa hivyo, inaonyesha wazi talaka Visiwani zinatolewa kama njugu, na hichi ni kielelezo cha kushuka kwa maadili katika jamii zetu. Katika mazingira kama haya akinan mama wengi hushindwa kuwalea vizuri watoto walioachiwa na hatimaye watoto hao huishia kupata malezi ya mitaani. Ndio maana wazee wetu wamesema: “mkono mmoja haulei mwana”.

Ndugu Wanakongamano, Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameiwezesha dunia kuwa kama kijiji kutokana na mtandao. Simu zimechukuwa nafasi za wazee. Mitandao hii inawawezesha vijana wetu kuangalia mambo mengi ikiwemo vitendo vinavyokwenda kinyume na silka, mila na utamaduni wetu ambao ni kinyume maadili ya Mtanzania.  Ni vyema katika mjadala wetu wa siku hii ya leo tuyazungumze na kuyatafutia ufumbuzi.

Mabibi na Mabwana, ni ukweli usiopingika kuwa ukosefu wa malezi mazuri nao unapelekea kwa kiasi kikubwa uporomokaji wa maadili nchini. Watoto wetu huishia vijiweni na kulelewa na wanavijiwe ambao mara nyingi sio watu wema. Hatimaye watoto wao huanza kujitumbukiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, pamoja na matendo maovu yasiyo na tija katika jamii yetu.

Ndugu Wanakongamano, tunaweza kuondoa au kupunguza uporomokaji wa maadili katika jamii yetu kama tutaelimishana vizuri na kufuatana maadili yetu yaliyotokana na wazazi wetu pamoja na viongozi wa dini zetu. Serikali kwa upande wake imetowa fursa kwa vijana wetu kujiunga na Jeshi la Uchumi (JKU) pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kujenga misingi imara ya maadili ya Taifa letu kwa vijana wetu. Ni vyema basi sisi kama wazee na wanasiasa tuwahamasishe vijana wetu kujiunga na vikosi vyetu hivi ili Taifa letu liwe na maadili bora ya baadae.

Ndugu Wanakongamano,
Mada ya maadili ya Mtanzania ni pana. Nawaomba sana mijadala yenu isiishie tu kwenye ukumbi huu. Ni vyema baada ya majadiliano yenu mkajipanga vizuri kutekeleza yale mliyokubaliana. Jumuiya ya wazazi ina nafasi kubwa nchini kuchangia malezi bora ya vijana wetu ili tuwe na Taifa lenye maadili mema.

Mwisho kabisa, nawaomba muitumie nafasi hii pia ikiwezekana kupendekeza sera ambayo kwa mitizamo yenu itasaidia kujenga familia bora nchini (family-friendly policy) kwani ni ukweli usiopingika kuwa maadili siku zote yanaanzia nyumbani. Tutakapokuwa na familia imara nchini tutakuwa na maadili imara pia. 

 Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa Kongamano hili la Maadili ya Mtanzania limefunguliwa rasmi.

 Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.