Habari za Punde

ZANZIBAR YAADHIMISHA WIKI YA KUNYONYESHA.

Afisa lishe Wilaya ya kati Unguja Mwanahija Kombo Mbarouk akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na Wiki ya Unyonyeshaji inayoanza leo, ambapo amewataka Wazazi kuwanyonyesha watoto muda usioupungua miezi sita bila kuwapa kitu chochote. (Picha na Abdallah Omar-Maelezo Zanzibar)
Na Ramadhani Ali – Maelezo.
Maafisa wa Kitengo cha Lishe Zanzibnar wamesisitiza umuhimu wa akinamama kufuata taratibu za kitaalamu katika kunyonyesha watoto wao ili kuhakikisha wanapata maziwa ya kutosha na kukua vizuri.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja, katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji, wamesema kutofuata taratibu zinazotakiwa katika kunyonyesha kunapelekea watoto wengi kupata maradhi ya mtapiamlo na kutokukua vizuri.
Afisa Lishe Wilaya ya Kati Wanu Haji Ali alisema jamii imejenga tabia ya kuwapa chakula chengine watoto wakiwa chini ya umri wa miezi sita kwa kisingizio kuwa maziwa ya mama pekee hayatoshi jambo ambalo sio la kweli.
Alisema katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo mtoto hatakiwa kupewa chakula chengine chochote, hata maji, isipokuwa maziwa ya mama pekee kwani yanavirutubisho vya kutosha kwa ajili ya kujenga afya yake.
Bi. Mwanahija alizitaja baadhi ya taratibu za kitaalamu za kunyonyesha mtoto kuwa ni muda wa dakika 20 kila baada ya saa mbili kwa kipindi cha miaka miwili bila kumuachisha ziwa.
Alisema maziwa ya mama yanamchanganyiko wa maji na chakula kwa ajili ya mtoto lakini akinamama wengi hawawapi muda wa kutosha watoto kunyonya na hatimae hupata maziwa ya mwanzo yaliyokosa virutubisha ya chakula.
Aliwashauri akinamama wanaofanyakazi na kuwaacha watoto kwa walezi kukamua maziwa ya kifua na kuyahifadhi katika mazingira mazuri na kupewa mtoto kwani yanaweza kukaa mpaka saa nane bila kuharibika na siku mbili yakitiwa ndani ya friji.
Kwa upande wake Afisa Lishe Wizara ya Afya Munira Khamis alisema mama anayenyonyesha anahitaji kupewa msaada na mashirikiano makubwa na familia ikiwa ni pamoja na kupunguziwa mzigo wa kazi.
Alisisitiza umuhimu kwa wazazi kuwanyonyesha watoto mara tu baada ya kuzaliwa kwani maziwa ya siku za awali ni kinga ya vimelea vya maradhi kwa mtoto mchanga.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji mwaka huu ‘maziwa ya mama ni chakula cha pekee kwa mtoto chini ya umri wa miezi sita’

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.