Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Azungumza na Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Leo.

 Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dr. Bashiru Ali Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
 Dr. Bashiru akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.
Kulia ya Dr. Bashiru ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dr. Juma Abdulah Saadala.
Balozi Seif akiagana na Dr. Bashiru baada ya mazungumzo yao huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud akiwa nyuma ya Dr. Bashiru, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mihayo Juma N’hunga  na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulah Saadala.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi {CCM} Dr. Bashiru Ali alionya kwamba CCM imejipanga na kuanza kuchukuwa hatua za kukabiliana na Makundi yoyote yenye tabia na nia ya kudhoofisha Taasisi hiyo kongwe ya Kisiasa  Nchini Tanzania.
Alisema Chama hicho kimeumizwa sana  na tabia hiyo mbovu isiyokubalika aliyoifananisha sawa na ugonjwa wa Kansa ambayo huchangia pia kuwachafua Viongozi na Wanachama wake.
Akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ofisini Vuga Mjini Zanzibar Dr. Bashiru Ali alisema kinachohitajika wakati huu ni kuimarishwa kwa Chama hicho chenye uwezo wa kuendelea kulinda na kusimamia Uhuru pamoja na Ukombozi wa Taifa hili.
Dr. Bashiru alieleza kwamba katika muelekeo wa uendelezaji wa CCM imara iliyoanza kurejesha imani kwa Wananchi walio wengi suala la makundi limefikia kikomo cha kuepukwa kabisa  kwa vile liko sawa na najisi kwa watu wenye Imani za Kidini.
Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba CCM kamwe haitokubali kushindwa na makundi ya Watu wasiokuwa na muelekeo wa ulinzi wa Ukombozi.
“ Katika utumishi wangu wa  Chama  katika nafasi ya utendaji Mkuu sitokubali kuchafuka wala kuchafuliwa, wala kuwachafua Viongozi wetu Wakuu walioniamini kunipa utumishi huu muhimu katika Chama chetu”. Alisisitiza Dr. Bashiru.
Aliwataka Viongozi waliopewa fursa za kuwatumikia Wananchi moja kwa moja hasa Majimboni kuacha tabia ya kupayuka payuka ovyo kwa vile kinachowapa nguvu ni Heshima ya chama wala si ubinafsi unaoweza kuwavuruga Wananchi wao.
Akigusia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyopata ridhaa ya Wananchi ya kuongoza Dola Bara na Zanzibar  Katibu  Mkuu wa CCM  Dr. Bashiru aliwaagiza Watendaji wa Serikali zote mbili kuendelea na uratibu wa utekelezaji wa kazi za Ilani ndani ya Serikali hizo.
Alisema Ripoti ya Utekelezaji huo wa Ilani utakaoainishwa kwa pamoja wa Serikali zote mbili utapaswa kuwasilishwa katika Uongozi wa juu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi.
Alifahamisha kwamba kitabu kitakachotayarishwa kutokana na Ripoti hiyo ya Utekelezaji wa Ilani wa Serikali zote mbili kitaweza kusaidia kujua masuala yote yatakayoibua mafanikio na changamoto zinazowakabili Wananchi katika maeneo yote Mjini na Vijijini.
Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwa uamuzi na busara zake za kuiongoza Zanzibar katika mfumo aliyouanzisha wa Kushirikisha Viongozi na Wananchi moja kwa moja katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.
Dr. Bashiru alisema mfumo huo ambao Tanzania Bara haupo hutoa fursa kwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu wa ngazi zote za Serikali kuafuatilia changamoto zinazowakabili Wananchi na matokeo yake yamekuwa chachu ya Maendeleo yanayopatikana kutokana na ushiriki wa kila Mwananchi.
Alisema katika kufanikisha maendeleo hayo Dr. Bashiru alishauri Kamati Maalum ya CCM Zanzibar iendelee kupewa nafasi yake katika masuala yote ya Kisiasa yanayoihusu Zanzibar.
Alisema Kamati Maalum iliyoundwa na Chama cha Mapinduzi  kwa kuzingatia mazingira Maalum ya Zanzibar lazima iheshimike kwa vile imeundwa kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama hicho.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema Zanzibar Kisiasa bado iko salama  licha ya upinzani mkubwa unaojitokeza wakati wa chaguzi mbali mbali zinazohusisha Vyama vya CCM na CUF.
Balozi Seif  alisema wakati amani hiyo inaendelea kuwapa fursa Wananchi kuendelea na harakati zao za kimaisha Uongozi wa CCM Zanzibar unaendelea kujiweka tayari ili ujihakikishie inaendelea kuongoza Dola kwa upande wa Zanzibar ifikapo Mwaka 2020.
Dr. Bashiru Ali aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi kujiridhisha na sifa na uwezo aliyonao na kupewa jukumu hilo zito la kukisimamia Chama hicho kikiwa miongoni mwa Vyama vikongwe Barani Afrika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.