Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni (kulia), akiwaongoza viongozi wengine kutembelea eneo la mwambao
wa Ziwa Victoria baada ya kuikabidhi
boti hiyo ya doria kwa Jeshi la Polisi, kutoka kushoto ni Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Daniel
Shilla, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel na Diwani wa Chato, Richard Bagolele
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni (aliyeshika koti), akishuka katika boti maalumu aliyowakabidhi
Kikosi cha Polisi wilayani Chato ikiwa ni mkakati wa Serikali kupambana na
uhalifu katika ukanda wa Ziwa na Bahari nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, akishuka katika boti maalumu iliyokabidhiwa na Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(hayupo pichani) kwa Kikosi
cha Polisi Wanamaji wilayani Chato,
ikiwa ni mkakati wa Serikali kupambana na uhalifu katika ukanda wa Ziwa na
Bahari nchini.
Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Geita, Daniel Shilla akimshukuru Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mhandisi Hamad Masauni baada ya kumkabidhi Kituo cha Polisi
kinachohamishika wilayani Chato.Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi
Robert Gabriel. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na
Mwandishi Wetu
Serikali imejipanga
kuimarisha Ulinzi na Usalama katika Ukanda wa Ziwa na Bahari kote nchini ili
kuweza kudhibiti uhalifu unaotekelezwa majini ikiwepo uvuvi haramu,
usafirishaji wa magendo na uhalifu mwingine unaotokea katika maeneo ya ziwa na
bahari.
Akizungumza wakati wa
makabidhiano ya boti maalumu ya doria na ufunguzi wa Kituo cha Polisi Wanamaji,
wilayani Chato, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni
amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha inadhibiti uhalifu
katika Ukanda wa Ziwa na Bahari kwa kutumia Vyombo vya Ulinzi na Usalama
vilivyopo chini ya serikali, ili kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli za
kuchumi bila ya kuwa na wasiwasi juu ya usalama wao
Alisema moja ya
changamoto kubwa aliyoelezwa wakati alivyofanya ziara ya awali wilayani Chato
ni kuwepo kwa matukio ya uhalifu ziwani yaliyopelekea baadhi ya wananchi
kusitisha shughuli za kiuchumi katika mwambao huo wa Ziwa Victoria.
“Serikali ya Awamu ya
Tano imedhamiria kuleta maendeleo katika nyanja zote na kuwawekea mazingira
mazuri wananchi wake kujishughulisha na shughuli za kiuchumi, hivyo basi
tutahakikisha tunaimarisha ulinzi katika sehemu zote ambazo wananchi wanafanya
shughuli zao ikiwepo ukanda wa ziwa na bahari na leo hii tunaanzia hapa
wilayani Chato.
“Pia nawasihi askari polisi
kufanya kazi kwa maadili na agizo hili nalitoa kwa nchi nzima na serikali
kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi aitomvumilia askari yoyote atakaebainika
kuwabambikia kesi wananchi,hatua kali zitachukuliwa kwa atakaebainika” alisema
Masauni ambae pia ni Mbunge wa Kikwajuni
Naye Diwani wa Kata ya
Muungano, wilayani Chato,Johnson Kilimokwanza alisema anaishukuru serikali kwa
kuleta boti hiyo na ufunguzi wa kituo cha polisi kwani moja ya changamoto
iliyokuwa inawasumbua wavuvi katika mwambao huo ni masuala ya uhalifu unaotokea
ziwani huku akiweka wazi uwepo wa kituo na boti ya doria vitapunguza masuala ya
uhalifu.
Mmoja wa askari polisi ambae
hakupenda jina lake litajwe alisema wao wanaishukuru serikali kwa
kuwaletea boti na kituo ambavyo
vitawarahisishia kupambana na uhalifu
“Muhimu naomba serikali
pia waweze kutuletea gari ambalo litasaidia pia katika mapambano hayo ya
uhalifu kama unavyoona tayari tuna kituo hapa cha wanamaji naibu waziri
amekizindua,muhimu sasa tuletewe usafiri utakaowezesha kupeleka mahabusu
mahakamani,” alisema askari polisi huyo.
No comments:
Post a Comment