Habari za Punde

Balozi Seif mgeni rasmi Siku ya Walimu duniani Michenzani Square

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud akiyapokea Maandamano ya Walimu kuadhimisha Siku ya Waalimu Duniani hapo Michenzani Square.

 Baadhi ya Walimu walioshiriki mbio za Magunia kuadhimisha siku ya Walimu Duniani kwa hapa Zanzibar zimefikia kilele chake katika Uwnja wa Kumbu kumu ya Mapinduz{Mapinduzi Square} Michenzani Mjini Zanzibar.
 Baadhi ya Walimu wa Zanzibar walioshiriki Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Waalimu Duniani hapo Mapinduzi Square wakifuatilia matukio mbali mbali yalaiyokuwa yakifanyika katika sherehe hizo
 Balozi Seif akimkabidhi zawadi Mshindi wa Pili wa mashindano ya mbio za Magunia Mwalimu Shariuf Mohamed kutoka Skuli ya Bwefum kwenye kilele cha Siku ya Waalimu Duniani hapo Mapinduzi Square
 Balozi Seif akizungumza na Walimu kwenye Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Waalimu Duniani zilizofikia kilele chake katika Uwanja wa Mapinduzi Square Michenzani. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Elimu Mh. Riziki Pembe Juma, Katibu Mkuu wa ZATU Maalim Mussa Omar Tafurwa, na kushoto ya Balozi Seif ni Rais wa ZATU Maalim Seif Mohamd Seif na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud.
 Balozi Seif aliyekaa kati kati Vitini akiwa katika Picha ya pamoja na Uongozi wa Chama cha Waalimu ZATU mara baada ya kukamilika kwa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Waalimu Duniani hapo Mapinduzi Square Michenzani.
Balozi Seif akiagana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma baada ya kukamilika kwa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Waalimu Duniani hapo Mapinduzi Square Michenzani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha kwamba si vyema na ni dhambi kubwa isiyosameheka hata kidogo kuona wapo baadhi ya Waalimu wachache Nchini wanaendeleza tabia ya kuichafua fani ya Ualimu na kusahau jukumu lao la ulezi wa Wanafunzi Maskulini.
Alisema haifai na haitakiwi kwa Mwalimu kutembea, kumbaka au kumpa ujauzito Mwanafunzi vitendo ambavyo ni aiba, fedheha  na kashfa kubwa kwa Watu ambao wameaminiwa kupewa Ulezi wa kutoa Elimu kwa Wana wa Taifa wakifanya vitendo vya ajabu visivyokubalika katika Jamii.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo baada ya kuyapokea Maandamano ya Waalimu kuadhimisha Siku ya Waalimu Duniani yaliyofanyika Mapinduzi Square kwenye Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi uliopo Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali na Jamii kwa ujumla hushtushwa na kupatwa na fadhaa pale inapopata Habari za Mwalimu kujihusisha na mambo yaliyo kinyume na Maadili yake wakati kinachotarajiwa kutoka kwa Mwalimu ni kile kinachomfanya aitwe Mwalimu na si vyenginevyo.
“ Huwa tunakosa amani kabisa katika nafsi yetu kusikia Mwalimu kamdhalilisha  au kumnyanyasa Mtoto au Mwanafunzi wake ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Aliiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar kwa kushirikiana pamoja na Wana Jamii wote kuwafichuwa Walimu wanaokiuka Miiko na Maadili ya Kazi na hatimae kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Balozi Seif  aliwapongeza Walimu wote walioshiba Maadili ya fani yao kwa kujiheshimu na kutambua kuwa wao ndio Kioo na kigezo chema kwa Wanafunzi na Jamii nzima Mitaani.
Alieleza kwamba Ualimu ni moja ya fani muhimu kwa Maendeleo ya Taifa lolote lile Duniani, ikiaminika kwamba kila Mwana Jamii anatambua umuhimu wa michango ya Walimu katika maisha yake ya kila siku iliyojenga misingi iliyoliwezesha Taifa kufikia hapa lilipo.
Balozi Seif alifahamisha wazi  kwamba azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  ni kuimarisha Sekta ya Elimu wakati wote  na kuhakikisha kuwa Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar  wanapata huduma ya Elimu bila ya Ubaguzi wa rangi, kabila au Dini.
Alisema hilo ndilo lengo la Chama cha Afro Shirazy Party na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 chini ya Muasisi na Jemedari wa Mapinduzi hayo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume aliyetangaza Elimu Bila ya Malipo Mnamo Tarehe 23 Septemba Mwaka 1964.
