Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto), akitoka kukagua Kituo cha Forodha na Ushuru cha Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji (Kilambo), alipofanya ziara na kuzungumza na wafanyakazi wa Kituo hicho, mkoani Mtwara.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara
WAKAZI wa Kijiji cha Kilambo, Wilaya ya Mtwara, mkoani
Mtwara, wameiomba Serikali iwasaidie kuwatafutia
mwekezaji atakayejenga kiwanda cha kusindika matunda na
mazao ya kilimo katika kijiji chao kutokana na kijiji hicho
kuwa na matunda na mazao mbalimbali yanayokosa soko na
kuwasababishia umasikini.
Wakazi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha
Kilambo Bw. Mohamed Mkama, wametoa ombi hilo mbele
yaWaziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango,
aliyefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Forodha cha
Kilambo, kilichoko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji,
mkoani Mtwara, kwamba kijiji chao kina fursa nyingi za
kilimo zinazohitaji viwanda vya kuongeza thamani ya mazao
yao na kutoa ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo Bw. Mohamed Mkama,
alisema kuwa Kijiji chao kinapakana na nchi ya Msumbiji
ambako kuna mwingiliano mkubwa wa watu katika masuala
ya biashara na uhusiano wa kijamii ikiwemo pande mbili za
nchi kuoleana hivyo kuwafanya wananchi wa Msumbiji
waishio mpakani kutegemea bidhaa kwa wingi kutoka katika
kijiji chao.
"Watu kutoka Msumbiji wananunua sana chakula na bidhaa
nyingine kutoka kwetu lakini tunawauzia bidhaa bila
kuongeza thamani hivyo uwepo wa kiwanda utakuza uchumi
wa kijiji chetu na tunakuomba Mhe. Waziri wa Fedha na
Mipango, utusaidie kupata kiwanda ili nasi tuweze
kunufaika" alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Kijiji
Mkazi mwingine wa Kijiji hicho Bw. Selemani Kumamba,
alimweleza Waziri wa Fedha na Mipango kwamba Kijiji chao
ni maarufu kwa kilimo cha matunda hivyo wanapendekeza
kujengwa kwa kiwanda cha kusindika matunda ili juisi
itakayozalishwa katika kijiji chao iwe na soko.
"Mhe. Waziri sisi ni wakulima wazuri wa matunda lakini
matunda yetu wakati wa msimu yanakosa soka, yanaoza na
tunayatupa jambo linalotulazimu tukuombe utusaidie
kuhamasisha wawezezaji waje wajenge kiwanda cha
kusindika juisi katika kijiji chetu ili nasi tuondokane na
umasikini" alisema mzee Selemani Kumamba
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango,
aliwaambia wakazi hao kwamba inabidi ufanyike utafiti wa
kutosha ili kubaini wingi wa mazao yanayozalishwa na
wakulima katika kijiji hicho na vijiji jirani ili kupata takwimu
sahihi za uzalishaji wa mazao hayo yakiwemo matunda ili
kuiwezesha Serikali kuwashawishi wawekezaji kujenga
kiwanda katika eneo hilo na kuwapongeza wakulima hao
kwakufanya kazi kwa bidii na mawazo yao ya kujiletea
maendeleo.
"Tukiwa na uhakika huo hata mwekezaji anayekuja
tutamwambia kwa mwaka mmoja, kwa wastani, kijiji hiki na
vijiji jirani vinazalisha maenbe kiasi fulani, kwa hiyo wazo la
kutaka kuwa ni kiwanda ni zuri lakini linahitaji kufanyiwa
kazi zaidi" alisema Dkt. Mpango aliyeambatana na Mkuu wa
Wilaya ya Mtwara, Bw. Evod Mmanda
Aliwasahauri wanakijiji hao kuanzisha mashamba mapya ya
matunda na kupanda mbegu za kisasa zinazozaa kwa wingi
na kuushauri uongozi wa wilaya kuwasaidia wananchi hao
kupata miche ya kisasa inayozaa kwa muda mfupi ili waweze
kushawishi zaidi kupatikana kwa kiwanda kijijini hapo.
Dokta Philip Mpango, yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya
kikazi ambapo pamoja na mambo mengine amekutana na
wafanyabiashara wa mkoa wa Kigoma pamoja na
Kutembelea taasisi zilizochini ya Wizara hiyo.
No comments:
Post a Comment