Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) alipokuwa akitoa hutuba yake kwa Wananchi na Wanafunzi katika sherehe ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Skuli mpya Sekondari ya Kinuni Jimbo la Pangawe Wilaya ya Magharibi"B" Mkoa wa Mjini Magharibi,sherehe zilizofanyika leo sambamba na Skuli 9 za Sekondari za Zanzibar,(kulia) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe.Riziki Pembe Juma(kushoto)Waziri Kiomgozi Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Kijito Upele Mhe.Shamsi Vuai Nahodha na Naibu katibu Mkuu CCM Zanzibar Dk.Juma Abdala Sadala(wa pili kushoto),[Picha na Ikulu.] 21/09/2018.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa azma ya Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume kutangaza elimu bure kwa watoto wa Zanzibar bila ubaguzi ilikuwa ni
utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha ASP ambayo inaendelea kutekelezwa
hadi hivi leo.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika hafla ya uwekaji mawe ya Msingi ya Skuli 9 za ghorofa Unguja na
Pemba ambapo kwa niaba ya skuli hizo aliweka jiwe la msingi skuli ya Kinuni,
Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni kati ya skuli hizo mpya hatua ambayo ni miongoni
mwa shamrashamra za kusherehekea miaka 54 ya Elimu bure ambapo kilele chake ni
Septemba 23 mwaka huu.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa utekelezaji huo unaendelea kutoka kwa chama cha ASP na hivi sasa CCM
ambapo ujenzi wa skuli hizo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwani
hayo ni mambo yaliopangwa na Chama hicho.
“Nilipoiona skuli hii
mpya niliona kweli kinu kimejaa hapana hata mmoja kati yetu aliyekuwa na wazo
kuwa Kinuni kutakuwa na skuli kama hii, lazima tushuruku neema hizi kwani
tukishukuru Mwenyezi Mungu atatuongezea”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alisema
kuwa kutangazwa kwa elimu bure kulikuwa na maana kubwa katika kutekeleza
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kusisitiza kuwa elimu bure msingi wake ni
kuondoa ubaguzi katika kuwapa elimu watoto wa Zanzibar kwani watoto wa kinyonge
walikuwa hawapati elimu inayopaswa kwani walidhulumiwa kupata haki yao hiyo ya
msingi.
Dk. Shein alisema kuwa elimu
ndio msingi wa mwanzo wa maendeleo na maisha ya mwanaadamu duniani hivyo ndio
maana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta hiyo na matokeo
ya mafanikio yanayopatikana hivi sasa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta
ya elimu yanayotokana na Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo Zanzibar
inajivunia hadi hii leo.
Alieleza kuwa akiwa Rais
wa Zanzibar anajivunia kuendelea kutoa elimu bure kwani Mzee Karume aliamua
chini ya ASP na awamu ya Saba itaendeleza chini ya uongozi wa CCM na kusisitiza
kuwa kuwa kasi ya Zanzibar ni kasi ya maendeleo katika kutoa elimu bora, na
kuipanua elimu kwa mahitaji ya sasa na ya hapo baadae na.
Akieleza juhudi
zinazochukuliwa katika kutatua changamoto kwenye sekta za elimu, Dk. Shein
alieleza kuwa hivi karibuni madawati yapatayo 22,000 yatawasili kutoka nchini
China na mengine yatafuata hapo baadae huku akieleza changamoto ya ukosefu wa
walimu wa sayanasi ambapo Serikali kupitia vyuo vyake vikuu vilivyopo nchini
kikiwemo chuo cha SUZA vinasomesha kada hiyo.
Hivi sasa Zanzibar
inasomesha wataalamu wake wenyewe ili kuweza kutoa mafunzo hasa katika masomo
ya sayansi. “Leo tumeandika historia potelea mbali wanaonuna na wanune lakini
tushajenga na watoto wetu watasoma, watapata elimu itakayowasaidia leo, kesho hadi
mtondogoo”, alisisitiza Dk. Shein.
Alisema kuwa utekelezaji
huo ni mpango uliopangwa mnamo mwaka 2014 wa skuli 10 ambapo moja ya skuli hizo
ni ya Mwembeshauri ambayo ni skuli mbili kwa pamoja ambapo Serikali imekopa
pesa kutoka ‘OPEC Fund” ili kuwaendeleza
watoto wa Zanzibar kupata elimu kwa azma ya kuja kuwaendesha wao na wazee wao.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa Serikali itaiendeleza Kinuni kutokana na eneo hilo kukua kwa idadi ya watu
pamoja na makaazi yao.
