Habari za Punde

SERIKALI YATOA SHILINGI MILIONI 500 KWA AJILI YA UJENZI WA KITUO CHA AFYA KIJIJI CHA MAKUNGU MKOANI SINGIDA

 Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mheshimiwa Elibariki Kingu, akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Makungu katika mkutano wa hadhara uliohusu miradi ya maendeleo ukiwemo wa ujenzi wa kituo cha afya kitakacho gharimu sh.milioni 500 zilizotolewa na serikali uliofanyika wilayani Ikungi mkoani Singida jana.
 Wananchi wakifuatilia mkutano huo.
 Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Iyumbu, Mohamed Itambu Athumani, akizungumza katika mkutano huo.
 Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Ikungi, Mheshimiwa Tweve, akizungumza kwenye mkutano huo.
 Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iyumbu, Tatu Bolosi, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Makungu.
 Diwani wa Kata ya Iyumbu, Peter Gwiligwa, akizungumza.
 Wananchi wa Kijiji cha Makungu, wakishoona mikono kukubali kushiriki shughuli za miradi ya maendeleo.
 Hapa ni furaha tupu wakati wakimsikiliza mbunge wao katika mkutano huo.
 Nyimbo za hamasa zikiimbwa kwenye mkutano huo.
 Mkutano ukiendelea.
 Mhandisi wa Maji, akizungumza na wananchi wa kijiji hicho kuhusu kupatikana kwa maji katika eneo hilo.
 Msanii Omari Kiherehere kutoka Mjini Singida akitoa burudani ya ushairi.
Baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Makungu wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano huo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

SERIKALI imetoa sh.milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya chenye hadhi ya kimataifa kitakachojengwa Kijiji cha  Makungu Kata ya Iyumbu Wilayani Ikungi Mkoa wa Singida.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mheshimiwa Elibariki Kingu, wakati akiwahutubia wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana.

"Ndugu zangu licha ya wiki iliyopita kunipokea kwa mabango yaliyokuwa yakielezea changamoto mbalimbali mlizonazo leo nimewaletea habari njema kwani kupitia jitihada zangu binafsi Serikali imeweza kusikia kilio chenu ambapo imetoa sh.milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kijiji chenu cha  Makungu" alisema Kingu huku wananchi wakilipuka kwa shangwe.

Kingu aliwaambia wananchi wa kata hiyo kuwa amerudi kwa mara ya pili katika kijiji hicho ili kuzungumzia utatuzi wa changamoto kadhaa walizozitoa wananchi hao kupitia mabango yao ambazo zilikuwa ni shule, maji, barabara, umeme pamoja na kuwekewa mnara wa simu ambapo tayari alikuwa ameenda na majibu yake.

"Nimekuja na majibu ya changamoto zetu kwani mungu amesikia kilio chenu kuhusu changamoto ya maji leo hapa nimekuja na Mhandisi wa maji ambaye atawaelezeni nini kifanyike ili mpate maji, na kuhusu shule licha ya kutoa saruji ambayo mmeifungia 
ndani bila kuifanyia kazi tangu mwaka 2016 nitawapa mifuko mingine 100 ili muendelee na ujenzi wakati Usambaji wa Umeme Vijiji wa REA awamu ya tatu ukisubiriwa baada ya kuhakikishiwa na wahusika ambapo utawekwa katika kata mbili ikiwemo hii ya kwenu katika mwaka huu wa fedha wa 2018/2019" alisema Kingu.

Akizungumzia miradi hiyo itakayo jengwa kwenye kata hiyo Kingu alisema kituo cha afya kitakaho jengwa katika kata hiyo kitakuwa na wodi kwa ajili ya wajawazito, chumba cha upasuaji, maabara, jengo maalumu la kuchomea takataka pamoja na nyumba ya daktari ambapo kuhusu mnara wa simu tayari ameitwa  jijini Dodoma na waziri husika kuona namna atakavyosaidiwa kuweka mnara huo haraka iwezekanavyo.

Kingu aliwataka wananchi hao kuunga mkono jitihada za serikali kwa kujitoa kimichango na nguvu kazi ili kukamilisha miradi hiyo ambapo wote kwa umoja wao walimuhakikishia ushiriki wao kwa kunyoosha mikono huku akimtaka Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Tatu Bolosi kuanza kuandaa eneo kitakapo jengwa kituo hicho ili ujenzi huo uanze mara moja baada ya fedha hizo kuingizwa benki mapema mwezi ujao. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.