Habari za Punde

UJAMBAZI WA SILAHA UMEPUNGUA NCHINI-IGP.


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na  na Wakazi wa Kata ya Mto wa Mbu Wilayani Monduli katika mkutano wa hadhara wakati wa Ziara yakeya kikazi Mkoani Arusha yenye lengo la kutatua changamoto za uhalifu (Picha na Jeshi la Polisi).



Na Jeshi la Polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro ametoa onyo kali kwa majambazi na wahalifu wengine hususani wanaotumia silaha za moto kuacha mara moja kabla ya kukutana na moto mkali wa Jeshi la Polisi ambapo pia ametoa wito kwa wazazi kuwakanya watoto wao kujihusisha na vitendo hivyo.
IGP Sirro ameyasema hayo wakati akizungumza na Wakazi wa Mto wa Mbu Tarafa ya Manyara Wilayani Monduli Mkoani Arusha wakati wa Ziara yake mkoani humo yenye lengo la kubaini changamoto za kiuhalifu na kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema hivi sasa ujambazi wa kutumia silaha umepungua kwa kiasi kikubwa na baadhi ya matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza yanaendelea kudhibitiwa na Jeshi la Polisi.
“Nawasihi wanaofikiria kuendelea kufanya vitendo vya uhalifu ikiwemo vya utumiaji wa silaha na kuua watu waache mara moja kwa kuwa wakikutana na moto wa Jeshi la Polisi wasije wakajilaumu mana kwa sasa moto wetu ni mkali hivyo nawashauri wazazi wakanye watoto wao” Alisema Sirro.
Aidha amewataka Wakazi wa Mto wa mbu Wilayani Monduli kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kuwa usalama umeimarishwa katika kupambana na wahalifu waliokuwa wakifanya vitendo vya kuwaua watu hususani wanawake ambapo katika kipindi cha hivi karibuni kuliripotiwa matukio kadhaa ambayo yalileta wasiwasi katika eneo hilo muhimu kwa utalii.
Amewataka Viongozi wa Vijiji na Kata kuhakikisha kuwa suala zima la ulinzi na usalama linatiliwa mkazo ili kuhakikisha hakuna mhalifu katika maeneo yao na wageni wanapoingia wachukue taarifa zao mapema.
Kwa Upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mto wa Mbu Bi. Kuluthum Hassan alisema Wahalifu wanaouza bangi, pombe ya gongo na dawa za kulevya wanaendelea kuwafichua ili wafikishwe katika vyombo vya dola na hivi sasa wanaendelea na mipango ya ujenzi wa kituo kikubwa cha Polisi kitakachoendana na hadhi ya eneo hilo.
Nao wananchi mbalilmbali wa Mto wa mbu wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanakuwa salama wakati wote hususani kipindi hiki cha watalii wengi katika maeneo hayo na wameahidi kuchangia ujenzi wa kituo cha Polisi ili kuboresha usalama katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.