Alitumia fursa hiyo
kutoa agizo kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kushirikiana
na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kuhakikisha kuwa mwezi
Septemba mwakani iwe imekamilisha ujenzi wa barabara ya Kinuni kwa kiwango cha
lami ili wananchi wakiwemo wanafunzi waweze kupita bila usumbufu.
Rais Dk. Shein
alisisitiza utekelezaji wa mipango ya ardhi katika kupanga majengo ya wananchi
pamoja na miundombinu mengine na ndio maana Serikali imeanza kujenga majengo ya
ghorofa kwa lengo la kutumia ardhi ndogo.
Alieleza kuwa pale
Serikali inapotangaza wananchi wake wasivamie ardhi wawe wasikifu kwani ardhi
ya Zanzibar ni ndogo na wananchi wake ni wengi kwani Zanzibar ina idadi ya watu
wanaokadiriwa kufikia milioni 1.5 wakati mpaka panafanyika Mapinduzi ya Januari
12, 1964 Zanzibar ilikuwa na idadi ya wananchi 320,000 tu.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa elimu ya Msingi na Sekondari itaendelea kutolewa bure na kwa wale
watakaowalipisha watoto wa skuli za Msingi hatua kali za kisheria zitachukuliwa
zidi yao huku akitumia fursa hiyo kuahidi kupelekwa walimu wa Sayansi katika
skuli hiyo.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwataka wananchi kuishi kwa amani, utumiliu na upendo na kuongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya kazi ya kuwapelekea maendeleo
wananchi wote wa Zanzibar bila ya ubaguzi kwa lengo la kufaidi matunda ya
Mapinduzi.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk.
Shein kutokana na Serikali anayoiongoza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo ikiwa
ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Waziri Pembe
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Wizara yake itahakikisha inatoa elimu iliyo
bora na yenye viwango huku akiahidi kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa
kwa yule atakayekwenda kinyume na taratibu zilizowekwa.
Alitoa pongezi kwa
Kampuni ya kizalendo ya Saleem Construction LMT (SALCON) kwa uzalendo mkubwa
ulioufanya wa kusaidia ujenzi wa madarasa manne iliyoyajenga pembezoni mwa
skuli hiyo mpya.
Mapema Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dk. Idrissa Muslim Hija alisema kuwa ujenzi
wa skuli hiyo mpya ya Sekondari ya Kinuni ni miongoni mwa skuli tisa
zinazojengwa Unguja na Pemba ambapo kati ya hizo tano zinajengwa Unguja na nne
zinajengwa Pemba.
Akizitaja zinazojengwa
Unguja kuwa ni Kinuni, Mwembeshauri, Chumbuni, Bububu na Fuoni na Pemba ni
Wara, Mwambe, Kizimbani na Micheweni ambapo ujenzi huo unatekelezwa kwa mashirikiano
makubwa kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wahisani “Opec Fund for
International Development” (OFID) kupitia mradi wa Zanzibar “Third Education
Project” (ZATEP).
Alisema kuwa skuli hiyo
na nyengine zinazojengwa zitasaidia sana kupunguza msongamano wa wanafunzi
darasani na kuweka mazingira mazuri ya kujifunza kwa watoto na hatimaye waweze
kufanya vizuri katika mitihani yao hasa ikizingatiwa kuwa watoto wanaosoma
skuli ya Msingi ya Kinuni pekee wanapindukia 5017.
Aliongeza kuwa jumla ya Dola
za Kimarekani milioni 10.2 za mkopo kutoka “OPEC Fund” zitatumika katika
utekelezaji wa mradi na Serikali itachangia asilimia 11.17 ya gharama ya ujenzi
kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano hayo.
Katibu Mkuu huyo
alieleza kuwa Skuli mpya ya Sekondari ya Kinuni ni ya ghorofa moja itakayokuwa
na madarasa 14, maabara 3, maktaba 1, chumba cha compyuta, ukumbi mkubwa, ofisi
za walimu pamoja na miundombinu kwa ajili ya wenye mahitaji maalum.
Alieleza kuwa ujenzi huo
umesanifiwa na unasimamiwa na Mshauri Muelekezi OGM CO. LTD ya Dar-es-Salaam
Tanzania na ujenzi unafanywa na Mkandarasi Saleem Construction LMT (SALCON)
kutoka Zanzibar ambapo ujenzi ulianza mwezi Oktoba mwaka 2017 na utakamilika
mwezi Januari 2019.
Dk. Hijja, alitumia
fursa hiyo kuwaomba wazee, wanafunzi na jamii yote kwa ujumla inayozunguka mazingira
ya skuli hiyo kuendelea kushirikiana katika kutunza majengo ya skuli hiyo na
rasilimali zake zote kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment