Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Aendelea na Ziara Yake na Kuhutubia Mkutano wa Hadhara Kata ya Kazuramimba.Mkoani Kigoma.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipungia wananchi wakati alipokuwa akiwasili kwenye uwanja wa mkutano tayari kuhutubia mkutano wa hadhara jana jioni katika kata ya Kazuramimba,wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 
Wananchi wa Kata ya Kazuramimba.Mkoani Kigoma wakati wa mkutano wa hadhara na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu kabla ya kuhutubia mkutano huo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakazi wa mkoa wa Kigoma kupima afya zao kwani kufanya hivyo kutawasaidia kujitambua na pia kutaisaidia Serikali kuwa na takwimu kamili za afya na kurahisisha utoaji huduma kwa waathirika.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano wa Kazuramimba, wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ikiwa siku ya tatu ya ziara yake ya kukagua na kuhamasisha shughuli za kimaendeleo.
Pia alihimiza wakina mama kuzingatia lishe bora kwa watoto kuepuka athari za udumavu “Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa uzalishaji chakula ni mkoa ambao hautuumizi kichwa katika kutafuta chakula cha Watanzania, unajitosheleza kabisa lakini kuna tatizo la lishe duni hasa kwa watoto”alisema Makamu wa Rais.
Takwimu zinaonyesha mpaka mwaka 2015 kiwango cha udumavu katika mkoa wa Kigoma ni asilimia 37.9
Makamu wa Rais amewaambia wakazi wa Kigoma kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa hasa kwa wageni wanaotoka nchi jirani ya Congo ili Taasisi za Serikali zifanye kazi yake haswa katika kuzuia waathirika wa ugonjwa wa Ebola kuingia nchini.
“Mgeni anapokuja semeni amekuja mgeni ili taasisi ya serikali zifanye kazi yake,kazi ya kuhakikisha mgeni aliyeiingia yupo msafi anakaa wapi, ataishi na nani, hatukatai wageni lakini toeni taarifa tuwajue na hii ni kwa faida yetu kama Taifa lakini yenu kama wana Kigoma, wana Uvinza ni kwa faida yenu wenyewe tunawalinda na maradhi, tunawalinda na uharamia,tunawalinda na mambo chungu mzima ya kiusalama wenu kwa hiyo ndugu zangu msifiche wageni wanapokuja tuambieni ili tuweze kuchukua zinazostahili”.  Alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya awamu ya tano imeamua kutumia pesa zake za ndani kwenye vipaumbele vikubwa vya Kitaifa katika ununuzi wa ndege, umeme wa kudumu na uhakika, kupeleka maji kwa wananchi, elimu bure pamoja na kuboresha huduma za afya na kuhakikisha madawa yanapatikana kwa urahisi.

Aidha, Mkuu wa mkoa wa Kigoma aliwaambia wananchi wa mkoa huo kuwa Kodi zinazokusanywa na Serikali ndizo zinajenga miundo mbinu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.