Na Ali Shaaban Juma
Kwawa wa Arctic ni ndege wa
pwani wa jamii ya kwawa ambao kwa kiingereza huitwa Arctic Tern. Jina la
kisayansi la ndege huyo ni Sterna paradisaea. Ndege hao hupatikana kwa wingi katika bahari Arctic
katika pembe ya kaskazini mwa dunia kwenye baridi kali. Bahari hiyo ya Arctic
ndiko linakopatikana jimbo la Alaska
huko Marekani, Canada, Greenland(Denmark), Iceland, Norway, Urusi na Sweden.
Kwawa
hao ni tofauti na kwawa wanaopatikana katika pwani ya Afrika Mshariki ikiwemo
visiwa vya Zanzibar. Kwawa wa Arctic ni ndege wenye ukubwa wa wastani wenye
uzito wa Gramu mia moja na urefu wa Inchi 11-15 ambapo mbawa zao zina upana wa inchi 28 hadi 30.
Ndege hawa huishi kwa kula samaki wadogo na vijidudu vya baharini. Wastani wa maisha ya ndege hao ni kati ya
miaka kumi na tano hadi thelathini na nne ambapo wataalamu wa sayansi za maisha
ya ndege wanakisia kuwa kuna zaidi ya Kwawa wa Arctic milioni moja.
Kwawa
wa Arctic ambao huishi jike na dume
huanza kutaga akiwa na miaka minne na hurejea kutaga katika kiota chao kila
mwaka. Wataalamu wa sayansi za ndege wa pwani
“Marine Ornithologists” wanasema kuwa uhusiano kati ya Kwawa jike na
dume huanza kwa kwawa jike kumfukuza dume juu sana angani na baada ya hapo
kwawa dume hubaka samaki na kumpa kwawa jike. Baada ya hapo kwawa jike na dume
huruka na kuzunguka angani pamoja. Kisha
ndege hao hutafuta kiota na baada ya kukubaliana kuhusu kiota hicho,
dume huwa ndio mlinzi wa kiota hicho. Kwa kawaida Kwawa wa Arctic hutaga kati
ya yai moja hadi matatu, lakini mara nyingi hutaga mayai mawili. Jike na dume
hulalia pamoja kwa zamu ambapo hutotoa baada ya siku 27 na kinda huruka siku 24
baada ya kutotolewa. Kutokana na mzunguuko mdogo wa kizazi chao, Kwawa wa
Arctic ni miongoni mwa ndege wachache duniani ambao hutumia muda wao mwingi
kulea watoto kidogo.
Kwawa
wa Arctic ni maarufu mingoni mwa wanasayansi na wanamazingira duniani kutokana
na kuwa ndio ndege pekee wanaosafiri masafa marefu kila mwaka kutoka huko
Greeland eneo la Arctic kaskazini ya dunia wanakotaga hadi eneo Weddell la bahari Antarctic kusini
ya dunia.
Huko
Greenland ndege hao hutaga katika maeneo mengi ya visiwa vidogo vidogo vilvyo
katika pwani ya nchi hiyo. Maeneo makuu ambayo ndege hao huishi na kutaga kwa
wingi ni Disko Bay, Sand Island,
Upernavik na Kitsissunnguit. Kwawa
wengi hupatikana katika kisiwa cha Kitsissunnguit
ambapo zaidi ya kwawa laki moja wanaishi na kutaga katika kisiwa hicho.
Kwa
kawaida majira ya baridi na theluji kali upande wa kaskazini ya dunia
wanakoishi kwa hao huanza mwezi wa Disemba na kumalizika Machi na majira ya
kiangazi katika eneo hilo ni kati ya Juni hadi Septemba. Tofauti na maeneo mengine ya dunia, eneo la
Arctic wanakoishi kwawa hao ni lenye theluji nyingi ambapo wakati wa kiangazi
baadhi ya siku jua halitui na kinyume chake wakati wa baridi kali baadhi ya
siku jua halitoki.
Kutokana
na mzunguko huo wa hali ya hewa, ndege hao huhama katika makaazi yao ya kawaida
kaskazini ya dunia pale baridi inaponza kuanzia mwezi wa Novemba na kuhamia
katika aneo la bahari ya Antarctic kusini ya dunia ambapo mara nyingi
ndege hao hufikia katika kisiwa cha Farne
kilichoko huko Northumberland
katika pwani ya Uingereza. Hurejea katika makaazi yao ya kudumu kaskazini ya
dunia kuanzia mwezi wa Machi. Kutokana na mzunguko huo wa safari ndefu, ndege
hao hutumia sehemu kubwa ya mwaka katika safari hiyo.
Kwa
vile ndege hao kusafiri masafa marefu
kuliko ndege wowote duniani, kwa miaka kadhaa wanasayansi na watafiti kutoka
mashirika ya mazingira, Vyuo Vikuu na taasisi nyenginezo wamekuwa wakifuatilia
safari za ndege hao ili kujua ukweli wa safari za ndege hao. Katika majira ya
kiangazi ya Oktoba mwaka 1982, Kwawa mmoja aliyekamatwa katika kisiwa cha Farme
huko Uingereza alifungwa kipande kidogo chenye alama mguuni na baada ya miezi
mitatu katika mwezi wa Disemba ndege huyo aifika pwani ya Melbourne nchini
Australia. Hiyo ni safari ya kilomita 22 Elfu ya kuvuka bahari.
Utafiti
mwengine ulofanywa na Carsten Egevang kutoka kituo cha utafiti cha Greenland
kiitwacho “Greenland Institute of Natural
Resources”, umeonesha kuwa wakati
wa kurudi kaskazini ya dunia, ndege hao
hufaidika na mwendo wa upepo ambao huvuma mwelekeo wa safari yao na hivyo kutumia nguvu kidogo katika safari
yao. Katika utafiti huo ndege hao waliruka kutoka Greenland tarehe 1 Septemba
2006 na walipofika pwani ya visiwa vya Cape Verde katika bahari kuu ya
Atlantiki ndege hao walijigawa makundi mawili.
Kundi moja
lilikwenda hadi pwani ya Afrika Kusini na kupumzika katika eneo hilo tarehe 1
Novemba,2006 ikiwa ni miezi miwili tokea kuondoka huko Greenland. Kundi la pili
lilivuka bahari kuu ya Atlantiki na kutua katika mwambao wa Amerika ya Kusini
hapo tarehe 1 Novemba,2006 ikiwa ni miezi miwili baada ya kuondoka huko
Greenland. Baadae makundi yote hayo
mawili yalielekea katika eneo la Weddell
katika bahari Antarctic kusini ya dunia na kubaki hapo hadi kwa miezi mine.
Ramani ya setelaiti ilionesha kuwa ndege hao walianza safari ya kurejea
kaskazini ya dunia tarehe 1 Aprili.2007 na baada ya mwezi mmoja walipumzika
katikati ya bahari kuu ya Atlantiki hapo tarehe 1 Mei 2007. Kutokana na urefu
wa safari hiyo, ndege hao walifika Alaska baada ya miezi mitano na uwasili huko
Greenland mwezi Novemba 2007.
Utafiti mwengine ulofanywa na Wanasayansi wa taasisi
ya “British
Antarctic Survey” kwa kuwafunga miguuni ndege hao kifaa kidogo cha
Kieletroniki cha “Geolocator”, imebainika kuwa ndege hao husafiri masafa ya
maili 44 Elfu (Kilomita 71,000) kila mwaka kutoka kaskazini ya pembe ya dunia
hadi kusini ya pembe ya dunia. Safari hiyo huanzia huko Greenland kaskazini ya
dunia katika makaazi ya ndege hao na kuishia katika fukwe za pwani ya Weddlle
kusini ya dunia wakati wa kiangazi. Kwa vile ndege hao huishi wastani wa miaka
34, safari hiyo ya kwenda kusini ya dunia na kurejea kaskazini ya dunia kila
mwaka ni sawa na safari ya umbali wa Maili Milioni 1.25 kwa kipindi hicho cha miaka 34
safari ambayo ni sawa na safari tatu za
kwenda mwezini!
Kutokana
na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hapo mwaka 2013 wanasayansi nchini Uholanzi waliwafunga miguuni Kwawa
kumi na mbili vifaa vidogo vya Kieletroniki vijulikanavyo kitaalamu kama “Geolocator tags” kifaa hicho chenye
uzito wa gramu 1.5 ambao ni sawa na asilimia 3% ya uzito wa ndege huyo
kiliwawezesha ndege hao kuruka kama kawaida. Kazi ya kifaa hicho kidogo cha
kieletroniki chenye betri inayofanya kazi mwaka mzima amabcho kilikuwa bora
zaidi kuliko vile vilivyotumiwa mwanzo ni kurikodi nyendo za ndege hao. Vifaa hivyo
viliunganisha mawasiliano kati ya Kwawa hao na Setelaiti angani ambapo
setelaiti hiyo nayo kwa kupitia kompyuta ilipeleka taarifa ya ramani ya njia
walimopita ndege hao katika kituo cha watafiti na hivyo moja kwa moja watafiti
hao kufanikiwa kufuatilia safari yote ya ndege hao bila kupoteza hata sekunde moja ya mawasiliano. Utafiti huo ulionesha
kuwa ndege hao walisafiri masafa marefu zaidi kuliko ilivyokadiriwa na tafiti
zilizofanywa hapo awali na wanasayansi wengine.
Ramani
iliyotumwa na setelaiti ilionesha kuwa Kwawa hao walisafiri umbali wa Kilomita
90,000 (Maili 56 Elfu). Ramani hiyo ilionesha
kuwa katika safari yao ya kuelekea kusini ya dunia, ndege hao walipita katika
mwambao wa bahari kuu ya Atlankiti pembeni ya bara Ulaya na Afrika Magharibi.
Baada ya kupinda katika pembe ya bahari ya Afrika ya Kusini, Kwawa hao
waliingia katika bahari kuu ya Hindi (Indiani Ocean) ambapo baadhi ya ndege hao
walielekea upande wa Australia na kisha kugeuza na kuelekea upande wa kusini
mwa bahari kuu ya Hindi na kutua katika
kisiwa cha Wilkesland kaskazini mashariki mwa bahari ya Antarctic.
Ramani
hiyo ilimuonesha ndege mmoja ambaye alisafiri kilomita mia kadhaa kusini mwa
mwambao wa Australia na kisha kuelekea
upande wa kusini katika bahari ya Antarctic, ambapo ndege mwengine alisafiri
kupitia eneo lote la mwambao wa pwani ya Australia kati ya bara hilo na kisiwa
cha Tasmania hadi pwani ya mjini Melbourne nchini Australi. Baada ya kuruka kutoka pwani ya Melbourne,
Kwawa huyo alielekea upande wa kusini katika bahari ya kisiwa cha Wilkesland
kaskazini mashariki ya bahari ya Antartic kupitia kisiwa kidogo kiitwacho
“South island” kulichoko kusini magharibi mwa New Zealand hadi nchini
Uholanzi nchi ambayo ndege huyo
aliondokea. Taarifa za setelaiti zilionesha kuwa safari ya ndege huyo ilikuwa
ni Kilomita 91,000 (Maili 57 Elfu) ambayo ndiyo safari ndefu kabisa ya kiumbe
kurikodiwa. Kumbukumbu zilionesha kuwa safari ya ndege hao kuelekea kusini ya
dunia ilichukua siku tisiini na tatu ambapo ndege hao walisafiri kwa kasi ya
kilomita 330 kwa siku. Hata hivyo kutokana na kusukumwa na upepo, safari ya
kurejea kaskazini ya dunia ilikuwa ni nyepesi kwani ndege hao walitumia siku
Arobaini na kusafiri kwa kasi ya Kilomita 670 kwa siku. Ndege hao hutua kwa
zaidi ya mwezi mmoja katikati ya eneo la kaskazini mwa bahari ya Atlantiki
kwenye samaki wengi ili kupumzika na kula.
Kwawa wa Arctic aliyefungwa mguuni kifaa kiitwacho
geo- locator akirejea katika maskani yake ya kutaga katika kisiwa kidogo kiitwacho Sand Island huko kaskazini mashariki
ya Greenland hapo mwaka 2007 baada ya kumaliza safari ya mzunguuko wa Kilomita
70,000 iliyoanzia kisiwani hapo mwezi Novemba, 2006.
Mwandishi wa makala haya ni Mwalimu wa
Chuo cha Uandishi wa Habari cha ZJMMC, Kilimani mjini Zanzibar.
E-Mail: Rafikifumba1@hotmail.com
No comments:
Post a Comment