Habari za Punde

Balozi Seif Aweka Jiwe la Msingi Skuli ya Biashara Mpendae.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi akiweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Biashara Mpendae iliyopo Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa Mjini Magharibi.Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Riziki Pembe Juma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, akizungumza na Wazazi, Wananchi, Walimu na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mpendae baada ya kuweka jiwe la msingi la Skuli hiyo ikiwa ni Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Elimu Bila ya Malipo Zanzibar.
 Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Biashara Mpendae wakifuatilia matukio mbali mbali yalikuwa yakiendelea kwenye hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la Skuli yao. 
kikundi cha sanaa cha  Skuli ya Sekandari ya Biashara Mpendae wakitoa Igizo linaloelimisha jamii  kuthamini Watoto wenye Mahitaji Maalum katika kuwapatia Elimu kwenye hafla ya uwekajiwa jiwe la Msingi.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Sekta ya Elimu itaendelea kusonga mbele  kwa kasi kubwa iwapo Wananchi na Serikali yao wataendelea kushirikiana kwa karibu katika kuimarisha miundombinu ya Sekta hiyo.
Alisema Jamii lazima ielewe kwamba Matatizo yanayojichomoza kwenye Sekta hiyo muhimu kwa Maendeleo ya Taifa yanapaswa kutatuliwa kwanza bila ya kusubiri Serikali kama wanavyofanya baadhi ya Wadau wa Maendeleo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo alipoweka Jiwe la Msingi la Maendeleo ya Ujenzi wa Skuli ya Biashara iliyopo Mtaa wa  Mpendae ikiwa ni Wiki ya Elimu Bila ya Malipo inayoadhimishwa kila ifikapo Tarehe 23 Septemba ya kila Mwaka.
Alisema wakati Serikali Kuu na Watu Binafsi wakiwemo wadau wa Maendeleo wanajitahidi kujenga Madarasa mapya ni jukumu la Wanajamii kuthamini jitihada hizo kwa kutoa ulinzi wa kutosha wa mali na maeneo ya Skuli hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba wapo baadhi ya Watu wanajitia mshipa wa fahamu kuharibu kwa makusudi miundombinu ya Majengo ya Skuli katika baadhi ya Maeneo hapa Nchini.
“ Ni vyema sote tukatoa ulinzi wa kutosha wa Skuli zetu. Maeneo haya yakiharibika lazima tufahamu kwamba tunaharibikiwa sote na wala si Serikali pekee”. Alisema Balozi Seif.
Alielezea faraja yake kuona kuwa Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Skuli ya Sekondari ya Biashara Mpendae unafanyika katika mwezi ambao Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume  alitangaza Rasmi Elimu Bila ya malipo Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif alisema tangazo hilo liliondoa utoaji wa Elimu kwa njia ya ubaguzi ambao ulitawala wakati wa sultani ambapo matokeo ya ubaguzi huo katika sekta ya Elimu  Watoto wengi hasa Waafrika hawakupata fursa ya kupata Elimu kutokana na kutokuwa  na uwezo wa kulipia Elimu hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba Tangazo la Elimu bila ya Malipo lililotolewa Mnamo Tarehe 23 Septemba Mwaka 1964 ni Tangazo la Ukombozi wa Wananchi wa Zanzibar dhidi ya Ujinga, Maradhi, na Umaskini.
Alieleza kwamba mambo yote matatu dawa yake ni upatikanaji wa Elimu na hilo ndilo lililopewa kipaumbelena Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya kufanyika kwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 chini ya Jemedari wakie Mzee Karume.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Skuli hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Idriss Muslim Hijja alisema Serikali imeamua kusamehe Kodi kwa Vifaa vyote vitakavyotumika kwenye ujenzi wa Skuli hiyo ya Sekondari ya Biashara Mpendae.
Dr. Idriss alisema Wizara ya Elimu katika kuona changamoto za wanafunzi wa Skuli hiyo zinamalizika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeahidi kutoa  samanina vifaa vyote vya Skuli hiyo.
Alieleza kwamba Jengo hilo ni Heshimna na Sadaka kubwa kwa Mhisani wa Ujenzi wake unaofanywa na kusimamiwa na Mheshimiwa Ahmada Yahya Abdulwakil ambapo aliwaomba Wananchi wanayoizunguuka Skuli hiyo kushirikiana naye katika kuhakikisha inamalizika vizuri.
Akitoa salamu zake Mhisani wa Ujenzi huo Mheshimiwa Ahmada Yahya Abdulwakil alisema wazo la kupanuliwa Skuli hiyo ameliibua mnamo Mwaka 2015 kutokana na idadi kubwa ya Wanafunzi  inayopelekea upungufu mkubwa wa Madarasa waliokuwa wakipata.
Alisema Ujenzi huo ulioanza  Mnamo Tarehe 8 Oktoba mwaka 2017 unatarajiwa kumalizika Mwezi Januari mwaka 2019 ukikadiriwa kufikia gharama ya Shilingi Milioni Mia 800,000,000/- ambapo hadi sasa umeshafikia Shilingi Milioni Mia 600,000,000/-.
Mh. Ahmada alieleza kwamba kazi haikuwa rahisi kwani wako baadhi ya Watu waliobeza na wengine kukejeli lakini nia safi ndio iliyompa nguvu, hekima na busara zilizomuwezesha kuukabili ujenzi huo.
Akimkaribisha Balozi Seif  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  Mh. Riziki Pembe Juma  alisema kitendo alichofanya Mheshimiwa Ahmada Yahya Abdulwakil cha kutoa sadaka ya ujenzi wa Skuli ya Biashara  Mpendae ni cha Kizalendo na kinastahiki kuheshimiwa.
Waziri Riziki alimuomba na kumshauri Mfadhili huyo aliyetia nia ya  kuisaidia Serikali katika Miradi ya Maendeleo na Kijamii kwamba Serikali wakati wote itakuwa tayari kushirikiana naye katika kuona kazi aliyojitolea kuizawadia Serikali inakamilika vyema tena kwa wakati.
Skuli ya Sekondari ya Biashara iliyopo Mtaa wa Mpendae  itakapomalizika itakuwa ya Ghorofa  Mbili itakayobeba  Madarasa Tisa, Maabara, Vyoo, Afisi ya Mwalimu Mkuu, Chumba cha Walimu pamoja na Maktaba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.