Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt.Ali Mohamed Shein Atembelea Eneo la Ujenzi wa Mahkama Kuu ya Zanzibar Tunguu leo.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, akitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Jengo la Mahkama Kuu ya Zanzibar Tunguu, akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Khatib Hassan Khatib, wakati wa ziara yake leo.

Na. Rajab Mkasaba Ikulu. 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafuata utawala bora na haiko tayari kupambana na wananchi wake na wala haitovumilia kuwaona baadhi yao wakivunja sheria ikiwemo kuvamia na kujenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya ziara yake fupi ya kuliangalia eneo lililopimwa na kutengwa maalum kwa ajili ya ujenzi wa Mahkama Kuu ya Zanzibar lenye ukubwa wa hekta 4.3 lililopo Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambalo liko mkabala na eneo la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Alisema kuwa Serikali haitokuwa tayari kuwaona baadhi ya wananchi wake wakivamia kwa kujenga katika maeneo yaliotengwa na Serikali kwa shughuli nyengine za kimaendeleo bila ya kufuata taratibu zilizopo.

Aliongeza kuwa katika eneo la Tunguu ambalo limetengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kupitishwa na kukubaliwa na Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) pamoja na ujenzi wa jengo jipya la Mahkama Kuu ya Zanzibar.

Alieleza kuwa kujitokeza kwa baadhi ya wananchi hao na kuvamia eneo hilo si jambo la busara wala halivumiliki na kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi wote wakiwemo wa Mkoa wa Kusini Unguja kutambua kuwa eneo hilo ni lao na kuwataka waisaidie Serikali katika kulilinda kwani ni la wananchi wote wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa SUZA pamoja na uongozi wa Mahkama Kuu kila mmoja kulilinda eneo lake alilopewa ili kuepuka uvamizi.

Alisisitiza kuwa mipango yote iliyopangwa na Serikali ikiwa ni pamoja na ujenzi huo wa jengo jipya la Mahkama Kuu mpya ya Zanzibar, uendelezaji wa majengo ya Chuo cha SUZA pamoja na barabara iliyoanzia Mwanakwerekwe hadi Tunguu ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa ardhi yote ni mali ya Serikali ambayo yeye ndio anayeisimamia hivyo hakuna mwananchi hata mmoja ambaye anaweza kujimilikishwa na kutumia ardhi bila ya kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Alieleza kuwa wananchi waliojenga katika eneo hilo ambalo limetengwa kwa shughuli hizo maalum hawakujenga kwa mujibu wa sheria kwani hawakuwa na hati ya kujenga katika eneo hilo lakini hata hivyo walipewa maelezo ya kutojenga katika eneo hilo kwa muda mrefu.

Alieleza kuwa hata hivyo walikaidi agizo hilo na kutumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kuchukua juhudi za kuwaondoa wale wote waliovamia katika eneo hilo jambo ambalo hakupenda lifikie hatua hiyo.

“Serikali haijatoa hati ya kutumiwa eneo hilo….hivyo ilibidi lazima waaondoshwe ili mambo mengine yaendelee”,alisisitiza Dk. Shein katika maelezo yake mara baada ya kulitembelea eneo hilo na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Mahkana, SUZA na Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa azma yake ni kujengwa jengo la Mahakama Kuu ya Zanzibar katika kipindi chake cha uongozi na kuizindua kabla ya kumaliza madaraka yake ya Urais huku akieleza kuwa kwa upande wa eneo la SUZA litaanza kujengwa hivi karibuni.

Kwa upande wa barabara inayotoka Mwanakwerekwe hadi Tunguu ambayo kwa sasa imeishia katika eneo la Fuoni Kituo cha Polisi, Rais Dk. Shein aliwaeleza wananchi waliofika katika eneo hilo kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuijenga na kuimaliza katika kipindi cha mwaka ujao.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alisema kuwa Zanzibar inaongozwa kwa misingi ya Utawala Bora na mambo yote yanayofanywa yanafanywa kwa ajili ya wananchi na kwa faida ya wananchi ikiwemo kupata haki zao.

Alisema kuwa mbali ya jengo hilo la Mahkama pia, patajengwa Skuli ya kuwafundisha wanasheria (School of Law), pamoja na kuongezwa majengo ya Chuo Kikuu cha SUZA, huku akisisitiza kuwa Serikali inafanya mambo yake kwa faida ya wananchi wote na si kwa mwananchi mmoja mmoja.

Mapema Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Abdala Juma Mabodi alimpongeza na kumshukuru Rais Dk. Shein kwa uongozi wake shirikishi kutokana na kuwashirikisha wananchi na viongozi wa sekta mbali mbali za Serikali katika ziara yake hiyo.

Mabodi aliongeza kuwa hatua hiyo ya Rais Dk. Shein ya kuhakikisha jengo la Mahkama Kuu linajengwa, uendelezaji wa Chuo Kikuu cha SUZA pamoja na ujenzi wa barabara hiyo ni  utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.