Habari za Punde

Dk Shein: Viongozi wa dini na kijamii wana dhima kubwa kuwaelimisha waumini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata Utepe kuashiria kuufungua Rasmi Msiki wa Ijumaa wa Chuini uitwao Al –Marhuma Fatma Bint Khalifa Masjid kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al – Hajj Dr. Ali Mohamed Shein.
Balozi Seif akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Mtaa wa Chuini Wilaya ya Magharibi “A” wakati wa ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa baada ya kumaliza sala ya Ijumaa.
baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wakifuatilia matukio ya harakati ziliyojiri wakati wa ufunguzi wa Msiki wa Ijumaa wa Chuini uliofunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al – Hajj Dr. Ali Mohamed Shein.
Sheikh Othman Maalim akitoa taaluma kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu walioshuhudia Ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa wa Chuini uyliopewa jina Al –Marhuma Fatma Bint Khalifa Masjid kutokana na mchango wake mkubwa.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis,. OMPR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al- Hajj Dr. Ali Mohamed Shein  alisema Viongozi wa Dini pamoja na wale wa Kijamii wana dhima ya kuendelea kuwaelimisha Waumini na Wananchi wao ili washibe takwa itakayowezesha kupambana na vitendo  viovu ndani ya Jamii huku wakitambua kwamba vitendo viovu ni kinyume na mafundisho ya Dini.
Alisema Jamii nchini hivi sasa inakabiliwa na mitihani mbali mbali inayoashiria kuporomka kwa Maadili kunakotokana na kundi kubwa la Watu hasa Vijana kujitumbukiza katika matumizi ya Dawa za Kulevya sambamba na vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia unaowakumba Wanawake na Watoto.
Dr. Ali Mohamed Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi  wa Msikiti wa Ijumaa baada kukamilika ujenzi wake uliopo Mtaa wa Chuwini Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema Uislamu unafundisha umuhimu wa kuzingatia nidhamu, maadili mema pamoja na kutii sheria zinazoiongoza Jamii. Hivyo kwa kuzingatia masuala hayo Jamii ina wajibu wa kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali kwa vile yana nia njema ya kuleta ustawi wa Jamii hiyo.
Rais wa Zanzibar alisema  Raia wema na hata wale wakorofi ni wajibu wao kuyatii na kuyatekeleza kwa moyo wa Kizalendo maelekezo  yanayotolewa na Viongozi wao Wakuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Taasisi za Serikali na hata Masheha Mitaani mwao ili kuimarisha Heshima ya Taifa.
Katika Hotuba yake hiyo Dr. Shein aliwashukuru Watu wote waliochangia kwa namna tofauti kuufanikisha Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Chuwini Jengo linalopendeza likionekana kuwa limejengwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya sasa ya kupata mahali pazuri pa kuendeleza harakati za Ibada zinazochangia pia kurejesha Maadili ya Jamii.
Al –Hajj Dr. Ali Mohamed Shein  alieleza kwamba Ujenzi wa Msikiti ni moja kati ya amali muhimu na yenye ujira mkubwa kwa Muumini aliyeamua kuitekeleza kwa agizo la Mwenyezi Mungu ambayo mja huyo  huendelea kupata fadhila zake hata pale anapoondoka Duniani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alifahamisha kwamba Muumini anapoamua kujenga msikiti anadhihirisha imani na uchamungu wake kwa kutii amri ya Mwenyezi Mungu na kutoa miongoni mwa neema ambazo ameruzukiwa na Mola wake kwa kufanya mambo ya kheri kama alivyoamrisha Mola wa Viumbe wote.
Alieleza kwamba ni vyema kwa Waumini wote wawe na utamaduni wa kukimbilia na kuhimizana kuzitumia neema walizopewa na Muumba wao katika masuala ya kheri kwani si busara kujilazimisha kutoa fedha taslim wakati hazipo, bali hata kutoa Viwanja kwa ajili ya ujenzi au usafi wa majengo hayo ya Ibada.
“ Kwa hakika kila Mtu aliyeshiriki katika kukamilisha ujenzi wa Msikiti huu ametoa sadaka ambayo siri yake kubwa ni mja kujiepusha na ubinafsi na kujipambanua katika ubora wa imani na upendo kwa wengine”. Alisema Dr. Shein.
Alisema kwamba  mafundisho ya Uislamu yanawahimiza Waumini kutoa sadaka kwani ni kitendo muhimu cha ihsani chenye kuitakasa nafsi ya Muumini na kumuelekeza Mtu kwenye Imani thabiti.
Alielezea matumaini yake makubwa kwamba msikiti huo utaendelea kuwa kitovu muhimu cha Waumini kufundishana mambo ya Dini, kwa kupeana mawaidha na kuendesha darsa mbali mbali, harusi pamoja na maandalizi ya mazishi kwa wale ambao Mola ameshawahitaji.
Rais wa Zanzibar alitahadharisha kamwe Nyumba hiyo ya Muungu isitumiwe kuwa Jukwaa la masuala ambayo hayana mnasaba na msikiti au kuwa chanzo cha migogoro, mivutano na uhasama kama inavyotokea katika baadhi ya Misikiti hapa Nchini.
Aliwanasihi Waumini wa Msikiti huo kuziepuka aina zote za uharibifu ili ubora wa jengo hilo linaloshuhudiwa uzuri wake hivi sasa uweze kudumu kwa kipindi kirefu sambamba na  kukumbusha Uongozi wa Msikiti huo kuhakikisha kwamba utunzaji mzuri unatekelezwa kwa niaba ya Waumini wote.
