Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Azungumza na Ujumbe Kutoka Nchini UAE Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Bibi Reem Ibrahim Alhashimy alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na ujumbe wake uliofika nchini kufuatia ziara ya Rais.aliyoifanya mwanzoni  mwa mwaka huu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Bibi Reem Ibrahim Alhashimy (katikati) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na ujumbe wake uliofika nchini kufuatia ziara ya Rais.aliyoifanya mwanzoni  mwa mwaka huu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifuatana na  Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Bibi Reem Ibrahim Alhashimy baada ya mazungumzo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na ujumbe wake waliofika nchini kufuatia ziara ya Rais.aliyoifanya mwanzoni  mwa mwaka katika Nchi hizo,[Picha na Ikulu.] 09/08/2018.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa Serikali ya Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuleta ujumbe wa timu ya Wataalamu ikiwa ni matokeo ya ziara yake aliyofanyika Januari mwaka huu katika umoja wa nchi hizo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) Reem Ibrahim Alhashimy ambaye pia, anaongoza wataalamu kutoka nchi za umoja wa nchi hizo aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa ujio huo umeonesha dhahiri kuwa viongozi wa kutoka Serikali ya Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wana hamu kubwa ya kutekeleza makubaliano ya mazungumzo aliyoyafanya kati yake na viongozi hao.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika ziara yake aliyoifanya mnamo mwezi Januari mwaka huu katika nchi za umoja huo ambako alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa umoja wa  nchi hizo ambao waliahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar ameamini kuwa azma yao hiyo imeanza kutekelezwa kwa vitendo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa azma hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo itatekelezwa kwa mashirikiano ya pande zote mbili.

Aliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar walipokea kwa furaha kubwa mazungumzo ya makubaliano yaliotokea baina ya pande mbili hizo na hatimae uongozi wa nchi za (UAE) ulipowafiki kuunga mkono mradi wa ukarabati wa hospitali ya Wete pamoja na ujenzi wa barabara ya Chake Chake Mkoani.

Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya miradi hiyo kwa upande wa kisiwa cha Pemba, miradi mengine yote iliyobakia kwa upande wa kisiwa cha Unguja wananchi wote kwa ujumla wamefurahia na kuonesha matumaini yao makubwa katika utekeleza wake ambao utasaidia kujiletea maendeleo na kuimarisha uchumi wa nchi.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza namna miradi hiyo itakavyoimarisha uchumi wa Zanzibar sambamba na kutekeleza vyema sekta za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo ikiwemo sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar.

Dk. Shein, pia, alieleza kuwa umoja wa nchi za (UAE) una historia ya muda mrefu katika kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya ambapo hapo siku za nyuma ilisaidia hata katika ukarabati wa hospitali kuu ya MnaziMmoja.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa matokea ya ziara yake ambayo yalimkutanisha na viongozi wakuu wa (UAE) akiwemo Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa (UAE), Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Makhtoum Makamo wa Rais na Waziri Mkuu wa (UAE) na Mtawala wa Dubai pamoja na Mtawala wa Sharjah Dk. Sheikh Sultan Mohammed Al Qasimi.


Nae kwa upande wake Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Nchi za UAE Reem Ibrahim Alhashimy, alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ujio wa Wataalamu hao kutoka (UAE) ni ishara kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya pande mbili hizo ni wa muda mrefu hivyo ni vyema ukaimarishwa.

Alieleza kuwa viongozi wan chi za umoja wa (UAE), umeazimia kutekeleza makubaliano yote yaliokubaliwa kufuatia ziara ya Rais Dk. Shein katika nchi hizo.

Aliongeza kuwa wataalamu wote waliokuwemo katika ujumbe huo anaoungoza watafanya kazi kwa kutembelea miradi iliyokusudiwa kwa upande wa Unguja na wengine wataenda kisiwani Pemba hapo kesho.

Waziri huyo alieleza kuwa kutokana na miradi hiyo kuwa na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii hasa katika masuala mazima ya miundombinu ikiwemo ya barabara, elimu, masuala ya kijamii, afya na mengineyo itasaidia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Zanzibar na wananchi wake.

Sambamba na hayo, kiongozi huyo alipongeza mapokezi mazuri aliyoyapata yeye na ujumbe wake na kuahidi kuwa (UAE) itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha yale yote yaliokubaliwa katika matokeo ya ziara ya Dk. Shein katika nchi za Umoja huo yanafanyiwa kazi kwa vitendo.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni pamoja na mradi wa ukarabati wa Hospitali ya Wete pamoja na ujenzi wa Barabara ya Chake hadi Mkoani kisiwani Pemba.
Aidha, kwa upande wa Unguja miradi itakayohusika ni mradi wa hospitali mpya ya Binguni, Mradi wa ukarabati wa nyumba za Mji Mkongwe, Miradi miwili ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) pamoja na Barabara ya Fumba-Uwanja wa ndege kuelekea mjini.
Katika timu hiyo ya wataalamu 16 pia, umo ujumbe kutoka Mfuko wa ‘Khalifa Fund’ ambao shughuli zake kubwa ni kuwasaidia wajasiriamali na wale wanaohitaji misaada ya aina mbali mbali

Dk. Ali AbdulKareem Al Obaidli ambaye ni Kiuu wa Kundi la masuala ya taaluma alitoa mwaliko kwa Zanzibar kuhudhuria katika Mkutano mkubwa utakaofanyika mnamo mwezi wa Septemba mwaka huu huko Abudhabi ambao utajikita zaidi katika masuala ya afya utakaozikutanisha nchi mbali mbali duniani ambapo pia, wajumbe watapata fursa ya kutembelea miradi mbali mbali ya afya nchini humo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.