Alisema tangazo hilo lililofuatiwa na mfumo sambamba na muongozo wa Elimu ilikuwa ni Ukombozi kwa Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar ambao wengi wao hawakuwa na uwezo wa kujilipia na kupata Elimu wakati wa kutawaliwa.
Akizungumzia Uwekezaji katika Sekta ya Elimu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali hivi sasa inatumia wastani wa asilimia 20% ya Bajeti yake katika uwekezaji wa Rasilmali ndani ya Sekta ya Elimu hapa Nchini.
Balozi Seif alisema Ujenzi wa Skuli za Ghorofa katika Wilaya zote Unguja na Pemba ni miongoni mwa Mikakati ya Uwekezaji huo ambao sio tu utaongeza mazingira mazuri ya kuvutia kwa Wanafunzi na nafasi za kutosha bali pia zitapunguza maeneo ya Ardhi yatumikayo kwa ujenzi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni kutaratajiwa kupokea vikalio kwa ajili ya  Maskuli ya Zanzibar kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.
Alisema vikalio hivyo vinatarajiwa kumaliza changamoto kubwa ya upungufu wa thamani katika Majengo ya Skuli mbali mbali za Unguja na Pemba ambayo ilikuwa ikiathiri mazingira ya ufundishaji wa Wanafunzi hasa wale wa Skuli za Msingi.
Akisoma Risala ya Walimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Zanzibar             {ZATU } Maalimu Mussa Omar Tafurwa alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuasisiwa kw Chama cha Waalimu Zanzibaf Miaka 16 iliyopita.
Maalim Tafurwa alisema umiliki wa Majengo Mawili ya Chama hicho pamoja na ujenzi wa Jengo la Ghorofa Kisiwani Pemba ni uthibitisho wa mafanikio ya Chama hicho kinachozingatia Sera, Mikakati ya Taifa pamoja  na Maazimio ya Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa {UNESCO} na lile na Kazi Duniani {ILO} yaliyofikiwa Mjini Paris Nchini Ufaransa Mwaka 1966.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Walimu Zanzibar alisema zipo baadhi ya changamoto zinazokwaza Waalimu katika utekelezaji wa majukumu nyao ya kuwafunda Wanafunzi katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Maalim Tafura alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na upungufu wa Walimu katika baadhi ya Skuli hasa Mikoani na Vijijini, ucheleweshaji wa Mishahara ya Walimu hasa kutokana na mfumo Mpya wa Ugatuzi unazozipa Mamlaka Manispaa na Halmshauri za Wilaya kusimamia Elimu ya Maandalizi na Msingi.
Maalim Mussa Omar Tafurwa kwa niaba ya Wanachama wa chama Cha Waalim Zanzibar wanaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya usimamizi wa Rais wake Dr. Ali Mohamed Shein kwa hatua za kuimarisha Sekta ya Elimu hapa Nchini.
Alisema juhudi hizo za Serikali zimekuwa zikishuhudiwa na Jamii ya Kitaifa na Kimataifa za namna miundombinu ya Sekta hiyo inavyozidi kuchanjambuga katika muelekeo wa uimarikaji wa Sekta hiyo muhimu kwa Uchumi wa Taifa.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika hadhara hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuchukuwa hatua za kupunguza Madeni ya muda mrefu yaliyokuwa yanawahusu Walimu.
Waziri Riziki alisema madeni hayo ya tokea Miaka ya 2011 na 2012 yaeanza kulipya kuanzia Mwaka 2013 hadi mwaka 2017 yakienda sambamba na ulipwaji wa malimbikizo ya posho za likizo.
Mh. Riziki aliwaeleza Walimu hao kwamba Serikali itaendelea kulipa Madeni hayo kadri ya hali ya Uchumi utakavyoruhusu ambapo kwa sasa tayari zaidi ya shilingi Milioni 500,000,000/- zimeshatolewa na na Serikali kulipa malimbikizo ya Maposho ya Walimu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali aliuomba Uongozi wa Chama cha Waalimu Zanzibar {ZATU} kutomtetea Mwalimu au Mwanachama wake ambaye atahusika na ukiukaji wa maadili ya kazi yake hasa suala ovu la udhalilishaji Wanafunzi ambalo limekuwa kero katika Jamii.
Katika kilele cha madhimisho hayo ya Siku ya Waalimu Duniani Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi zawadi kwa Washindi wa shindano la mbio za Magunia lililoshiorikisha Walimu kutoka Skuli mbali mbali hapa Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.