RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amelipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini
ya uongozi wa Spika wa Bunge hilo Job Ndugai kwa kutekeleza vyema kazi zake
ikiwa ni pamoja na kuwawakilisha vyema wananchi.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Job Ndugai aliyefika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa pamoja na viongozi wa Kamati ya uongozi wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na uongozi mzuri wa Spika wa Bunge hilo
hali inayoonesha kuwa Bunge hilo limepata maendeleo makubwa katika
kuwawakilisha wananchi.
Alieleza kuwa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza kupata mafanikio makubwa kutokana na
kuwa na uongozi makini sambamba na kuwepo Wabunge wenye ari na moyo wakuwatumikia
wananchi waliowachagua.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa kasi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mijadala
yake ni kubwa na inaonesha jinsi Wabunge walivyokuwa na ari ya kuwaletea
maendeleo wananchi.
Kutokana na juhudi
hizo, Rais Dk. Shein aliwataka Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuendelea kulitumikia vyema Bunge hilo kwa manufaa na maslahi ya nchi
na wananchi wote wa Tanzania kwani anaamini kuwa Tanzania itajengwa na
Watanzania wenyewe.
Aliongeza kuwa licha
ya kuwepo baadhi ya changamoto ndogo ndogo lakini bado Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania limekuwa likifanya kazi zake kwa ufanisi ukubwa na kuleta
matumaini makubwa kwa wananchi kwa kuyatetea maslahi yao.
Alieleza kuwa kutokea
kwa baadhi ya changamoto ndani ya Bunge kwa baadhi ya wakati kunatokana na uhalisia
wa Bunge kwani Mabunge yote duniani yamekuwa yakikabiliwa na changamoto kadhaa,
ambapo kwa Bunge la Tanzania hutokea kama
yalivyo Mabunge mengine na hatia hupatiwa ufumbuzi kutokana na uongozi makini
uliopo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa kwa upande wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar nalo kwa upande
wake limekuwa likifanya kazi vyema na kwa ari kubwa kutokana na Wajumbe wake
kuwa makini na kuwa na uwelewa na utambuzi mkubwa wa mambo.
Kwa upande wa
maendeleo ya kiuchumi yaliofikiwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais
Dk. Shein alisema kuwa Tanzania iko vizuri kutokana na uchumi wake kukua kwa
haraka ikilinganishwa na nchi nyengine za bara la Afrika hivyo ipo haja ya
kuendelea kuongeza kasi kwa mashirikiano ya pamoja.
Alieleza kwa upande wa
Tanzania Bara maendeleo yaliofikiwa leo sio yale yaliokuwa mwaka 1961 na kwa
Zanzibar hatua za maendeleo zilizofikiwa haiwezi kulinganishwa na ilivyokuwa
mwaka 1964 ambapo Zanzibar ilipata uhuru wake.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar nao kwa upande wake umekuwa
ukiimarika siku hadi siku kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na uongozi
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kulisimamia hilo.
Akieleza kuhusu suala
zima la amani, utulivu na usalama, Rais Dk. Shein alimueleza Spika huyo wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ujumbe wake kuwa Zanzibar iko
salama.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alisisitiza kuwa akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi ataendelea kuiongoza vyema Zanzibar na watu wake wote bila ya ubaguzi
wa aina yoyote.
Nae Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alimueleza Rais Dk. Shein madhumuni
makubwa ya uwepo wa viongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapa
Zanzibar.
Spika Ndugai
alimueleza Rais Dk. Shein kuwa viongozi wa Bunge hilo wapo Zanzibar kwa mafunzo
maalum ya siku mbili yanayowahusisha wajumbe wa Kamati ya uongozi, makamu
wenyeviti na wajumbe wa Tume ya Bunge yaliyoanza jana na kumalizika hivi leo
huko katika ukumbi wa Ofisi ndogo za Bunge ziliozpo Tunguu, Mkoa wa Kusini
Unguja.
Alieleza kuwa katika
mafunzo hayo pia, wamewahusisha Spika wastaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Zanzibar kwa lengo la kuchota busara, maarifa, uzoefu na umakini
mkubwa wa ungozi wa Mabunge kutoka kwa viongozi hao.
Spika huyo wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesifu amani, utulivu na usalama mkubwa uliopo
Zanzibar na kupongeza hatua na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein katika kuendelea
kuiletea maendeleo Zanzibar na watu wake.
Pia, Spika huyo wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesifu hatua zilizochukuliwa katika
ujenzi wa hoteli za kisasa katika mji wa Zanzibar ambazo zimekuwa kivutio kikubwa
kwa wageni na wenyeji wa Zanzibar ikiwemo hoteli mpya ya kisasa ya Verde.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment