Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndg Abdalla Juma Mabodi Amesema Watoto Yatima Kuthaminiwa







Na.Is-haka Omar. Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 
Zanzibar  Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi  amesema 
taasisi hiyo inathamini juhudi na mchango wa kuwasadia 
watoto yatima zinazofanywa na wadau wa maendeleo kutoka 
nchi mbali mbali duniani.

Hayo aliyasema wakati alipotembelea Kituo cha kulelea 
watoto yatima kinachomilikiwa na shirika la Direct AID 
kutoka nchini Kuwait kilichopo mtaa wa Ijitimai ya zamani 
Mwanakwerekwe Unguja, Dk. Mabodi alieleza kuwa 
ameridhishwa na juhudi za kituo kinachowapatia malezi 
bora watoto yatima wanaolelewa na shirika hilo.

Alisema shirika hilo limekuwa likifanya kazi kubwa ya 
kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala 
ya kijamii hasa uimarishaji wa huduma za maji safi na 
salama na elimu.

Dk.Mabodi alisema kwamba CCM ikiwa ni taasisi ya kisiasa 
itaendelea kuwa karibu na mashirika mbali mbali yenye 
dhamira ya kuendelea kuunga mkono juhudi za 
serikali,  katika kutatua kero na changamoto za jamii.

Amefafanua kwamba watoto ambao wazazi wao wamefariki 
wasipotunzwa na kuhudimiwa vizuri wanaweza kukosa haki 
zao za msingi zikiwemo malezi mazuri na elimu bora.

Alitoa wito kwa wananchi wa maeneo mbali mbali kuwa 
karibu na Watoto yatima kwani wengi wao wanakuwa 
wakitengwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishwaji hata 
kukosa fursa ya kupewa huduma muhimu za kibinadamu.

“CCM tutakuwa karibu zaidi na Direct AID kwani mmeamua 
kuisaidia jamii yetu nasi lazima tuonyeshe ungwana wetu wa 
kushirikiana nanyi kutatua changamoto zinazowakabili 
katika upangaji wa mikakati yenu ya kuisaidia jamii.”, 
alisema Dk. Mabodi.

Naye Mkurugenzi wa shirika hilo, Nd. Ayman Mohamed 
alisema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kuwapatia 
elimu watoto hao ili waweze kuwa na uwezo wa kujitegemea 
wenyewe mara baada ya kumaliza muda wa kuishi katika 
kituo hicho.

Alisema kituo hicho kimeweza kutoa vijana wengi wasomi 
wanaofanya kazi katika sekta mbali mbali za serikali na 
binafsi.

Nd.Ayman aliyataja malengo ya shirika hilo kuwa ni kujenga 
Vituo vya kisasa vya kulelea watoto yatima vitakavyokuwa na 
shule, vituo vya Afya na vyuo vya masomo ya dini ya 
kiislamu kwa Unguja na Pemba.

Akizungumza mmoja ya vijana waliolelewa katika Kituo 
hicho, Mhandisi  Abdulahi Salum Kassim alisema kituo 
hicho kimemlea akiwa na umri mdogo na kumsomesha hadi 
ngazi ya elimu ya juu ambapo hivi sasa ni mtumishi 
serikalini.

Alikiri kuwa mafanikio hayo yametokana na utaratibu mzuri 
uliowekwa na serikali wa kuruhusu shirika la Direct AID 
kuwasaidia watoto yatima.

“Shirika hili limenilea nikiwa mtoto mdogo na kunisomesha 
mpaka nimekuwa mtu mzima mwenye familia ambaye pia 
nawasaidia vijana wenzangu ambao nao wazazi wao 
walifariki wakiwa wadogo.”, alifafanua Mhandisi Abdulahi.

Naye Diwani wa Wadi ya Meli nne, Saleh Juma Kinana 
ambaye pia ni miongoni mwa vijana waliolelewa katika Kituo 
hicho, alisema watoto yatima wanatakiwa kulelewa na 
kuthaminiwa kama walivyo watoto wengine katika jamii.

Kituo hicho kinafuata malezi na miongozo ya dini ya Kiislam 
kina jumla ya watoto 44 ambao ni watoto yatima.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.