Habari za Punde

TRA Yaendelea Kutoa Elimu ya Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Kodi.

 Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka akitoa elimu juu ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi wakati wa semina elekezi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali iliyofanyika mkoani Kigoma kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu msamaha huo.
Afisa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Chama Siriwa akiwasilisha mada kuhusu msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi wakati wa semina elekezi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali iliyofanyika mkoani Kigoma kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu msamaha huo.
Baadhi ya wafanyabiashara na wadau mbalimbali waliohudhuria semina elekezi ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi iliyofanyika mkoani Kigoma kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu msamaha huo. 
Baadhi ya wafanyabiashara na wadau mbalimbali waliohudhuria semina elekezi ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi iliyofanyika mkoani Kigoma kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu msamaha huo. (Na Mpiga picha wetu)

 Na Veronica Kazimoto. Kigoma 26 Agosti, 2018
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kutoa elimu juu ya namna ya kuomba msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa semina elekezi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali mkoani Kigoma, Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo Rose Mahendeka amewaambia wafanyabiashara hao kuwa lengo la kutoa msamaha huo ni kuwapunguzia mzigo ili waweze kulipa kodi ya msingi isiyokuwa na riba wala adhabu ambapo mwisho wa kulipa kodi hiyo ni tarehe 30 Juni, 2019.

"Serikali imeamua kutoa msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 ili kuwasaidia wafanyabiashara kulipa kodi ya msingi tu ambayo mfanyabiashara anaweza kuilipa mara moja au kwa awamu ndani ya Mwaka wa Fedha 2018/19," alisema Mahendeka.

Mahendeka ameeleza kuwa, msamaha huu ni wa miezi 6 na ulianza mwezi Julai na utamalizika Desemba, 2018 na kuongeza kuwa huu ni muda muafaka wa wafanyabiashara hao kutuma maombi ya msamaha huo kabla muda uliopangwa haujamalizika.

"Natumia fursa hii kuwasihi wafanyabiashara kutuma maombi TRA ya msamaha huu kabla ya mwezi Novemba, 2018 na msisite kuwasiliana na ofisi yetu ya hapa mkoani pindi mtakapohitaji ufafanuzi zaidi," aliongeza Mahendeka.

Aidha, Mahendeka alisisitiza kuwa TRA itatoa majibu ya maombi ya msamaha huo kwa maandishi ndani ya siku thelathini (30) tangu siku ya kupokea maombi.

Naye Mfanyabiashara wa Vifaa vya Ujenzi ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani hapa Raymond Ndabhiyegetse ameishukuru TRA kwa kutoa elimu hiyo ya msamaha wa kodi  na kuiomba mamlaka kuwashawishi watengeneza hesabu (wahasibu) kuwekeza mkoani Kigoma kwa kuweka wahasibu wengi ambao watawasaidia kutengeneza hesabu za biasahara zao.

"Mimi napenda kuishukuru TRA kwa kutupatia uelewa huu wa namna ya kuomba msamaha wa riba na adhabu za kodi, kwakweli elimu mliyotupatia leo imetusaidia sana. Pia naomba TRA mtusadie kuwashawishi watengeneza hesabu waje Kigoma kwa sababu tuna changamoto kubwa ya watengeneza hesabu na kwa sasa tunao wawili tu, hivyo tunapata changamoto kubwa katika kutengeneza hesabu zetu," alisema  Ndabhiyegetse.


Baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoa msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100, TRA imejiwekea mikakati ya kufikisha ujumbe huo kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukutana na wafanyabiashara kwa lengo la kutoa uelewa juu ya namna ya kuomba msamaha huo kabla muda uliopangwa haujamalizika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.