Akizungumzia neema ya Ardhi waliyoruzukiwa Wazanzibari Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi kuacha kujenga katika maeneo ya mabondeni pamoja  na uuzwaji holela wa Viwanja kwa ajili ya Ujenzi wa Nyumba za kudumu katika Eka Tatu Tatu Walizopewa kwa kuendeleza Kilimo.
Alisema kwa bahati mbaya au hata makusudi wapo baadhi ya Wananchi wakiwemo wa Mitaa ya Chuwini, Mbuzini na Maeneo jirani wanaendelea kujenga kati kati ya mabonde ya Mpunga wakati wengine wakikata miti ovyo ikiwemo Minazi kwenye eka na kuuza Viwanja.
Dr. Ali alionya kwamba jambo hilo ni kinyume na Sheria na Taratibu zilizowekwa za matumizi ya neema ya Ardhi ambapo likiendelea linaweza kuleta matokeo mabaya na pia ni mfano wa matumizi mabaya ya Ardhi.
Alisema zipo aya mbali mbali katika Vitabu vya Dini zinazohimiza juu ya umuhimu wa kuitumia vyema ardhi iliyopo kama ambavyo Serikali kwa Awamu zote zilizopita za Uongozi imekuwa ikiyazingatia.
Alieleza kwa mnasaba huo Serikali inaendelea kuwasisitiza Wananchi wote kuzingatia Sheria na Mipango Miji, ili Ardhi iweze kutumiwa kwa manufaa ya kudumu ikiwemo kujenga panapostahiki na kuitumia nyengine kwa shughuli za uzalishaji kama Kilimo kwa dhamira ile ile ya Muasisi wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kugawa Eka Tatu bila ya ubaguzi.
Kuhusu suala la Amani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al – Hajj Dr. Ali Mohamed Shein alisema lulu ya Amani iliyopo hapa Nchini ndio inayowapa fursa Waumini kufanya Ibada zao kwa utulivu.
Dr. Shein alisema hatua za Maendeleo ya haraka kamwe hazitafikiwa wala kupatikana iwapo Amani ya Nchi itashindwa kulindwa kwa pamoja kati ya Jamii na Serikali kwa ujumla.
“Tumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Viumbe vyote kwa kutupa neema hii ya Amani na sisi ni jukumu letu sote kuendelea kuidumisha kwa nguvu zetu zote”. Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Alisema Wananchi ni vyema wakajifunza kwa mifano kutoka Mataifa mengine ambayo Waumini wa Dini wanakosa utulivu katika kufanya Ibada zao mbali mbali kutokana na kukosekana kwa Amani.
Mapema katika Risala yao Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi wa Mtaa wa Chuwin Mmoja miongoni mwa Makhatib wa Msikiti huo Sheikh Moh’d Ame Mgeni alisema Ujenzi wa Msikiti huo wa Ijumaa ulioanza kujengwa  mnamo Tarehe 24 Novemba Mwaka 2017  hadi kukamilika kwake  umepitia katika hatua mbali mbali.
Sheikh Moh’d alisema ujenzi huo umekuja kufuatia ongezeko  kubwa la Waumini wa Eneo hilo ambao mwanzoni Msikiti huo ulichukuwa Waumini 30, baadae ukajengwa na kuhudumia Waumini 300 walioweza kusali wakati hivi sasa umemalizika kujengwa ukiwa na uwezo wa kusaliwa na Waumini wasiopungua Elfu 1,000 kwa wakati mmoja.
Aliwaomba Waislamu waliojaaliwa uwezo na Allah {SW} kuendelea kusaidia ujenzi wa nyumba za Ibada katika maeneo mbali mbali  hapa Nchini kwa lengo la kuendeleza Dini.
Waumini hao pia wakawaomba Waislamu mahali popote pale kujitolea kusaidia ujenzi wa Madarasa yaliyopo nyuma ya Msikiti huo ambayo yalivunjwa kutokana na upanuzi wa Bara bara pamoja na Janareta la hakiba ambalo litakuwa mbadala wa umeme endapo utazimwa kwa kuendesha shughuli za Msikiti huo.
Msikiti wa Ijumaa wa Mtaa wa Chuwini umepewa Jina la Al- Marhuma Fatma Binti Khalifa Masjid kutokana na mchango mkubwa wa Marehemu Bibi Fatma wakati wa uhai wake alipokubali kuujenga Msikiti huo tokea mwanzo hadi kukamilika kwake.
Akitoa mawaidha kuthibitisha ubora wa mali katika kuitolea sadaka Shekh Othman Maalim alisema kila Muumin anapaswa kujitathmin namna gani anaitumia mali yake halali aliyochuma  katika kutoa zaka na sadaka.
Sheikh Othman alisema ujenzi wa misikiti, Madarasa, uchimbaji wa visima na misaada kwa mafukara na maskini ni miongoni mwa amali zinazoendelea kumsaidia Muumini hata kama ameshatangulia mbele ya haki.
Alitahadharisha kwamba mali inayolimbikizwa katika majengo ya Benki, na Biashara hayatamsaidia mchumaji katika kuelekea kwenye kheir na matendo yanayomridhia Mwenyezi Muungu.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza na Waumini na Wananchi wa Mtaa wa Chuwini Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi aliinasihi Jamii ya Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kukumbushana katika mambo ya kheir ili dhama ya kulipwa mema iwathibitikie wakati wakisubiri malipo mema wakati watakaporejea kwa Mola wao.
Sheikh Saleh Omar Kabi alisema masuala ya kukumbushana miongoni mwa Waumini na Wananchi ni jambo la msingi na la Ibada kwa vile linaendelea kuleta takwa, mapenzi na ihsani ndani ya Jamii katika ardhi tukufu ya Mwenyezi Muungu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.