Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Amezitaka Taasisi Husika na Sekta ya Elimu Kumuaanda Mwanafunzi Masomo ya Kilimo Ngazi ya Msingi Hadi Sekondari na Chuo Kikuu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na vyombo mbali mbali vya Habari mara baada ya kumaliza zaiara yake ya kutembelea mabanda mbali mbali ndani ya Uwanja wa Mwalim Julius K. Nyerere Mkoani Morogoro. Picha na – OMPOR – ZNZ.
Na.OthmanKhamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema umefika sasa kwa kwa Wizara na Taasisi zinazohusika na Sekta ya Elimu Nchini kumuandaa Mwanafunzi katika masomo ya Kilimo kuanzia ngazi ya Msingi hadi Sekondari ili atakapofikia uwezo wa kuingia chuo Kikuu awe tayari ameshaelewa nini Kilimo.
Alisema uingizwaji wa  Mitaala ya Kilimo ndani ya masomo ya kawaida maskulini itamuwezesha Wanafunzi kujitayarisha mapema katika muelekeo wa kujijengea uwezo wa ajira ya uhakika ndani ya Sekta ya Kilimo wakati amalizapo masomo yake ili aweze kujitegemea kupitia Sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri wakati akizungumza na vyombo mbali mbali vya Habari mara  baada ya kumaliza ziara yake ya kuangalia Maonyesho  mbali mbali ya Siku ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoani Morogoro.
Alisema wakati Nchi imelenga kuwa Taifa la Viwanda litakayokuwa na Uchumi wa Kati ifikapo Mwaka 2525 maandalizi ya haraka yanahitajika yatakayokwenda sambamba na mpango huo utakaotoa afueni ya changamoto ya ajira inayowakumba zaidi Vijana wanaomaliza masomo yao ya Sekondari na Vyuo.
“ Mwanafunzi lazima aandaliwe mapema tokea elimu ya Msingi na Sekondari ili afikapo chuo Kikuu awe tayari ameshaelewa nini hasa Kilimo”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif aliwaeleza Wanahabari hao kwamba Wanafunzi wanaweza kuwa wajasiriamali wakubwa endapo wataamua kuelekeza nguvu zao katika Kilimo kilichoonyesha mabadiliko makubwa kutokana na Utaalamu wa kisasa unaotumika kwenye Sekta hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwasihi Vijana wa Zanzibar na Tanzania Bara kwa jumla kujikita zaidi katika Sekta ya kilimo huku Sewrikali zote mbili zikiendelea kujikita katika kutilia mkazo Sekta hiyo kwa kuongeza miundombinu imara zaidi inayokwenda na wakati wa sasa wa sayansi na Teknolojia.
Mapema Naye Katibu Tawala msaidizi wa Mkoa wa Morogoro  anayesimamia Kilimo, Uchumi na Uzalishaji Bwana Ernest Mkango alisema Maonyesho hayo yameshirikisha Taasisi na Wajasiri Amali kutoka Mikoa ya Tanga, Dar es salaam, Pwani na wenyeji Morogoro.
Bwana Ernest  alisema juhudi kubwa zimeanza kuchukuliwa na Serikali Kuu katika kuimarisha  miundombinu ya Sekta ya Kilimo sambamba na  upatikanaji wa zana bora na za kisasa za Kilimo zitakazowashawishi moja kwa moja Vijana kujiingiza katika Sekta ya Kilimo.
Katibu Tawala huyo Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro alifahamisha kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kutoka kwa Washirika wa Maonyesho hayo kutokana na ubinifu wa hali ya juu ulitumika katika uzalishaji wa Bidhaa na Mazao tofauti yanayoonekana kupendwa na Wananchi wanaotembelea maonyesho hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea baadhi ya Mabanda ya Maonyesho yao ikiwa ni pamoja na Manispaa ya Kiondoni Jijini Dar es salaam pamoja na Banda la Halmashauri ya Mkuranga.
Nyengine ni Banda la Manispaa ya Tanga, Halmashauri ya Kilosa Morogoro,Mradi wa kilimo cha mboga mboga wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Morogoro, Kiwanda cha Sukari Morogoro pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewapongeza Wajasiri Amali Nchini kwa hatua kubwa waliyopiga katika uzalishaji wa Bidhaa zinazokwenda na soko linalokubalika Kitaifa na nyengine Kimataifa.
Maadhimisho ya Siku ya Nane Nane  yafikia kilele chake Jumatano Tarehe 8 Agosti ambayo huadhimishwa Nchini Kote na ni siku inayokuwa mapumziko Tanzania Nzima.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.