Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein, Azungumza na Wafanyabiasha na Wawekezaji na Kuwakaribisha Kuweza Zanzibar.

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Meya wa Jimbo la Gorontalo Prof.Nelson Pamalingo wakati wa mkutano na Meya huyo yaliyogusia zaidi katika ushikiano wa kilimo cha Minazi hafla ya mazungumzo hayo ilifanyika katika ukumbi wa Hoteli ya  Borobudur Mjini Jakarta,Indonesia katika ziara ya kikazi kwa mualiko wa Makamo wa Rais wa Nchi hiyo Mohammed Jusuf Kalla.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchini Indonesia kuja kufanyabiashara na kuwekeza Zanzibar kutokana na fursa mbali mbali zilizopo.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda ya Indonesia (KADIN), huko katika ukumbi wa ofisi ya Jumuiya hiyo iliyopo mjini Jakarta Indonesia.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuna sababu mbali mbali ambazo wawekezaji wanaweza kuichagua Zanzibar kama ni sehemu pekee ya kuekeza ikiwa ni pamoja na kuwepo mazingira mazuri ya uwekezaji yaliowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwa na soko kubwa la kibiashara linalojumuisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha, Rais Dk. Shein aliwaeleza wanajumuiya hiyo kuwa miongoni mwa sababu kubwa ambayo Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia ni kuwepo kwa amani, usalama na utulivu mkubwa nchini Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa kunaweza kuimarishwa uhusiano madhubuti kati ya taasisi zinazomilikiwa na Serikali zote mbili katika maeneo ya biashara na uendelezaji wa miundombinu ambapo uhusiano kama huo pia, unaweza kuanzishwa kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kampuni mbali mbali za binafsi za nchini Indonesia.

Akitangaza fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar katika sekta mbali mbali za uchumi, katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis Nassor alieleza kuwa Zanzibar ni eneo la pekee lenye matumaini katika kuekeza sekta kadhaa za uchumi.

Nao viongozi na Wanajumuiya ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda ya Indonesia (KADIN), walileza mafanikio waliyoyapata katika Jumuiya yao hiyo na kuahidi kuitumia vyema fursa ya kuja kuekeza na kufanya biashara Zanzibar ikiwa ni kuitikia wito wa Rais Dk. Shein wa kuwataka kuekeza Zanzibar.

Mara baada ya mkutano huo, Rais Dk. Shein alikutana na uongozi wa Kampuni ya mafuta na gesi ya Pertamina ya nchini humo ambao ulimueleza mafanikio iliyoyapata katika shughuli zake kwenye sekta hizo na kueleza kuwa tayari imeshaanza kufanya shughuli zake  huko Tanzania Bara katika maeneo ya Lindi na Mafia.

Hivyo, kutokana na mkutano huo Kampuni hiyo ilivutika na kuahidi kuitumia fursa hiyo ili kuangalia uwezekano wa kuanzisha mashirikiano na kuja kuekeza Zanzibar hasa ikizingatia uzoefu na mafanikio iliyoyapata katika sekta hizo.

Mapema katika ukumbi wa Hoteli ya Borobudur, Rais Dk. Shein alikuna na kufanya mazungumzo na Meya wa Jimbo la Gorontalo, Profesa Nelson Pomalingo ambapo Rais Dk. Shein na kiongozi huyo walieleza haja ya kuimaisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Indonesia katika sekta ya kilimo hasa kilimo cha minazi.

Nae kiongozi huyo wa Jimbo la Gorontala alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Indonesia na Zanzibar ni maeneo yaliyofanana kijiografia hivyo kushirikiana katika sekta ya kilimo kuna weza kuongeza tija na hatimae kuleta mafanikio kwa pande zote mbili.

Hata hivyo, kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa katika kilimo cha minazi licha ya kuwa changamoto zilizopo katika kilimo hicho kwa upande wa Indonesia zinafanana na zile za Zanzibar lakini hata hivyo nchi hiyo imeweza kupata mafanikio makubwa kayika kilimo cha minazi.

Katika mazunguzo hayo, kiongozi huyo wa Gorontalo aliahidi kuanzisha na kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo na kusisitiza kuwa atahakikisha mashirikiano yanafanyika katika kuhakikisha kilimo hicho kinaimarika katika visiwa vya Zanzibar.

Wakati huo huo, viongozi na watendaji wakuu wa Serikali walioambatana na Rais Dk. Shein katika ziara yake hiyo walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na watendaji wenzao wa nchini Indonesia katika ukumbi wa hoteli ya Borobudur.

Katika mikutano hiyo iliyofanyika kwa nyakati tofauti, viongozi na watendaji hao walieleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja sambamba na kubadilishana uzoefu na utaalamu katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiweko sekta ya utalii, uvuvi na kilimo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.